Thursday, November 10, 2011

Mganga wewe mwenyewe

Wa’ngaika kila siku, ukiwasaka waganga,
Waenda kule na huku, umefika hata Tanga,
Mepeleka hadi kuku, ‘lipokwenda Sumbawanga,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Tajihangaisha bure, kudhani wanakuroga,
Mume usimpapure, ukadhani yeye boga,
Mume simcheze shere, kwayo mambo ya kuiga,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Mume usipomtii, lazima atakuchoka,
Kama wewe husikii, ndoa itaharibika,
Na ndoa haikawii, vivi hivi kuvunjika,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Chunga mwenendo wako, uone kama wafaa,
Wacha kufanya vituko, ndoa itakuchakaa,
Sikudanganye wenzako, kwani dunia hadaa,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Mpe mumeo heshima, naye atakuthamini,
Mwambie kwayo hekima, yaliyo mwako moyoni,
Kubali akikutuma, uwache umajinuni,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Usiufate mkumbo, sijaribu asilani,
Yatakuchachia mambo, wenza wacheke pembeni,
Ndoa hainazo tambo, bali busara kichwani,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Mwanamke mpumbavu, hubomoa nyumba yake,
Na mwanamke mvivu, hajui wajibu wake,
Tena hawi msikivu, labda siku atake,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Watu wakikukosoa, ni vema uwaelewe,
Ndoa kiitia doa, talia wewe mwenyewe,
Wengine wataopoa, kutunza usaidiwe,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

2 comments:

 1. Ahsante kwa ushauri huu kaka Fadhy! lakini nina swali moja je kama mume hamtendei mema mkewe mke inabidi amuheshimu tu? maana kuna wanaume wengine wanachukulia mke ndo afanye kila kitu na ukizingatia ile kauli isemayo wanawake muwatii waume zenu. Ingekuwa safi kama wote tuna/wanaheshimiana sio upande mmoja tu.

  ReplyDelete
 2. "MGANGA WEWE MWENYEWE" (UKWELI)

  Mganga wewe mwenyewe, nusuru huko endako
  Unamroga mwenyewe, kwazo mbaya ila zako
  Yote wayataka wewe, rekebisha mwendo wako
  Mganga wewe mwenyewe, umganguwe mwenzako!

  Kupenda mkapendana, lake yeye liwe lako
  Siyo kuadhiriana, waja hawapa vicheko
  Metakana kwa mapana, leo vya nini vipako?
  Mganga wewe mwenyewe, umganguwe mwenzako!

  Mke kumtii mume, na mume wajibu wako
  Siendeane kinyume, kwenye ndoa hivyo mwiko
  Sijione mfalume, mke kijakazi wako
  Mganga wewe mwenyewe, umganguwe mwenzako!

  Chanzoche ukichunguze, wapi alipo jikwaa
  Kwa pole umtulize, muweke kitako kaa
  Taratibu mueleze, siende kusikofaa
  Mganga wewe mwenyewe, umganguwe mwenzako!

  Mke sifanywe mtumwa, hakize mtimizie
  Kwa uzima na kuumwa, kwa yote muhudumie
  Utakalo hutonyimwa, hatongoja umwambie!
  Mganga wewe mwenyewe, umganguwe mwenzako!

  Umpe uhuru wake, kiasi asizidie
  Acheke na shoga zake, na hali awajulie
  Ajuwe mipaka yake, furutu asifikie
  Mganga wewe mwenyewe, umganguwe mwenzako!

  'Mwanamke mpumbavu', mekulevya huba zake
  'Na mwanamke mvivu', mbona umeganda kwake?
  'Tena hawi msikivu', hutaki akubanduke!
  Mganga wewe mwenyewe, umganguwe mwenzako!

  Kukosa kukosowana, hilo nyote mtambuwe
  Siyo mmoja kujiona, mwenziwe amcharuwe
  Mkamilifu hakuna, mapungufu muyajuwe
  Mganga wewe mwenyewe, umganguwe mwenzako!

  ReplyDelete