Monday, September 3, 2012

Kalamu yangu andika

Nyerere alishasema, fitna na iwe mwiko,
Tuseme kweli daima, pasi fitini wenzako,
Maneno yenye hekima, yandikwe kila andiko,
Kalamu yangu andika, dunia ipate soma.

Andika pasi kuchoka, hata wamwage risasi,
Nenolo lahitajika, andika tena upesi,
Fikisha ‘nakofikika, ‘siwaogope watesi,
Kalamu yangu andika, dunia ipate soma.

Dunia inasubiri, andika basi haraka,
Weleze yalo dhahiri, wanyonge tumeshachoka,
Amani siyo kamari, mfanye mnavyotaka,
Kalamu yangu andika, dunia ipate soma.

Dunia ipate soma, yaandike kwa uwazi,
Wanakuza uhasama, kutuua kama mbuzi,
Hatupo tena salama, hawataki mageuzi,
Kalamu yangu andika, dunia ipate soma.

Dunia yote ijue, nini kinaendelea,
Hatua izichukue, jahazi kuliokoa,
Jamii ijitambue, izidi kujikomboa,
Kalamu yangu andika, dunia ipate soma.

Wino wako unadumu, usomwe vizazi vyote,
Andiko lako muhimu, lidumu milele yote,
Kwa awamu na dawamu, andika tu usisite,
Kalamu yangu andika, dunia ipate soma.

Ipe dunia ukweli, usiogope risasi,
Wao wasostahimili, huishi kwa wasiwasi,
Viongozi baradhuli, wajue yetu fokasi,
Kalamu yangu andika, dunia ipate soma.

Andika uwaeleze, kamwe haturudi nyuma,
Wao wajiendekeze, chakaribia kiyama,
Waache watuchokoze, hatutaki shika tama,
Kalamu yangu andika.

Fadhy Mtanga,
Mbeya Tanzania.
Jumapili, Septemba 2,2012.

1 comment:

  1. Hakia umeneno tusiwe wannyonge na kukubali kuuwawa kana mbuzi..na wala sidiriki kuogopa kwani hao ni watu kama sisi bila hayo marisasi hawana nguvu. Jamani Tanzania tunakwenda wapi?

    ReplyDelete