Wednesday, September 26, 2012

Wewe ndiyo sababu

Naamka nimejawa tabasamu,
Na kwacho chakula siishiwi hamu,
Furaha yangu yaushinda wazimu,
Moyo wangu una raha muhashamu,
Wewe ndiyo sababu.

Maishani nimejawa na furaha,
Nilishasahau kuhusu karaha,
Najihisi ni kwenye nyota ya jaha,
Hata mwendo wangu hujawa madaha,
Wewe ndiyo sababu.

Ukiwepo huwa kitamu chakula,
Hata usiku kwa raha ninalala,
Napenda niwe nawe kila mahala,
Moyo 'mekolea mapenzi jumla,
Wewe ndiyo sababu.

Wasopendwa nahisi wana taabu,
Ila sitaki juwa yanowasibu,
Raha yangu ni kuwa nawe muhibu,
Nina raha nimepata utabibu,
Wewe ndiyo sababu.

Kwenye mapenzi mie ninafaidi,
Penzi jekundu lishindalo waridi,
Tena ni tamu lilojawa sudi,
Linifanyalo nisihisi baridi,
Wewe ndiyo sababu.

Sasa ninaijua yake thamani,
Penzi la kweli lisilo na kifani,
Nina raha raha kutoka moyoni,
Nina furaha furaha duniani,
Wewe ndiyo sababu.

Fadhy Mtanga,
Mbeya, Tanzania.
Jumatano, Septemba 26, 2012.

2 comments:

  1. Hakika huu ni ujumbe wenye upendo wa kutoka moyoni. Na nadhani aliyeandikiwa ataupokea kwa mikono miwili kwani akiukataa atakuwa ana shida...Mtani kazi nzuri nimelipenda hili shairi:-)

    ReplyDelete
  2. Kikazi cha mapenzi,mshairi ndo mtenzi,japo yalianza enzi,mapenzi ki2 azizi,ya2toa bumbuwazi,apendwae hajiwezi

    ReplyDelete