Tuesday, November 1, 2011

Leo ni leo

Kesho kesho ya manyani, wangali hawajajenga,
Ilitokea zamani, nyani nao wakapanga,
Wataka wakae ndani, waache kutangatanga,
Wakaiweka yamini, sasa kipigwe kipenga.

Mwingine kakosekana, wakabaki jiuliza,
Akawasili mchana, kisa akawaeleza,
Mtoto kaugua sana, ikabidi kumwuguza,
“Kesho kwa mapema sana, jambo tutatekeleza”.

Kesho ilipofikia, manyani wakajihimu,
Mwenzao hajatokea, ikawajaza wazimu,
Walipomuulizia, mtotowe kanywa sumu,
Nyani wakajiambia, “basi kesho tulazimu”.

Na kesho kulipokucha, mwenzao haonekani,
Wakadhani kawakacha, kemua nenda mitini,
Mwenzao hakujificha, kewa’leza kulikoni,
Amejikwaa ukucha, damu yatoka doleni.

Nyani sasa wakasema, “hebu tusikilizane”,
Kesho yaenda mrama, na mambo yashindikane,
Tuitumie hekima, mambo haya tupangane,
Mwingine akalalama, vema tusubiriane.

Basi hadi leo hii, nyani wasubiri kesho,
Kesho haiwafikii, pengine yao ‘spesho’,
Sasa hawafikirii, weshaona ni michosho,
Pori hawalikimbii, huko sasa kwao mwisho.

Leo ni leo sikia, asemaye kesho mwongo,
Leo leo ngetumia, kuuchekecha ubongo,
Sipende kusubiria, kesho ufanye mipango,
Kesho haitofikia, hata ngetegea ‘mingle’.

Usiwe kama manyani, hukosi visingizio,
Ziweke vema ‘plan’, yanowezekana leo,
Chekecha vema kichwani, kabla yake machweo,
Tena singoje jioni, muda huu egemeo.

Leo iwe yako ada, kesho siisubirie,
Utumie vema muda, kesho ukusaidie,
Kesho ngeipaka poda, bado situmainie,
Leo hainayo shida, siku yako itumie.

2 comments:

 1. @ Fadhy......

  Simulizi za manyani, na zile za Bulicheka
  Hizo ngano za zamani, baadhi sahaulika
  Loe tosikiza nani, kila mtu chakarika
  Kwa mja leo ni leo, kesho ndiyo ya manyani!

  Wasokaa kwa kituo, tulia japo pangoni
  Lokosa mipangilio, kizeekea mitini
  Kutwa matawini mbio, sojuwa mwisho ni lini?
  Kwa mja leo ni leo, kesho ndiyo ya manyani!

  Kwa lake mja ni leo, kesho angojee nini?
  Akikamata koleo, keshaingia kazini
  Hupima mafanikio, aone kavuna nini
  Kwa mja leo ni leo, kesho ndiyo ya manyani!

  Hana cha kungoja kesho, kijaaliya MANANI
  Hadi aujuwe mwisho, ndipo hatia sainii
  Manyani yao michosho, 'jengo' halipo kichwani
  Kwa mja leo ni leo, kesho ndiyo ya manyani!

  Leo linowezekana, ngoja kesho kulikoni?
  Ni papo hapo kufana, hoja ni kujiamini
  Si manyani nozugana, kesho twajenga 'rosheni'
  Kwa mja leo ni leo, kesho ndiyo ya manyani!

  Ni kuyaweka malengo, na nzuri tathmini
  Haimarisha mipango, na kubuni ya usoni
  Sipokwenda 'songombingo', mia kwa mia mewini
  Kwa mja leo ni leo, kesho ndiyo ya manyani!

  Leo mithili ya zege, lala haliwezekani
  Mbio mbio ulimwage, likiganda mtihani
  Sivyo usilikoroge, kesho kiwaiga nyani
  Kwa mja leo ni leo, kesho ndiyo ya manyani!

  ReplyDelete
 2. Ni kumbukumbu nzuri hii nilianza kuisahau. Ahsante....Kweli leo ni leo asemaye kesho ni mwongo. Kazi nzuri Fadhy!!

  ReplyDelete