Saturday, June 28, 2014

Wewe huyo

Unang'ara mwangu machoni,
Wachanua mwangu moyoni,
Niende kote duniani,
Sitoona chako kifani,
Nikupende wewe tu,
Ndivyo moyo wanambia!

Nasema yangu ya moyoni,
Kuficha siwezi jamani,
Nimezama mie dimbwini,
Nimezama mi mapenzini,
Mahaba nivuruge tu,
Moyo wangu wafurahia!

Nivuruge tu hak'ya nani,
Mahaba nijaze rahani,
Nikoleze hadi moyoni,
Nikoroge mwangu kichwani,
Unijaze mahaba tu,
Nifurahi na dunia!

Unibusu pangu shavuni,
Na mpapaso mgongoni,
Ninong'oneze sikioni,
Kwa sauti yako laini,
Nakutamani wewe tu,
Ambaye kwako nimetua!

Furaha yangu duniani,
N'sahaulishe ya zamani,
Maumivu siyatamani,
We ndo tabibu wa thamani,
Unanimudu wewe tu,
Juu yako nayeugua!

Umetamalaki moyoni,
Unatawala mawazoni,
U mwenza wangu duniani,
Na rafiki yangu ndotoni,
Wacha nikuwaze wewe tu,
Ndicho nachokifurahia!

Fadhy Mtanga,
Kijitonyama, Dar es Salaam.
Jumamosi, Juni 28, 2014.

1 comment:

  1. Hakika ni bonge la utamu kwa kusoma shairi hili...nimependa na kutamani ningekuwa mimi nimeandikiwa:-)

    ReplyDelete