tamasha

Majaliwa
Tunduma 1995

Ndani ya ukumbi wa mahakama ya mwanzo Karoleni watu walijaa pomoni. Ukumbi wenyewe si ukumbi hasa. Ni chumba kidogo cha wastani ndani ya jengo ambalo awali lilikuwa gereji. Watu walifurika kushuhudia kesi ya kijana Majaliwa. Majaliwa alifikishwa mahakamani hapo akituhumiwa kuiba. Hata hivyo wizi wenyewe haukufanikiwa kwani alikamatwa na wakazi wa nyumba hiyo aliyojaribu kuiba wakati ndiyo akijiaandaa kuondoka na kiroba cha mahindi kiasi cha debe moja ambacho alijaribu kukiiba ndani ya nyumba hiyo.

Ukimtazama Majaliwa namna alivyonuna pale mahakamani waweza angua kicheko badala ya kumwonea huruma. Kununa kwake kulitengeneza sura ya peke yake ukijumlisha na vidonda na nundu kutokana na kipigo alichokipata mara baada ya kukamatwa. Weusi wake na para alilonalo kichwani pake vilitengeneza taswira halisi ya kibaka mzoefu. Macho yake yalikuwa makali mithili ya paka.

Muda wote huo kabla ya kesi kuanza, Majaliwa hakuacha kupiga jicho pande zote za chumba hicho kana kwamba anajaribu kuyasoma mawazo ya watu hao waliohudhuria ambao hata hivyo hawakutosha mle ndani na wengine kulazimika kusimama nje ya chumba hicho. Akili ya Majaliwa ilikazana kuwamaki viherehere wote ili mara kesi yake itakapokwisha, basi hao ndiyo aanze nao kulipa kisasi.
Mara macho yake yanagongana na macho ya mama yake mzazi aliyekuwa akilia muda wote kwenye kona ya chumba hicho cha mahakama ya mwanzo. Majaliwa aliyakwepesha haraka macho yake kwani angeweza kuwa jasiri katika mambo mengine yote magumu ya ulimwengu, lakini siyo kutazamana na mama yake katika wakati kama huu. Alihisi macho ya mama yake yalikuwa yakimsuta. Alihisi macho ya mama yake yakibeba ujumbe mzito sana kumkumbusha shida tele ambazo mama yake alikubali kukumbana nazo katika kujitahidi kumpa malezi bora ambazo hata hivyo ziligonga mwamba.

Pamoja na umasikini wake, mama Majaliwa alijitahidi kupika pombe ili walau amudu kumshonea sare za shule mwanawe wa pekee Majaliwa. Pombe ikikosa wateja, angefanya vibarua vya kuchota maji kutoka karavatini na kwenda kuyauza maeneo ya Kilimanjaro ama Mashineni ili aweze kumudu kulipia karo ya shule ya kijana wake Majaliwa. Hayo yasingemtosha, mama Majaliwa angepika maandazi na kwenda kuyauza Tazara nyakati za treni za abiria ili kuhakikisha mlo wa kijana wake wa pekee ambaye hakuwahi kumwona tena baba yake mara baada ya kufanya naye mapenzi siku moja ambayo alinasa mimba ya Majaliwa.

Akiwa kigori wa miaka kumi na tano, Sikitu alikuwa akifanya vibarua vya kuchota maji kwa ajili ya waosha magari makubwa ya mizigo. Magari hayo ambayo husafirisha bidhaa zake kati ya Tanzania na nchi za jirani Zambia, Kongo na Zimbabwe hupaki mjini hapo Tunduma mamia kwa mamia yakisubiri taratibu za forodha ili yavuke mpaka na kuingia nchini Zambia. Kutokana na shida ya maji mjini hapo Tunduma, waosha magari hulazimika kununua maji ya kwenye ndoo ambayo huchotwa mbali huko mabondeni.

