Saturday, July 9, 2016

Uzuri wako

Uzuri wako wewe unanipa kiwewe,
Nifanye nini mie ili niwe na wewe?
Mi si Mr Nice wimbo uimbiwe,
Wewe ukadhani aimbiwa mwinginewe, 
Lahaulah!

Moyo wangu umeujaza tele hisia,
Namna siku z'endavyo nazo zazidia,
Kukufahamu wewe mie najivunia,
Wanipa raha maisha kuyafurahia,
Alhamdulillah!

U mzuri mwenye macho mithili ya hua,
Kila niyaonapo nahisi kuugua,
Nina raha u tabibu unayenijua,
Nami najivunia wewe kukuchagua,
Ewaaaaaaah!

Rangiyo yavutia toto rangi rangile,
Rangi ivutiapo, yang'ara naturally,
U msichana mrembo zako sifa tele,
Wan'ache nikusifie kwa vigelegele
Mashaallah!

Unayo sauti utadhani ya kinanda,
Ama ya ndege tena yule angali kinda,
Sauti iso na mawaa iso na inda,
Naitamani iniambie wanipenda,
Inshaallah!

Uzuri wako niufananishe na nini?
Ah wapi, cha kufananishia sikioni!
Waniache nikupende nizame dimbwini,
Dimbwi la mahaba kwa raha yalosheheni,
Aaaaah!

Wewe u pekee, peke yako duniani,
Katu sitosema you are my number one,
Kwa maana wewe kwangu hunacho kifani,
Sijaona kokote, kote bara na pwani,
Walaah!

Fadhy Mtanga,
Mbeya, Tanzania.
Jumamosi, Julai 9, 2016.

2 comments:

 1. UZURI WAKO (MAONI)

  Uzuriwe sikulize, si wa kudumu milele,
  Tabiaye ichunguze, si kwa pupa pole pole,
  Ndipo mengi mnyunyize, kwa sifa hizi na zile,
  Usoni asikulize, habaki kupewa pole.

  ReplyDelete
  Replies
  1. Uzuri umezidia, naamini utadumu,
   Yu fora kwa tabia, wangu muhashamu,
   Mengi namnyunyizia, amejaa ufahamu.

   Delete