Monday, August 26, 2013

Yeye yule

Nipo kilimani ninaranda,
Wala singoji Peugeot kupanda,
Ninamngoja ninayempenda,
Moyo wangu alouchukuwa.

Aloniponya changu kidonda,
Alonifanya n'ache kukonda,
Moyo wangu mwenye kuulinda,
Kwayo mahaba ninayopewa.

Mpenzi wangu nayempenda,
Kwa silabi irabu na inda,
Ambaye bilaye swezi enda,
Juu yake ndo nishanogewa.

Kwa dhati ya moyo nampenda,
Wala hakuna wa kumshinda,
Namuwaza kila nakokwenda,
Penzi moyoni limeridhiwa.

Fadhy Mtanga,
Arusha Tanzania,
Jumatatu, Agosti 26, 2013.

Sunday, August 4, 2013

Peleka salamu

Njoo rafiki yangu kalamu,
Uziandike hizi salamu,
Zimfikie wangu muhimu,
Juu yake ninayeugua.

Muda ndo huu umeshatimu,
Nami nazidi pata wazimu,
Hata kula sina tena hamu,
Kwa jinsi ninavyomuwazia.

Usingizi ni mang'amung'amu,
Alfajiri ninajihimu,
Utadhani ndimi mnajimu,
Kumbe yeye namuugulia.

Kalamu zifikishe salamu,
Mwambie ye ndo muhashamu,
Moyoni nimempa sehemu,
Ili yeye apate tulia.

Kamwambie asinidhulumu,
Asinifanye nibwie sumu,
Ndugu wote watamlaumu,
Wanajua ninamzimia.

Kamfanye vema afahamu,
Nimemwandalia penzi tamu,
Ambalo halitomwisha hamu,
Daima atalifurahia.