Tuesday, December 3, 2013

Ya'ani?

Hino si sino yaani, siy’echi yalo ngamani,
Neno ndilo mdomoni, waama sina utani,
Ushanijaa moyoni, sifurukuti yaani,
Ya’ani kuficha?

Siyo mboni ‘lo jichoni, bali moyo ‘lo moyoni,
Maneno tupu sineni, nakutenda yalo shani,
Meshiba mie pendoni, nakupendaje yaani,
Ya’ani kuficha?

Vijinopembe pembeni, yawachome mioyoni,
Nishazama ‘mo rahani, nilotopea dimbwini,
Dimbwini ‘ko mahabani, mbona ‘na raha
yaani,
Ya’ani kuficha?

Jamani mie jamani, msin’ulize ‘na nini,
Nimependa duniani, sisikii ‘la sioni,
Guuni ‘di utosini, sijielewi yaani,
Ya’ani kuficha?

Kote kote duniani, mwingine ‘tomtamani,
Nitataka tena nini, na sitaki abadani,
Nihangaike kwa’ani, basi n’wehuke yaani,
Ya’ani kuficha?

Mlo na gere oneni, mgae gae upwani,
Zino kavu mtaleni, mu’nge wajihi puani,
Nimependa niwacheni, nijinomee yaani,
Ya’ani kuficha?

Sifichani ‘mo nenoni, utamuwe ‘so kifani,
Yaani!

Fadhy Mtanga,
Mtongani, Dar es Salaam.
Jumanne, Disemba 3, 2013.

2 comments:

  1. Yaani, shairi limetulia mpaka raha usomapo unajisikia kama vile maneno hayo unaambiwa wewe mmmmhhh watu wana vipaji..

    ReplyDelete