Thursday, January 14, 2016

Nataka Chai

Siyo iliyochemshwa,
Itakuwa tu mchemsho,
Itanichemsha!

Nataka iliyopikwa,
Bonge la mpiko,
Ikapikika.

Tena kwa ufundi,
Siyo ufundoo,
Ikafundika.

Nataka yenye utamu,
Siyo tamutamu,
Bali tamu kolea.

Hadi kisogoni!

Nataka yenye viungo,
Siyo uongo uongo,
Weka masala,
Yafate hata Salasala!
Yatangulizie sala.

Nataka chai mie,
Nna kiu nayo!

Iweke kila kitu,
Mdalasini,
Tangawizi,
Pilipili manga,
Majani yake,
Sukari usiisahau.
Ukiweza,
Weka asali.

Niweke mezani,
Meza safi,
Iliyosafishwa,
Ikasafishika.

Chai kikombeni,
Nataka kikombe kimoja tu,
Na mshikio wake moja,
Kikombe cheupe,
Kiso na doa.

Nataka chai,
Ndashene!

Chai tamu,
Tamu yenye utamu,
Utamu mtamu,
Utamu kolea.

Nataka chai miye!

Usininyime mwanakwetu!

Lakini,
Sinipe yenye kuunguza,
Wangu ulimi.

Fadhy Mtanga,
Chole Road, Masaki, Dar es Salaam.
Alhamisi, Januari 14, 2016.

5 comments:

 1. Mmm Chai kumbe mtani ni mpenzi wa chai kama mimi:-) Bonge la shairi nimelipendaje na hapa yaja chai yako....
  Chai ni hii mtani....
  Nimewweke kila kitu,
  Mdalasini,Tangawizi,
  Pilipili manga,
  Majani yake,
  Ila sio Sukari isipokuwa,
  Nimeeka asali.

  ReplyDelete
  Replies
  1. Ooooh ahsante kwa yako chai,
   Chai tamu,
   Tamu yenye utamu mtamu,
   Inogayo mdomoni!

   Ladha iso kifani.

   Delete
 2. Hahahahahahahahahaha..... noma sana

  ReplyDelete
 3. UTAMU MTUPU.LAKINI UTAMU WA CHAI SUKARI SIYO RANGI.SHAIRI ZURI ONGERA>

  ReplyDelete
 4. Ahsanteni sana kwa kupita na kuacha maoni.

  ReplyDelete