Sikitu hakuipenda kazi hiyo ngumu iliyokuwa na maslahi madogo mno. Alilazimika kuifanya kutokana na ugumu wa maisha uliomwandama. Alikuwa akiishi na bibi yake eneo la Migombani baada ya wazazi wake wote wawili kufa kifo cha kutatanisha akiwa bado mdogo sana. Wengine husema walifariki kwa kurogwa, na wengine husema walipatwa na gonjwa la ajabu. Sababu za kifo cha wazazi wake hazikumgusa, zaidi ya hali duni ya maisha iliyomwandama.
Awali hakupenda kufanya hivyo. Lakini baadaye akajikuta akianza kujihusisha mahusiano ya kimapenzi na madereva na matingo wa malori hayo makubwa. Ilikuwa ndiyo fasheni kwa mabinti wanaochipukia kufanya hivyo wakizuzuka na mikate kutoka Dar es Salaam ama vipodozi kutoka Zambia na Kongo.

Jua likishazama, Sikitu alienda eneo hilo la Kilimanjaro ambalo liliitwa hivyo kutokana na baa ya Kilimanjaro iliyokuwa maarufu sana enzi hizo. Atakunywa bia mbili akiwa na shefa wake aidha brazameni wa Kitanzania, ama wa Kizambia ama wa Kikongo alimradi siku haikupita kavu. Alitembea na wanaume wa tofauti tofauti. Maisha yakazidi kusonga mbele.
Mara akapata ujauzito. Kwa hakika hakumfahamu aliyempa ujauzito huo. Hakuhitaji kuzaa kwa wakati huo. Hata hivyo jitihada za kuitoa mimba hiyo ziligonga mwamba. Hatimaye akajifungua toto la kiume lenye afya njema. Akamwita mtoto wake Majaliwa. Siku za utoto wa Majaliwa hazikuwa njema. Aliugua mara kwa mara. Mungu si Athumani, akamjalia akakua vema na afya yake njema.

Sikitu ama mama Majaliwa akakomaa akili kutokana na ugumu wa maisha. Akazidi kuchakarika kumlea mtoto wake aliyeonesha kuanza utukutu akiwa angali mdogo. Mtoto ambaye hakufahamu kama ni Mtanzania, Mzambia, Mkongo ama Mkenya ama vinginevyo. Majaliwa akapelekwa shule. Pamoja na kukazaniwa sana kusoma shule na mama yake, hakikuwezekana kitu. Majaliwa akaacha shule akiwa darasa la nne pale shule ya msingi Maporomoko. Kikubwa kilichomsukuma kuacha shule ni biashara ya kuuza biskuti maeneo ya Customs na Tazara nyakati za treni za abiria.

Biashara haikuwa nzuri kwa Majaliwa kutokana na kutokuwa na mtaji. Taratibu akajifunza tabia ya udokozi na hatimaye wizi. Mama yake hakufahamu kijana wake amekuwa mdokozi. Tabia ya Majaliwa ya kutokuwa mwongeaji ilimtuma mama yake kuendelea kuamini kijana wake ni kijana asiye na makuu wala tamaa na vitu vilivyo nje ya uwezo wake.

Majaliwa mwenyewe alianza kuipenda sana kazi yake mpya ya wizi. Akawa kibaka mzoefu lakini akiwa na bahati ya kutokamatwa. Mara zote mwili wake mdogo ulimweka mbali na tuhuma za moja kwa moja zaidi ya hisia tu. Mwenyewe alilifahamu hilo. Akawa mjanja sana. Wenzake wakambatiza jina la Sungura kutokana na kujaliwa maarifa na akili ya kufikiri haraka. Wenzake walipenda kumtania kama angeamua kuzingatia masomo na shule, haikosi angekuja kuwa hata profesa. Yeye aliupuuzia sana utani unaomhusisha na mambo ya shule kwani shule hakuipenda kabisa moyoni mwake. Mateso ya kwenda shule na njaa mara nyingi, ama kuvaa kaptula iliyotoboka matakoni huku matako hayo hayo yakicharazwa bakora nyingi kwa kosa dogo tu la kuchelewa shule ukizingatia umbali wa shule na nyumbani ulikuwa ukijulikana vema.

