Wednesday, July 1, 2015

Oooh!

Kijana!
Mwanakwetu una nini, nauliza,
Ni nani kakurubuni, waniliza,
Umepatwa mashetani, nguvu giza?
Wanishangaza!

Kijana!
Shuleni umekwenda, umesoma,
Twangojea matunda, yalo mema,
Na siyo yaliyovunda, tukatema,
Kijana wewe!

Kijana!
Watetea mafisadi, kisa pesa,
H'wambiliki kaidi, tele visa,
Tena wafanya kusudi, umenasa,
Huna maana!

Vijana!
Eti mnazo timu, hovyo hovyo,
Mnajitia wazimu, mfanyavyo,
Muda utawahukumu, nionavyo,
Mnatumika!

Vijana!
Timu nao marafiki, mmekwisha,
Wala hamueleweki, mwatuchosha,
Na tena hatuwataki, mwapotosha,
Nchi si yenu!

Wenzangu!
Na msituchagulie, hatutaki,
Na msitusafishie, kwayo jiki,
Nyie mumtumikie, ni rafiki,
Ila si kwetu!

Wenzangu!
Historia huhukumu, ilisemwa,
Na maandishi hudumu, yakasomwa,
Msitupe sie sumu, tukaumwa,
Wala si sawa!

Wananchi!
Oktoba ikifika, tujihimu,
Kura zetu kuziweka, ni muhimu,
Tuchague kwa hakika, muashamu,
Kutuongoza!

Wananchi!
Ni vema tudhamirie, kwazo nia,
Makosa tusirudie, tutalia,
Kwa busara tuchague, Tanzania,
Atufaaye!

Wananchi!
Wito wangu nautoa, kwa yamini,
Mola azidi jalia, taifani,
Uchaguzi 'kifikia, umakini,
Chaguo bora!

Fadhy Mtanga,
Kihesa, Iringa.
Alhamisi, Julai 2, 2015.

2 comments:

  1. Eeehh! Mtani ni siku nyingi sana hujaandika mashairi nimekuwa nikijiuliza kulikoni mtani wangu. Na hatimaye umeandika nimefurahi sana. Ahsante

    ReplyDelete
    Replies
    1. Mtani, kuna pepo la uvivu liliniandama. Nimelikemea kwa nguvu zote.

      Delete