Thursday, September 12, 2013

Wewe ndo furaha yangu

Wangu moyo laazizi, wewe nimekupatia,
Juu yako sijiwezi, moyo umekuchagua,
Kukupenda s’oni kazi, mwenyewe nimeridhia,
Wewe ndo furaha yangu, wanipa kutabasamu.

Sipigi tena miluzi, nukta nishaitia,
Kutangatanga siwazi, vyote we’ wanipatia,
Kwingine kwenda siwezi, hakuna ‘lokufikia,
Wewe ndo furaha yangu, mapenzi yako matamu.

We ndo wangu usingizi, daima nakuwazia,
Wanijia kwenye njozi, hakuna wa kunambia,
Moyo mejaa mapenzi, wewe nimekujazia,
Wewe ndo furaha yangu, juu yako si’shi hamu.

Siw’ogopi wazengezi, kwako nimeshatulia,
Wengine naw’ona ndezi, moyo umeshachukua,
Hayatoshi maongezi, wewe nikakusifia,
Wewe ndo furaha yangu, wa moyoni muhashamu.

Maisha yana viunzi, penzi kutuharibia,
Nabana zangu pumzi, penzi letu nalindia,
Wengine wana majonzi, kutwona twafurahia,
Wewe ndo furaha yangu, duniani kote humu.

Nayasema wazi wazi, kwako nimeshakolea,
Kwingine sikuangazi, kwako wewe nimetua,
Kukusaliti siwezi, leo ahadi  natoa,

Wewe ndo furaha yangu, ya daima na dawamu.

Fadhy Mtanga,
Sinza Mori, Dar es Salaam.
Alhamisi, Septemba 12, 2013.

Sunday, September 8, 2013

Kama nyota za angani

Kama nyota za angani,
Usiku zinavyong’aa, ndivyo penzi langu kwako,
Mapenzi yamenijaa, huba tele juu yako,
Wala sikati tamaa, mimi ndiye mali yako.

Kama nyota za angani,
Usiku zinavyong’aa, ndivyo ninavyokupenda,
Kwako mefika haswaa, kwingine siwezi kwenda,
Maneno nayakataa, yaso ubani yavunda.

Kama nyota za angani,
Usiku zinavyong’aa, wewe ndo mpenzi wangu,
Bora wakinishangaa, sitoweza peke yangu,
Kamwe sijihisi njaa, uwapo pembeni yangu.

Kama nyota za angani,
Usiku zinavyong’aa, daima nitakuenzi,
Siwezi kukuhadaa, ewe wangu laazizi,

Moyoni ushanikaa, we ndiwe wangu mpenzi.

Fadhy Mtanga,
Kijitonyama, Dar es Salaam.
Jumapili, Septemba 8, 2013.