Wednesday, September 26, 2012

Wewe ndiyo sababu

Naamka nimejawa tabasamu,
Na kwacho chakula siishiwi hamu,
Furaha yangu yaushinda wazimu,
Moyo wangu una raha muhashamu,
Wewe ndiyo sababu.

Maishani nimejawa na furaha,
Nilishasahau kuhusu karaha,
Najihisi ni kwenye nyota ya jaha,
Hata mwendo wangu hujawa madaha,
Wewe ndiyo sababu.

Ukiwepo huwa kitamu chakula,
Hata usiku kwa raha ninalala,
Napenda niwe nawe kila mahala,
Moyo 'mekolea mapenzi jumla,
Wewe ndiyo sababu.

Wasopendwa nahisi wana taabu,
Ila sitaki juwa yanowasibu,
Raha yangu ni kuwa nawe muhibu,
Nina raha nimepata utabibu,
Wewe ndiyo sababu.

Kwenye mapenzi mie ninafaidi,
Penzi jekundu lishindalo waridi,
Tena ni tamu lilojawa sudi,
Linifanyalo nisihisi baridi,
Wewe ndiyo sababu.

Sasa ninaijua yake thamani,
Penzi la kweli lisilo na kifani,
Nina raha raha kutoka moyoni,
Nina furaha furaha duniani,
Wewe ndiyo sababu.

Fadhy Mtanga,
Mbeya, Tanzania.
Jumatano, Septemba 26, 2012.

Monday, September 24, 2012

Wewe pekee

Nitakupa bega langu uliegamie,
Nitakupa mdomo wangu usemee,
Nitakupa masikio yangu usikilizie,
Nitakupa miguu yangu utembelee,
Kwa kuwa nakupenda sana.

 Dunia nzima nitaiambia isikie,
Tuzo ya thamani ndiwe uistahilie,
Hatokei mtu yeyote wewe akufikie,
Maishani wacha tu nikufurahie,
Uzuriwo umeshinda kawaida.

 Upo kwangu ya nyuma usiyawazie,
Mungu kanionesha wewe nikuchague,
Yanifanya daima wewe nikufikirie,
Penzi lenye thamani nikugaie,
Maana kwangu umeshatosha.

 Wewe pekee!

 Fadhy Mtanga,
Mbeya, Tanzania.
Jumatatu, Septemba 24, 2012.

Monday, September 3, 2012

Kalamu yangu andika

Nyerere alishasema, fitna na iwe mwiko,
Tuseme kweli daima, pasi fitini wenzako,
Maneno yenye hekima, yandikwe kila andiko,
Kalamu yangu andika, dunia ipate soma.

Andika pasi kuchoka, hata wamwage risasi,
Nenolo lahitajika, andika tena upesi,
Fikisha ‘nakofikika, ‘siwaogope watesi,
Kalamu yangu andika, dunia ipate soma.

Dunia inasubiri, andika basi haraka,
Weleze yalo dhahiri, wanyonge tumeshachoka,
Amani siyo kamari, mfanye mnavyotaka,
Kalamu yangu andika, dunia ipate soma.

Dunia ipate soma, yaandike kwa uwazi,
Wanakuza uhasama, kutuua kama mbuzi,
Hatupo tena salama, hawataki mageuzi,
Kalamu yangu andika, dunia ipate soma.

Dunia yote ijue, nini kinaendelea,
Hatua izichukue, jahazi kuliokoa,
Jamii ijitambue, izidi kujikomboa,
Kalamu yangu andika, dunia ipate soma.

Wino wako unadumu, usomwe vizazi vyote,
Andiko lako muhimu, lidumu milele yote,
Kwa awamu na dawamu, andika tu usisite,
Kalamu yangu andika, dunia ipate soma.

Ipe dunia ukweli, usiogope risasi,
Wao wasostahimili, huishi kwa wasiwasi,
Viongozi baradhuli, wajue yetu fokasi,
Kalamu yangu andika, dunia ipate soma.

Andika uwaeleze, kamwe haturudi nyuma,
Wao wajiendekeze, chakaribia kiyama,
Waache watuchokoze, hatutaki shika tama,
Kalamu yangu andika.

Fadhy Mtanga,
Mbeya Tanzania.
Jumapili, Septemba 2,2012.