Leo hii akiwa amesimama kizimbani katika mahakama hii ya mwanzo, akalikumbuka tukio lililomfikisha hapo. Lilitokea mwezi moja uliopita alipoingia nyumbani kwa mtu maeneo ya Maporomoko na kujaribu kuiba. Uwani mwa nyumba hiyo kulianikwa mahindi yaliyotoka kuvunwa. Wenyewe waliyaanika uwani hapo wakiwa wanaendelea na mchakato wa kuyapiga na kuyahifadhi vema.

Majaliwa alifanikiwa ndani ya uwa huo uliozungushiwa wigo wa matete kwa kukata mahali. Kwa akili yake kutokana na eneo lote kutawaliwa na kiza, aliamini wote wamelala. Kwa mbali alisikia sauti ya redio ikitumbuiza muziki wa taratibu kwa sauti ya chini sana. Akafahamu hiyo ni dawa ya usingizi kwa watu wengi.

Akaanza kuyakusanya mahindi taratibu kwa umakini mkubwa na kuyahifadhi ndani ya kiroba alichokuja nacho. Alipokijaza akakivuta taratibu hadi nje ya wigo huo ambako rafiki yake alikuwa akimsubiri. Akamkabidhi na kuchukua kiroba kingine kitupu na kuingia ndani kuendelea na zoezi lake. Akaanza kukijaza kwa utulivu wa hali ya juu huku akijiamini kabisa.
“Unafanya nini wewe?” Swali hilo liliendana na teke la mgongoni pale alipokuwa amechuchumaa akizoa mahindi.
Akili ikamruka ghafla.

Akayumba kiasi cha kutaka kudondoka. Wakati akijaribu kufikiri imekuwaje akashitukia amepigwa teke jingine. Teke hilo ndilo lililomzindua. Akamtazama aliyempiga. Akagundua ni kijana wa kawaida tu. Akili yake ikafanya kazi haraka. Akamtishia kijana huyo jisu alilokuwa nalo. Kijana huyo akatishika. Majaliwa akapata upenyo na kutoka nduki.
Kijana yule akaanza kumfukuzia huku akipuliza filimbi. Ilikuwa ni majira ya saa nane usiku lakini watu wakatoka majumbani mwao na kuanza kumfukuzia Majaliwa aliyekuwa akizimudu vema mbio mithili ya mwanariadha wa Marathon.

Kama si tuta la viazi lililomchanganya Majaliwa na kumfanya adondoke, basi asilani abadani wafukuzaji wale wasingemkamata kama ambavyo hawakuweza kumkamata mwenzake.
Majaliwa akapokea kipigo kitakatifu kutoka kwa wananchi. Walimcharaza bakora huku wengine wakimpiga mateke alimradi kila mtu aliyekerwa na tabia za vibaka akitoa adhabu kwa mtindo wake. Busara ya mzee mmoja tu ndiyo iliyomwoka Majaliwa asichomwe moto wakati tayari alishamwagiwa galoni zima la mafuta ya taa mwilini mwake huku akilia kwa lugha zote alizozifahamu kuomba asamehewe. Hakuwahi kuingia kanisani wala msikitini, lakini siku hiyo alimtaja Mungu akimwomba amnusuru mikononi mwa wananchi wenye hasira kali.
Mungu akasikia sala yake.

Watu wale wakaamua kumpeleka kituo cha polisi huku tayari wakiwa wamemwachia maumivu ya kutosha. Polisi nao wakamtupa ndani ili aweze kufikishwa mahakamani.
Siku ya kwanza mahakamani hapo kesi yake ilitajwa na kuanza kusikilizwa baada ya upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo ikiwa ni pamoja na kukusanya mashahidi. Upande wa mashitaka ulitoa ombi kesi hiyo kusikilizwa haraka kwani sehemu kubwa ya mashahidi walikuwa ni wanafunzi waliopo likizo hivyo siku si nyingi watarejea mashuleni kwao.

