Kuhusu mimi

NILIZALIWA katika hospitali ya mkoa mjini Iringa. Familia yetu ni ya watoto watatu.
Nikapelekwa shule ili nijue kusoma na kuandika. Wakati nikijifunza hayo, nikawa na ndoto. Kila mtoto huwa na ndoto.

NDOTO YA KUWA MWANDISHI
HAIKUWA rahisi, wala haikuwezekanika kabisa kwangu kuachana na ndoto ya kuwa mwandishi wa hadithi za kubuni. Katika maisha ya mwanadamu, ndoto hizi haziji vivi hivi. Daima huwa na chanzo chake. Mwanadamu awaye yeyote yule, huwa na ndoto wakati wa kukuwa kwake. Mwingine aweza kuwa na ndoto ya kuja kuwa daktari, mwingine kuwa askari, mwingine kuwa mwanasheria, mwingine kuwa rubani na kadhalika.

Ndoto juu ya maisha yako ya baadaye huwa na msukumo wake. Msukumo huo, endapo utaendelezwa, ndipo njia kwa ajili ya kuitimiza ndoto yako, huwa ya wazi na yenye kutia moyo. Chambilecho wahenga, penye nia pana njia. Ninaamini wajibu wa kila mzazi ni kujaribu kuwa karibu na mwanawe, kumsoma ili kubaini karama zilizojificha ndani yake. Kisha kumsaidia kuzitoa nje na kuzifanya zitumike katika maisha yake.
Tuje upande wangu.

Rafiki zangu hupenda kuniuliza mara kwa mara, nini kilinisukuma kuwa kupenda kuwa mwandishi wa mashairi na hadithi za kubuni? Hata mimi hupenda kujiuliza swali hilo hilo kila mara. Lakini kwangu, jawabu huwa rahisi sana. Ngoja nieleze historia ya kukuwa kwangu kwa ufupi.

Nyumbani kwetu kulijaa vitabu chungumbovu.
Kwa kuwa mama yangu ni mwalimu, basi hakuacha kuijaza nyumba vitabu. Hivyo, wakati wa utoto wangu, nilipojua tu kusoma na kuandika, nikaanza kuogelea katika bahari ya vitabu. Vitabu nilivyoanza kuvisoma utotoni mwangu ni vingi sana. Lakini bado nakumbuka vitabu kama Hadithi Za Bibi, Hekaya za Abunuwasi, Someni Kwa Furaha, Adili Na Nduguze, Alfu Lela Ulela, Ujinga Wa Mwafrika na vingine vingi vilivyokuwa maarufu wakati huo.

Niseme pia kuhusu marehemu baba yangu. Yeye kitaaluma alikuwa mhasibu na mkaguzi wa mahesabu. Lakini marehemu baba yangu, alikuwa na mapenzi makubwa sana na fasihi ya Kingereza. Si tu kuwa mpenzi wa fasihi, lakini pia kuwa mnunuaji mzuri sana wa vitabu. Katika urithi pekee ninaojivunia kutoka kwa marehemu baba yangu ni vitabu. Kutoka maktaba yake nimebahatika kurithi vitabu vingi, vikiwemo, The Black African Voices, How Europe Underdeveloped Africa, The Great Controversy, The Adventure Of English Literature, Norton Anthology Of English Literature, Anthology Of A Verse, Makers Of Modern Europe, Potrait In America na Modern American Drama. Niliweza kuvitunza vema vitabu hivyo. Sasa ni lulu kwangu.

Nikiwa darasa la pili nilikwenda kuishi kwa bibi yangu kijijini kwetu Ilembula wilayani Njombe. Huko nikajiunga na Shirika la Huduma za Maktaba la Taifa. Uanachama wangu wa maktaba ukanifanya kusoma vitabu vingi zaidi. Kila siku tulitoka shule saa tano asubuhi. Baada ya chakula cha mchana, nilikwenda kushinda maktaba hadi ilipofungwa saa kumi unusu jioni. Kipindi hicho niliweza kusoma riwaya nyingi sana za Kirusi ambazo zilitafsiriwa katika Kiswahili. Niliwasoma waandishi wa riwaya wa Kirusi kama Alexander Pushkin na Fyodor Dostoyevsky. Nilisoma hadithi kuhusu maisha ya watu kama Vladmir Ilich Lenin, Mwalimu J K Nyerere, Kwame Nkrumah, Pengine niseme, hadi kufika darasa la pili, nilikuwa nimeweza kusoma vitabu vingi vya fasihi ya Kiswahili vilivyokuwa maarufu wakati huo. Pia niliweza kusoma matoleo ya majarida maarufu sana wakati huo ya Sani likiwa limejaa riwaya za Said na Amri M M Bawji. Pia jarida la Tanzania Film likiwa na simulizi za kusisimua za Faraji H H Katalambula.

