Thursday, April 18, 2013

Juu yako sina hali

Mwenzio mi sijiwezi,
Siupati usingizi,
Layumba langu jahazi,
Mapenzi yan'elemea.

Naumwa si kikohozi,
Ugonjwa wangu mapenzi,
Tabibu we' laaziz,
Maradhi yanizidia.

Usingizi sikupati,
Moyo wangu hatihati,
Mapenzi yangu ya shari,
Wewe nimekupatia.

Natamani nikupate,
Nikuvishe yangu pete,
Hariri umeremete,
Nayo ahadi kutoa.

Kwako mie naugua,
Moyo wangu we chukua,
Kichwani wanizuzua,
Siachi kukuwazia.

Hakuna chako kifani,
Japo moja hafanani,
Wewe u nambari kwani,
Nami nikakuchagua.

Tafurahi kinipenda,
Vinginevyo nitakonda,
Sitokipona kidonda,
Na sitoacha kulia.

2 comments:

 1. Bonge la ujumbe...nadhani ujumbe umepokelewa kwa mikono miwili

  ReplyDelete
 2. Hayo meanza zamani, toka 'Adam na Hawa'
  Seuze yako loghani, mithili umepwerewa,
  Wapo lokubuhu fani, uhai yaliwatowa,
  Sianze chochea kuni, pika usichokijuwa!

  ReplyDelete