Tuesday, October 1, 2013

Jivute taratibu

Mpenzi sogea ujivute taratibu,
Haya maradhi ya moyo uje kuyatibu,
Njoo unibembeleze ukiwa karibu,
Ewe nikupendaye ulo wangu muhibu,
Jivute taratibu, sogea karibu.

Njoo karibu nikweleze yanonisibu,
Nikueleze ewe ulo wangu tabibu,
Unipozaye yanijiapo masahibu,
Mapenzi unipayo yenye nguvu ajabu,
Jivute taratibu, sogea karibu.

Mpenzi wangu wang'ara kuzidi dhahabu,
Mpenzi wanukia nukato mahabubu,
Tunu nakupatia kwa moyo kuratibu,
Wewe ndo wangu hunacho kifani taibu,
Jivute taratibu, sogea karibu.

Ukiniacha moyo utapata taabu,
Nichanganyikiwe nikose hata adabu,
Nijaze mapenzi tena bila kuhesabu,
Wewe kukuacha katu siwezi jaribu,
Jivute taratibu, sogea karibu.

Mapenzi unipayo tuzo yako thawabu,
Kwako nimezama mapenzini nimeghibu,
Nikikosa nambie sitosita kutubu,
Usininunie mapenzi tukaharibu,
Jivute taratibu, sogea karibu.

Fadhy Mtanga,
Morogoro.
Jumanne, Oktoba 1, 2013.

2 comments:

  1. Mmmh! Shairi tamu toka kwenye kidole gumba mpaka kichwani-:) sidhani linalomuhusu akisoma hawezi kukucha mtani wangu

    ReplyDelete