Siku hii ilikuwa ni muhimu sana kwa Majaliwa. Ni siku ya hukumu. Mwenendo wa kesi hiyo uliwavuta watu wengi hususani majirani pamwe wafanyabiashara ndogondogo wenzake mama Majaliwa. Marafiki zake walijaribu kumfariji. Wengine kama kawaida hawakuacha kumsimanga kuwa walimwambia mara nyingi amkanye kijana wake lakini akawapuuzia. Kumbukumbu ya maneno hayo ya watu ikawa moja ya vitu vilivyomwumiza zaidi mama Majaliwa. Akatamani angeweza kuurudisha nyuma muda ili aweze kuzungumza na kijana wake na kumshauri aachane na mambo hayo, ikibidi waungane kwenye biashara ndogondogo.

Muda wote mama Majaliwa alikuwa akimtazama mwanawe wa pekee pasipo kuamini kinachoendelea. Mara kadhaa alijihisi kuzama katika ndoto fulani iliyomsafirisha hadi ulimwengu mwingine uliojaa mateso makali na majonzi mazito mioyoni mwa wanadamu. Siku hiyo ilikuwa ngumu sana kwake kwani alipata maumivu makali sana ya tumbo la uzazi. Machozi yalizidi kumtoka. Akawa anamtazama Majaliwa aliyekuwa akifanya juhudi kutomtazama yeye.

“Koooooooorti!”

Kuingia kwa hakimu kukawaondoa Majaliwa na mama yake katika ulimwengu waliokuwa na kuwarejesha katika ulimwengu halisi. Mahakama ya mwanzo Karoleni mji mdogo wa Tunduma. Hakimu huyo mwanamke akaketi. Kisha ukasomwa muhtahasari we kesi hiyo pamoja na majumuisho ya ushahidi wa pande zote mbili.
Hatimaye wakati ukawadia.

“Kutokana na ushahidi uliotolewa hapa mahakamani. Mahakama hii tukutfu imekukuta ndugu Majaliwa Sichembe na hatia ya kuvunja na kuiba. Mahakama inakuhukumu kifungo cha mwaka moja.”

Kilio kilisikika kutoka kona aliyokuwepo mama Majaliwa. Watu wote waligeuka kumtazama mama huyo aliyedondoka chini. Watu wakambeba haraka na kumtoa nje ya mahakama hiyo ili apate kuzinduka. Mahakama nzima ikashikwa na bumbuwazi la nukta kadhaa.

Nukta hizo kadhaa zikaizungusha haraka sana akili ya Majaliwa. Akamtazama askari na kumwona macho yote kayaelekeza nje. Nukta moja ilimtosha kufanya maamuzi. Nukta nyingine ikamshuhudia akiwa tayari nje ya mahakama hiyo akitimua mbio.

“Huyooo anakimbia!”

Sauti ya mwananchi mmoja ndiyo iliyoizindua mahakama hiyo kutoka katika bumbuwazi lililoishika mahakama hiyo kwa nukta kadhaa. Askari akatoka baruti kumfukuzia Majaliwa aliyekuwa akikimbia kuelekea kota za Tazara eneo la Tanesco. Umati wa watu ukaanza kumfukuza. Ama kwa hakika Majaliwa alikuwa mwanariadha hodari. Alipandisha kimlima chote cha Mpondaraha pasi kupunguza mwendo. Askari naye alijitahidi kukazana ingawa pumzi hazikumruhusu kabisa. Alibaki akitweta huku akikifikiria kibarua chake kitakavyoota nyasi kwa kosa la uzembe kama hilo.

“Mwizi huyoooo!”

Sauti hiyo iliwafikia watoto wanne wa shule ya msingi waliokuwa eneo la Mkataperani katika kota za Tazara wakijiandaa kurudia shule kwa masomo ya mchana.

“Yuko wapi?” Mtoto mmoja akawauliza wenzake.

“Yule kule mbele.” Majaliwa akawajibu watoto hao akiwa amewakaribia huku akinyoosha kidole chake mbele kwa lengo la kuwapoteza.

“Huyo huyo mkamateni.” Sauti kutoka kwa wakimbizaji waliokuwa bado mbali kidogo ikasikika.

