Tuesday, October 25, 2011

Pole sana Shaaban

Salamu zangu natuma, kwako kipenzi rafiki,
Hali yangu mimi njema, nipo katika mikiki,
Ninamwomba Mungu mwema, akutoe kwenye dhiki,
Pole sana Shaaban, ajali ilokufika.

Hakika nimeshituka, habari kuisikia,
Jasho tele kunitoka, nikatamani kulia,
Kweli nimesikitika, hilo lililotukia,
Pole sana Shaaban, ajali ilokufika.

Rafiki nimeumia, siwezi kuelezea,
Pindi niliposikia, haya yaliyotokea,
Mola ‘takusaidia, twazidi kukuombea,
Pole sana Shaaban, ajali ilokufika.

Twashukuru umepona, ingawa umeumia,
Twafurahi kukuona, hasa yako familia,
Tunamwomba Maulana, afya akakujalia,
Pole sana Shaaban, ajali ilokufika.

Uzima ndiyo muhimu, ndani ya hii dunia,
Daima yatulazimu, huo kuupigania,
Tutimize majukumu, yanayotuangalia,
Pole sana Shaaban, ajali ilokufika.

Mola atakujalia, uweze pona haraka,
Maisha kupigania, kwa kuzidi chakarika,
Mola twa’tumainia, akupe zake baraka,
Pole sana Shaaban, ajali ilokufika.

Shairi hili ni maalumu kwa rafiki yangu na mwanablog mwenzangu Shaban Kaluse aliyepata ajali ya kugongwa na gari leo asubuhi wakati akielekea kazini. Ninamwombe kupona haraka kwa mkono aliovunjika na maumivu mengine aliyoyapata.

2 comments:

 1. POLE SANA SHAABAN.

  Katu nikhusu kwa 'ndewe', alotajwa muhusika
  Wala 'sikio' lenyewe, ila nimei sikitika
  Salama na uuguwe, mkono ulovunjika
  Pole sana Shaaban, atakuafu RABUKA.

  Ajali haina kinga, wala miadi kuweka
  Si mipango nayo panga, vizuri ukajiweka
  Popote yaweza tinga, muhimu kunusurika
  Pole sana Shaaban, atakuafu RABUKA.

  Pole uguwa salama, kubwa upone haraka
  Siha yako iwe njema, kazini vyema tumika
  RABI kuruzuku mema, yenye shari kukwepuka
  Pole sana Shaaban, atakuafu RABUKA.

  ReplyDelete
 2. Pole sana kaka Shaban kwa ajali iliyokupata. Hata hivyo twamshukuru Mungu ingwa umevunjika mkono. Twakuombea upone haraka ili uweze kuwa nasi na kujenga Taifa pia kuwa na familia yako.

  ReplyDelete