Nilipofika darasa la tatu, ndipo hamu ya kuwa mwandishi iliponiingia kwa mara ya kwanza. Siku moja mwezi Januari mwaka 1992, nilimfuata mama yangu na kumwambia nataka kuandika shairi. Mama alitabasamu sana. Niliweza kuuona mshangao uliouvaa uso wake ingawa yeye hakutaka niuone kwa kuhofu kunikatisha tamaa. Nikamwonesha shairi nililokuwa nimeliandika. Kwa kuwa nilikuwa msikilizaji mzuri wa kipindi cha mashairi kilichokuwa kikirushwa na iliyokuwa Redio Tanzania Dar es Salaam, lile shairi nililiandika shaghalabhaghala kufuata tu sauti ya waimbaji wa mashairi redioni. Wala sikuwa nafahamu kabisa habari ya vina na mizani.

Mama akaniambia nimeandika vizuri sana. Akaniahidi zawadi ya nguo mpya. Lakini alijua kuwa sikuliandika vizuri zaidi ya kuwa kituko. Asingeweza kunikatisha tamaa. Jioni tulipomaliza kula, akaniita na kuniambia, “Umeandika shairi zuri sana, nataka sasa nikufundishe namna ya kuandika shairi vizuri zaidi.”
Hapo ndipo akanipa somo juu ya sheria na kanuni za kuandika mashairi. Lakini somo la mizani niliona ni jepesi. Kasheshe ilikuwa ni somo la vina. Kwa umri niliokuwa nao na uhaba wangu wa misamiati, niliona ni jambo nisiloliweza kabisa. Akanipa moyo kuwa nipende kusoma mashairi ya watu wengine, lakini nisiyaige. Akaniambia kwa kusoma mashairi na vitabu vingi zaidi kadri niwezavyo, kutanifanya kuwa mshairi mzuri.

Siku chache baadaye, akaniletea zawadi ya vitabu vinne, Diwani Ya Saadan Kandoro cha hayati Kandoro, Shida cha Ndyanao Balisidya, Kufa Na Kupona cha Elvis Musiba na Kuli cha Shafi Adamu Shafi. Wakati huo huo nikasoma riwaya ya Duniani Kuna Watu ya Muhammed Said Abdullah. Hapo nikazidi kuzama kwenye bahari ya usomaji wa vitabu. Hadi kufika Oktoba ya mwaka huo huo, nilikuwa nimeweza katika kiwango kilichomshangaza hata yeye, kuandika mashairi kwa kufuata vina, mizani, vituo na mtoshelezo.

Wakati namaliza darasa la saba, tayari nilikuwa nimesoma riwaya nyingi sana za kusisimua kutoka kwa waandishi wa Kitanzania kama Elvis Musiba, Ben R. Mtobwa, Jackson Kalindimya, William Mkufya, Euphras Kezilahabi, Edwin Semzaba, John Simbamwene, Jumanne Mayoka na wengine lukuki. Lakini pia nilikuwa nimeweza kuandika mashairi mengi sana ambayo mengine bado ninayo hata leo. Wakati huo huo, ndipo nami nikaanza kuandika hadithi katika madaftari yangu. Ninafurahi kuwa moja ya hadithi hizo bado ninayo hata leo.

Nikiwa kidato cha kwanza, ndipo nilipoanza kusoma riwaya ya Kingereza. Kitabu cha kwanza kukisoma, kinaitwa Zero Hour kilichoandikwa na Ben R. Mtobwa, na kingine cha Kinaijeria, Forgive Me Maryam.

Kila nikikumbuka kukuwa kwangu najawa na hisia za ajabu sana. Najawa kumbukumbu za bahari ya vitabu. Natamani sasa nyakati zile.

Naweza kusema, kusoma vitabu vya riwaya, hadithi fupi na mashairi ukawa utamaduni wangu ambao ninamshukuru Mungu nimeweza kuudumisha hata leo hii. Miaka ishirini na mbili nyuma, ndipo utamu wa fasihi ulipoanza kuninogea. Ndipo hamu hasa ya kuwa mwandishi wa mashairi, hadithi fupi na riwaya iliponiingia mwilini. Leo hii naweza kusema tu, sijaweza kuitimiza ndoto yangu, lakini nimeweza kuandika haya ukayasoma.