Friday, August 15, 2014

Nayapenda maisha

Nayapenda maisha,
Kwa furaha yanipayo,
Kwa huzuni yanileteayo.

Nayapenda maisha,
Kwa mapenzi niyapatayo,
Kwa chuki zinipitiazo.

Nayapenda maisha,
Kwa mafanikio nipatayo,
Kwa changamoto nizipatazo.

Nayapenda maisha,
Kwa jitihada nilizonazo,
Kwa uvivu niupatao.

Nayapenda maisha,
Kwa ndugu wema nilionao,
Kwa ndugu wanichukiao.

Nayapenda maisha,
Kwa marafiki wema niwapatao,
Kwa wanafiki watokeao,

Nayapenda maisha,
Kwa afya njema niliyonayo,
Kwa maradhi yanipitiayo.

Nayapenda maisha,
Kwa akili nilizonazo,
Kwa umbumbumbu nilionao.

Nayapenda maisha,
Kwa imani na dini niliyonayo,
Kwa kutikiswa nikupitiako.

Nayapenda maisha,
Kwa maono na dhamira niliyonayo,
Kwa kukata tamaa nisikokuwa nako.

Nayapenda maisha.

Nayapenda sana.

Fadhy Mtanga,
Kabwe, Mbeya.
Ijumaa, Agosti 15, 2014.

Saturday, June 28, 2014

Wewe huyo

Unang'ara mwangu machoni,
Wachanua mwangu moyoni,
Niende kote duniani,
Sitoona chako kifani,
Nikupende wewe tu,
Ndivyo moyo wanambia!

Nasema yangu ya moyoni,
Kuficha siwezi jamani,
Nimezama mie dimbwini,
Nimezama mi mapenzini,
Mahaba nivuruge tu,
Moyo wangu wafurahia!

Nivuruge tu hak'ya nani,
Mahaba nijaze rahani,
Nikoleze hadi moyoni,
Nikoroge mwangu kichwani,
Unijaze mahaba tu,
Nifurahi na dunia!

Unibusu pangu shavuni,
Na mpapaso mgongoni,
Ninong'oneze sikioni,
Kwa sauti yako laini,
Nakutamani wewe tu,
Ambaye kwako nimetua!

Furaha yangu duniani,
N'sahaulishe ya zamani,
Maumivu siyatamani,
We ndo tabibu wa thamani,
Unanimudu wewe tu,
Juu yako nayeugua!

Umetamalaki moyoni,
Unatawala mawazoni,
U mwenza wangu duniani,
Na rafiki yangu ndotoni,
Wacha nikuwaze wewe tu,
Ndicho nachokifurahia!

Fadhy Mtanga,
Kijitonyama, Dar es Salaam.
Jumamosi, Juni 28, 2014.

Friday, March 28, 2014

Tumerogwa?

Dziseketa mwileme!

Kwa makuhani, wanaohani na makuhana,
Waugeuzao usiku kwa hila ili uwe mchana,
Waso haya, waso sudi wawazao tu kutukana,
Wasojali na kuzijali walizopewa hizo dhamana,
Wadhaniao wao ndo wa leo ilhali zetu fikra za jana,
Bado tukawaamini tukawaambia tena na tena,
Tumerogwa?

Tabibu?
Kwao weledi walokubuhu vichwani pengine kwa funza,
Wenye mang'onyo wakalewa misasati vichwani wakateleza,
Watuaminishao kwa yao matingo kichwa kichwa tukajiingiza,
Tumepotea, tumepotezwa, tumepotezana ama tumepoteza?
Kaa? Tiba? Yaliapo mbwata kwa ushambenga muda tukipoteza,
Twajiona sisi ndo kitu na kilakitu sisi ndo tunaweza,
Tumerogwa!

Fadhy Mtanga,
Kijitonyama, Dar es Salaam.
Ijumaa, Machi 28, 2014