Friday, October 28, 2016

Waulizeni

Waulizeni watu wale,
Na wasilale,
Wakumbusheni siku zile,
Na mambo yale,
Kama ni chakula wakile,
Wasijali hata kama cha wale,
Maana ni yale yale!

Mnaandika lakini?

Waulizeni kwa yakini,
Wafikiri vichwani,
Tangu lini?
Iliwajia machoni,
Ile namba ya mwanzoni,
Ikawa asalini,
Tangu lini?

Ama kumekucha?

Hauchi hauchi wecha,
Wavichachuavyo vimechacha?
Ye wapi yenu mapakacha,
Kumekucha na makucha,
Si asali bali ‘tocha’,
Waulizeni pasi kuacha,
Hata neno msijeficha.

Watasema kweli?

Lanipa shaka shauri hili,
Kama watalihimili,
Yaone macho yao mawili,
Na mioyo yao ikubali,
Kuwa kuna kufeli,
Ama kufaulu asilimia mbili,
Basi, msiulize tena maswali.

Fadhy Mtanga,
Mbeya.

Ijumaa, Oktoba 28, 2016.

1 comment:

  1. Mtani duh! ni siku nyingi sana afadhali umeandika hili shairi maana nilikuwa najiuliza sana na kutamani kusoma angalio mstari tu...

    ReplyDelete