Saturday, November 12, 2011

Mbeya twataka amani

Mola nipe ujasiri, leo niyaseme wazi,
Ninene yalo dhahiri, masikio yayajazi,
Siitaki iwe siri, sitaki kigugumizi,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Mbeya twataka amani, tumechoka kuonewa,
Mwatuweka kundi gani, la mchwa ama la chawa?
Mmeuguwa vichwani, pengine mpewe dawa,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Asotaka aondoke, Mbeya akatuachia,
Situfanye tuta’bike, mabavu kuyatumia,
Aondoke ende zake, mji uweze tulia,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Mbeya mahali pazuri, wachache wapaharibu,
Vichwani hawafikiri, huongozwa na gadhabu,
Hudhani umashuhuri, jamii kuiadhibu,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Dada kamwambie kaka, avifungashe virago,
Kaseme tumeshachoka, atuondolee zogo,
Amani in’otoweka, aibebee mpago,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Aondoke ende zake, asirudi tena Mbeya,
Kamwe tusimkumbuke, kwa huo wake ubaya,
Sana asahaulike, fikiraze zilopwaya,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Pamoja tushikamane, kuitetea amani,
Kamwe tusivurugane, wabaya wapigwe chini,
Sisi sote tuungane, kuondoa wafitini,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Tuijenge Mbeya yetu, ili izidi kung’aa,
Ili wale waso utu, wabaki kuishangaa,
Na tusikubali katu, Mbeya yetu iwe jaa,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Chonde chonde waungwana, maneno myasikie,
Ubabe wenu hapana, kwingine mkafanyie,
Kwetu hamna maana, si wagomvi watu sie,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Aende afanye hima, atuwekea usiku,
Atwache sisi salama, kwani sisi siyo kuku,
Aende zake mapema, tutamtoa mkuku,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

5 comments:

 1. Ni kweli jamani naungana na kaka Fadhy tunataka amani Mbeya maana kila kukicha hili kwanini? Acheni vurugu ongezeni amani.

  ReplyDelete
 2. Mbeya tena kulikoni, mabavu si suluhisho,
  Hekima wapi jamani, polisi mu kichekesho,
  Akili sasa kichwani, labda ndo ukaribisho,
  Kuja kwa huyu mgeni, 'sijekawa sababisho.

  ReplyDelete
 3. Kaka Albert umenena. Hivi mbona ulipotea sana ulikuwa wapiiii???

  ReplyDelete
 4. @ Fadhy.....

  MBEYA tena kun'nini, mbona ghafula geuka?
  Si zamani karibuni, 'kuparemba' hukuchoka
  Leo kimezidii nini, zahama gani mezuka?
  Japo sinayo POLENI, tawanusuru RABUKA.

  ReplyDelete