Friday, June 17, 2016

Tabibu

Nataka uwe tabibu,
Wala usilete gubu,
Nani alokughilibu,
Mie ukanikimbia?

Miaka mingi yaenda,
Hakiniponi kidonda,
'Lisema hutonitenda,
Nini kikaja tokea?

Ulisema utabaki,
Penye raha ama dhiki,
Ghafla 'katoka nduki,
Simanzi kuniachia.

Ni wapi huko uliko,
Nikuf'ate hukohuko,
Hadi n'fanye zindiko,
Ndipo utaporejea?

Nambie nifanye nini,
Tuishi kama zamani,
'Siseme mwako moyoni,
Eti 'lishaniondoa.

Fadhy Mtanga,
Mbeya, Tanzania.
Ijumaa, Juni 17, 2016.

2 comments:

 1. Mmmmhhh shairi latekenya mtani. ...Hasa hapa
  Ni wapi huko uliko,
  Nikuf'ate hukohuko,
  Hadi n'fanye zindiko,
  Ndipo utaporejea?
  Ahsante...

  ReplyDelete
  Replies
  1. Shukrani sana Mtani kwa kuendelea kuyapenda mashairi yangu miaka nenda miaka rudi.

   Delete