Saturday, November 12, 2011

Mbeya twataka amani

Mola nipe ujasiri, leo niyaseme wazi,
Ninene yalo dhahiri, masikio yayajazi,
Siitaki iwe siri, sitaki kigugumizi,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Mbeya twataka amani, tumechoka kuonewa,
Mwatuweka kundi gani, la mchwa ama la chawa?
Mmeuguwa vichwani, pengine mpewe dawa,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Asotaka aondoke, Mbeya akatuachia,
Situfanye tuta’bike, mabavu kuyatumia,
Aondoke ende zake, mji uweze tulia,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Mbeya mahali pazuri, wachache wapaharibu,
Vichwani hawafikiri, huongozwa na gadhabu,
Hudhani umashuhuri, jamii kuiadhibu,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Dada kamwambie kaka, avifungashe virago,
Kaseme tumeshachoka, atuondolee zogo,
Amani in’otoweka, aibebee mpago,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Aondoke ende zake, asirudi tena Mbeya,
Kamwe tusimkumbuke, kwa huo wake ubaya,
Sana asahaulike, fikiraze zilopwaya,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Pamoja tushikamane, kuitetea amani,
Kamwe tusivurugane, wabaya wapigwe chini,
Sisi sote tuungane, kuondoa wafitini,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Tuijenge Mbeya yetu, ili izidi kung’aa,
Ili wale waso utu, wabaki kuishangaa,
Na tusikubali katu, Mbeya yetu iwe jaa,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Chonde chonde waungwana, maneno myasikie,
Ubabe wenu hapana, kwingine mkafanyie,
Kwetu hamna maana, si wagomvi watu sie,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Aende afanye hima, atuwekea usiku,
Atwache sisi salama, kwani sisi siyo kuku,
Aende zake mapema, tutamtoa mkuku,
Mbeya twataka amani, asotaka aondoke.

Thursday, November 10, 2011

Mganga wewe mwenyewe

Wa’ngaika kila siku, ukiwasaka waganga,
Waenda kule na huku, umefika hata Tanga,
Mepeleka hadi kuku, ‘lipokwenda Sumbawanga,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Tajihangaisha bure, kudhani wanakuroga,
Mume usimpapure, ukadhani yeye boga,
Mume simcheze shere, kwayo mambo ya kuiga,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Mume usipomtii, lazima atakuchoka,
Kama wewe husikii, ndoa itaharibika,
Na ndoa haikawii, vivi hivi kuvunjika,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Chunga mwenendo wako, uone kama wafaa,
Wacha kufanya vituko, ndoa itakuchakaa,
Sikudanganye wenzako, kwani dunia hadaa,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Mpe mumeo heshima, naye atakuthamini,
Mwambie kwayo hekima, yaliyo mwako moyoni,
Kubali akikutuma, uwache umajinuni,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Usiufate mkumbo, sijaribu asilani,
Yatakuchachia mambo, wenza wacheke pembeni,
Ndoa hainazo tambo, bali busara kichwani,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Mwanamke mpumbavu, hubomoa nyumba yake,
Na mwanamke mvivu, hajui wajibu wake,
Tena hawi msikivu, labda siku atake,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Watu wakikukosoa, ni vema uwaelewe,
Ndoa kiitia doa, talia wewe mwenyewe,
Wengine wataopoa, kutunza usaidiwe,
Mganga wewe mwenyewe, kunusuru ndoa yako.

Tuesday, November 1, 2011

Leo ni leo

Kesho kesho ya manyani, wangali hawajajenga,
Ilitokea zamani, nyani nao wakapanga,
Wataka wakae ndani, waache kutangatanga,
Wakaiweka yamini, sasa kipigwe kipenga.

Mwingine kakosekana, wakabaki jiuliza,
Akawasili mchana, kisa akawaeleza,
Mtoto kaugua sana, ikabidi kumwuguza,
“Kesho kwa mapema sana, jambo tutatekeleza”.

Kesho ilipofikia, manyani wakajihimu,
Mwenzao hajatokea, ikawajaza wazimu,
Walipomuulizia, mtotowe kanywa sumu,
Nyani wakajiambia, “basi kesho tulazimu”.

Na kesho kulipokucha, mwenzao haonekani,
Wakadhani kawakacha, kemua nenda mitini,
Mwenzao hakujificha, kewa’leza kulikoni,
Amejikwaa ukucha, damu yatoka doleni.

Nyani sasa wakasema, “hebu tusikilizane”,
Kesho yaenda mrama, na mambo yashindikane,
Tuitumie hekima, mambo haya tupangane,
Mwingine akalalama, vema tusubiriane.

Basi hadi leo hii, nyani wasubiri kesho,
Kesho haiwafikii, pengine yao ‘spesho’,
Sasa hawafikirii, weshaona ni michosho,
Pori hawalikimbii, huko sasa kwao mwisho.

Leo ni leo sikia, asemaye kesho mwongo,
Leo leo ngetumia, kuuchekecha ubongo,
Sipende kusubiria, kesho ufanye mipango,
Kesho haitofikia, hata ngetegea ‘mingle’.

Usiwe kama manyani, hukosi visingizio,
Ziweke vema ‘plan’, yanowezekana leo,
Chekecha vema kichwani, kabla yake machweo,
Tena singoje jioni, muda huu egemeo.

Leo iwe yako ada, kesho siisubirie,
Utumie vema muda, kesho ukusaidie,
Kesho ngeipaka poda, bado situmainie,
Leo hainayo shida, siku yako itumie.