Sunday, August 4, 2013

Peleka salamu

Njoo rafiki yangu kalamu,
Uziandike hizi salamu,
Zimfikie wangu muhimu,
Juu yake ninayeugua.

Muda ndo huu umeshatimu,
Nami nazidi pata wazimu,
Hata kula sina tena hamu,
Kwa jinsi ninavyomuwazia.

Usingizi ni mang'amung'amu,
Alfajiri ninajihimu,
Utadhani ndimi mnajimu,
Kumbe yeye namuugulia.

Kalamu zifikishe salamu,
Mwambie ye ndo muhashamu,
Moyoni nimempa sehemu,
Ili yeye apate tulia.

Kamwambie asinidhulumu,
Asinifanye nibwie sumu,
Ndugu wote watamlaumu,
Wanajua ninamzimia.

Kamfanye vema afahamu,
Nimemwandalia penzi tamu,
Ambalo halitomwisha hamu,
Daima atalifurahia.

1 comment:

  1. Duh! Bonge la ujumbe..nimeupenda...mtani huyu mtu inaonyesha ni muhimu kweli kwako natumaini umemfikia.

    ReplyDelete