Watoto wale wa shule wakamtazama Majaliwa. Naye akawatazama huku akiwaonesha mbele zaidi huku akikaribia kabisa mahali walipo lakini akiendelea na mbio. Watoto wale wakatazama mbele na kutoona dalili za mwizi zaidi ya mashamba.

Bila ajizi mwanafunzi mmoja wa kiume aliyetokea nyuma ya nyumba akamkata ngwara Majaliwa iliyompeleka chini. Watoto wale wote wakamvaa na kuanza kumdondoshea kichapo cha nguvu.

“Siyo mimi jamani mnanionea bure!” Majaliwa alijitahidi kujitetea.

Watoto wa shule walimpiga sana. Mara wale wananchi waliokuwa wakimfukuza wakawasili na kuongeza kipigo. Akatokea mkulima mmoja aliyekuwa akikusanya mabua shambani baada ya mavuno. Akamsindilia na reki ya kusafishia shamba mgongoni mwa Majaliwa. Ikamchimba ku kumfanya atoe kilio zaidi huku mgongo wake ukivuja damu mithili ya bomba la mvua.

Huyu mwingine akatoka alikotoka. Akaja na gunia tupu.
“Tumwingize humu tumchome moto.”

“Eeeh! Tufanye hivyo hawa wamezowea sana.”

“Achomwe huyu si mnaona polisi kala pesa kamwachia akimbie.”

“Asulubiweeeeee!” Watoto wa shule nao hawakuwa nyuma kushadadia.

Wananchi wakachangamka na kumwingiza ndani ya gunia lile. Majaliwa alikuwa akilia huku maumivu makali yakimwelemea kutokana na kipigo hicho. Kwa tabia ya wananchi wa Tunduma wakamatapo mwizi, alifahamu nini kitakachoendelea. Akawa anajaribu kujitetea. Akatulia alipoisikia sauti ya askari maana aliamini huo ndiyo usalama wake.

Maji yalishamwagika.

“Hebu acheni kujichukulia sheria mkononi.” Askari polisi alisema baada ya kuwasili pale akitweta kwa nguvu.

“Tena toka zako kabla hatujakuachia kichapo na wewe!” Raia mmoja akamchimba mkwara.

“Nyie hamfai kabisa.”

“Kila siku tunawaleta kwenu mnawaachia wanatoroka.”

“Halafu wanakuja kutamba mitaani.”

“Wanapewa pesa hao hao hawana maana kabisa.”

“We’ huyu si umekula hela ukamwacha akimbie?”

“Hebu tuondokee huko kabla hatujakutia kiberiti na wewe.”

Askari yule alifahamu fika wananchi wale hawakuwa wakitania. Kujichukulia sheria mkononi ndiyo utaratibu wao wa maisha. Ni mara chache sana mtuhumiwa kufika kituo cha polisi. Mara nyingi waliishia kuwa majivu. Askari akazidi kuchanganyikiwa asijue la kufanya. Alibaki kuwatazama wananchi wale waliomzidi nguvu wakimfunga Majaliwa ndani ya gunia. Hakuwa hata na bunduki kiasi kwamba angepiga walau risasi hewani kuwatawanyisha.

Petroli hata haikujulikana imetoka wapi na saa ngapi. Askari akashuhudia lile gunia likimwagiwa petroli na dakika hiyo hiyo gunia likapigwa kiberiti. Nalo pasi ajizi likashika moto hasa. Likawaka kwa nguvu zote. Sauti ya Majaliwa haikusikika tena maana ilishakauka na moto kumzidi pumzi.

Wananchi wakalizunguka gunia lile wakilitazama namna linavyotekea kwa moto huku wakipiga kelele za shangwe.
“Dawa yao ni hii hii!”

“Wamezowea hao!”

“Hawa ni kupiga petroli tu!”

Wananchi wakalitazama gunia lile likiwaka moto hadi kuwa majivu kabisa.

Wakaondoka kila mtu na hamsini zake huku wakishangilia.
Ukawa ndiyo mwisho wa Majaliwa.


MWISHO.