Thursday, October 27, 2011

Ukipenda boga

Pendo pendo mwapendana, nyie ni nyie wawili,
Pendo pendo mwashibana, lenu la jambo muhali,
Mwanoga mwaambiana, mwingine hatobadili,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Mapenzi yake matamu, wanogewa na mumeo,
Kamwe haiishi hamu, ana upya kila leo,
Penzi lashika hatamu, huwajali visemeo,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Mumeo umemkuta, anao na ndugu zake,
Binti unafurukuta, hutaki kwako wafike,
Wataka mume kufyata, lako tu nd’o alishike,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Siyo vema mwanakwetu, si tabia yenye sudi,
Nao waoneshe utu, upendo kwao si budi,
Mabezo si malikitu, siwoneshe ukaidi,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Kwa mumeo umekuta, tayari alishazaa,
Kabla hajakupata, akupe wake wasaa,
Mtoto wamkorota, zaidi wamkataa,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Nawe umepata mke, tayari ana mtoto,
Simfanye ateseke, kuiweka nyumba joto,
Haki yake apendeke, siyo kuleta fukuto,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Usipende nusu nusu, nani tena wamwachia,
Yake yote yakuhusu, nayo uyapende pia,
Sisite kumruhusu, nduguze kutembelea,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Mapenzi huleta raha, kwa dhati mkipendana,
Tena huipata siha, kama mwasikilizana,
Siyafanyie mzaha, mkaja kuumizana,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Cha mwenziyo kyone chako, halafu ukithamini,
Kipende moyoni mwako, sikitenge asilani,
Sikifanyie vituko, kamwe kamwe abadani,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Ya kusema nimesema, ni vema kuyasikia,
Yatunze yaliyo mema, kazi ukayafanyia,
Pendo lijae hekima, nyote kulifurahia,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

10 comments:

 1. thanx sana kaka Barton. Pamoja sana mkuu toka zamani.

  ReplyDelete
 2. Shairi la leo limenikumbusha mbali kweli kuna rafiki yangu mmoja kapata mchumba lakini sasa "tatizo" kijana zamani alikuwa na "mke" na akapata mtoto. Na sasa kila kitu kilikuwa tayari kwao msichana alishapata na pete ya uchumba. Alipåoambiwa kuwa kijana atawaleta na watoto wake kukawa ugomvi kwelikweli hataki kabisa watoto wale. "Ukipenda boga penda na ua lake" inaonekana hapa hiyo haipo.

  ReplyDelete
 3. da Yasinta inamaanisha rafikiyo alilipenda sana boga lakini hakuwa tayari kuyapenda maua yake. hilo tatizo lipo sana katika mahusiano mengi sana.

  ReplyDelete
 4. Ndiyo Fadhy...alipenda mno boga na sio maua yake. Ningependa wengi wangepata mwanya na kusoma ujumbe huu na yote unayoandika.

  ReplyDelete
 5. @ Fadhy....

  Vipi boga penda mwanzo, uwale alichukie?
  Hajuwi uwa ndo chanzo, ndipo tunda lifikie
  Hilo halina mzozo, ndo khabari umwambie
  Kidonda akikipenda, usaha asichukie!

  Pendo hapo hushibana, pepo khisi yenu nyie
  Hili lile liwazana, la nani mlisikie?
  Mwendapo mwaongozana, 'kumbi-kumbi' mithilie
  Kidonda akikipenda, usaha asichukie!

  'Chongo' katu kuiona, 'kengeza' jina mtie
  Fukuzana kila kona, mivunguni muingie
  Za ulimi kilishana, nyama mzifurahie
  Kidonda akikipenda, usaha asichukie!

  Mapenzi yao wawili, ndio wasiingilie
  Lakini utu kujali, ukarimu uzidie
  Kwa mume wa kuwajali, ndipo wake wafatie
  Kidonda akikipenda, usaha asichukie!

  Nyumba yote iwe yake, eti umuwachilie?!
  Jimwaga na ndugu zake, nduguzo awachukie!
  Wako mlango sishike, chumbani wake wangie?
  Kidond akikipenda, usaha asichukie!

  Hutaka abimbwe yeye, beba wenziwe alie
  Mume asije 'Mamaye', shemeji asiingie
  Ndani ndugu zake yeye, nje mume wabakie!?
  Kidonda akikipenda, usaha asichukie!

  Awape mahanjumati, wako 'dona' washindie
  Jioni chai chapati, chumba awaandalie
  Wako njozi hawapati, 'boriti' waangalie
  Kidonda akikipenda, usaha asichukie!

  Siyo njema desturi, bora hilo umwambie
  Hefundwa akiwa mwari, kungwi umtafutie?!
  Au ni chake kiburi, hamnazo ajitie
  Kidonda akikipenda, usaha asichukie!

  Mume yote mwelezea, hubani tangu wangie
  La wana kumletea, kwa yote awangalie
  Vipi nje mtolea, ningoje nikuzalie!
  Kidonda akikipenda, usaha asichukie!

  Mapenzi ya nusu nusu, mume ayaangalie
  Ya kupigana mabusu, mithili 'nyenje' walie
  Dharau yanowakhusu, watakuja wajutie
  Kidonda akikipenda, usaha asichukie!

  Tena mapenzi matamu, juu juu yasikie
  Wako sipokudhulumu, nawe umsabilie
  Farakana ni vigumu, kutwa mu-wachanga nyie!
  Kidonda akikipenda, usaha asichukie!

  Chako akifanye chake, na chake umtunzie
  Siwe mbaya roho yake, kwake ngoma awambie
  Huba ndani peke yake, nje yako familie!
  Kidonda akikipenda, usaha asichukie!

  Akikipenda kidonda, usaha avumilie
  Tena kila ukivunda, ndipo raha asikie
  Muda wote kanda kanda, muhusika siumie
  Kidonda akikipenda, usaha asichukie!

  ReplyDelete
 6. Hallyie....

  Mema umekwishasema, ni vema wayasikie,
  Nami ujumbe natuma, waliko uwafikie,
  Uale boga ni jema, si vema walichukie,
  Ili wakipenda boga, ua wasilikimbie.

  ReplyDelete
 7. @ Fadhy.....

  UKIPENDA BOGA (SISITIZO)

  Sio kulifakamia, kula zaidi ya moja
  Chanzoche hakichukia, utakavyo hakifuja
  Kulala chanzo sinzia, ndipo na njozi zikaja
  Kila nolipenda boga, apende na ua lake!

  Lipendwe nalo uwale, bure silitie inda
  Majaniye vile vile, kwa bamia tayapenda
  Matawi huku na kule, ni asiliye kutanda
  Kila nolipenda boga, apende na ua lake!

  ReplyDelete