Friday, August 31, 2012

Nimeshindwa vumilia

Siwezi siwezi tena, siwezi kuvumilia,
Hali miye tena sina, sinayo menizidia,
Usiku nao mchana, nazidi tu kuumia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Mejaribu kujikaza, kinywa nikakizuia,
Mezidi moyo umiza, nafuu h’ijatokea,
Moyo pendo mekoleza, mekolea kuzidia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Mejaribu kutosema, moyo haujatulia,
Juu juu ninahema, kama nataka jifia,
Kwako nilishatuwama, sina ninalosikia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Usingizi siupati, wewe tu nakuwazia,
Nipo hoi hatihati, hatihati kuugua,
Nawaza kila wakati, ni vipi nitakwambia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Nimechoka nimechoka, nimechoka vumilia,
Leo nakwita itika, moyo upate kutua,
Maana ushaniteka, na moyo usharidhia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Nipo hoi taabani, moyo kwako umetua,
Nitakuwa furahani, wewe kinikubalia,
Nimekuweka moyoni, uniweke nawe pia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Chonde chonde muhashamu, nifanye moyo tulia,
Nikupe pendo adhimu, pekee hii dunia,
Pendo liso na awamu, kila siku lachanua,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Nikupe pendo la huba, pendo nalosisimua,
Pendo tele na si haba, moyoni ‘shakujazia,
Pendo mara saba saba, mahaba yalozidia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Siwezi tena kungoja, kusubiri kukwambia,
Moyoni ipo haja, zaidi nitajifia,
Nakupenda wewe mmoja, hakuna nokufikia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Uwe wangu wa milele, name niwe wako pia,
Nikupe mapenzi tele, nawe tayafurahia,
Pamoja huku na kule, kwa raha ilozidia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Nimeshindwa vumilia, nd’o ma’na nimekwambia,
Kwamba ninakuzimia, juu yako naugua,
Natumai mesikia, kisha tanikubalia,
Kwani siwezi himili, kutosema nakupenda.

Fadhy Mtanga,
Mbeya Tanzania.
Ijumaa, Agosti 31, 2012.

Tuesday, August 28, 2012

Upo wapi usikivu?

Mwasema muwasikivu, ati yetu mwasikia,
Ati muwavumilivu, changamoto ‘kiwajia,
Mbona mwatumia nguvu, ukweli wakiwambia?
Upo wapi usikivu?

Upo wapi usikivu, jamii yataka jua,
Tuonacho ni mabavu, jamii kuitishia,
Kwao wasio na nguvu, nyie ndo mwazitumia,
Upo wapi usikivu?

Upo wapi usikivu, mwaishangaza dunia,
Hamna hoja za nguvu, mnazoweza tumia,
Mioyo yenu mikavu, iso na huruma pia,
Upo wapi usikivu?

Twonesheni usikivu, tumechoka vumilia,
Kwani hatuzili mbivu, dawamu ‘mesubiria,
Twa’mbulia maumivu, ‘nayotusababishia,
Upo wapi usikivu?

Twambieni kavu kavu, twaona mwatuchezea,
Fikira zenu chakavu, bora ngazi kuachia,
Mmeshakuwa masuzu, hata kubweteka pia,
Upo wapi usikivu?

Wacha tuseme ‘laivu’, iwe itakavyokua,
Mungwenu labda ‘shivu’, si huyu ‘nomwabudia,
Mungu wetu msikivu, twamwomba atusikia,
Wapi wenu usikivu?

Mabavu yenu mabavu, mwisho utawafikia,
Si punde siku angavu, Mungu atatupatia,
Mola wetu msikivu, hakika atajalia,
Hatuishiwi imani!

Fadhy Mtanga,
Mbeya Tanzania.
28 Agosti 2012.