Tuesday, April 23, 2013

Majibu tunayo

Ila maswali hakuna.

Maswali yaliyopo hayafai,
Wao hawapo tayari,
Kuyajibu.
Majibu hawayajui,
Ni vilaza.

Wawezayo kuyajibu wao,
Ni yale tusowauliza,
Bla bla tu!
Na takwimu,
Na matusi pia,
Mbona wana mambo?
Mamboyo si haba.

Hapa haba,
Pale kibaba,
Halafu wanasema,
Binadamu wote ni sawa
Na Afrika ni moja!
Kumbe,
Je?
Si hivyo.

Hatuna maswali,
Tushajijibu wenyewe,
Akili kumkichwa!

Alaa kumbe!

Thursday, April 18, 2013

Juu yako sina hali

Mwenzio mi sijiwezi,
Siupati usingizi,
Layumba langu jahazi,
Mapenzi yan'elemea.

Naumwa si kikohozi,
Ugonjwa wangu mapenzi,
Tabibu we' laaziz,
Maradhi yanizidia.

Usingizi sikupati,
Moyo wangu hatihati,
Mapenzi yangu ya shari,
Wewe nimekupatia.

Natamani nikupate,
Nikuvishe yangu pete,
Hariri umeremete,
Nayo ahadi kutoa.

Kwako mie naugua,
Moyo wangu we chukua,
Kichwani wanizuzua,
Siachi kukuwazia.

Hakuna chako kifani,
Japo moja hafanani,
Wewe u nambari kwani,
Nami nikakuchagua.

Tafurahi kinipenda,
Vinginevyo nitakonda,
Sitokipona kidonda,
Na sitoacha kulia.