Tuesday, October 11, 2011

Ningoje hadi lini?

Mwenzio bado nangoja, ahadi uliyonipa,
Hali yangu reja reja, wala si ya kuchumpa,
Nilishazitowa hoja, basi sinitowe kapa,
Ningoje hadi lini?

Nambie lini wakati, utaponipa majibu,
Moyo kizungumkuti, kwani waupa adhabu,
Hauna tena ukuti, wakusubiri tabibu,
Ningoje hadi lini?

Kwamba nivute subira, nishasubiria sana,
Hadi hali yadorora, usiku nao mchana,
Nitoe kwenye madhara, nishazama kwacho kina,
Ningoje hadi lini?

Jibulo lanipa hamu, hamu ya kulisikia,
Ila sinipe wazimu, chonde sinipe umia,
Likoleze uhashamu, nifurahie dunia,
Ningoje hadi lini?

Usiku wote silali, wewe nakufikiria,
Mwenzio sinayo hali, jibu ninaliwazia,
Chonde mara mbili mbili, niepushie kulia,
Ningoje hadi lini?

Ninakonda ninakonda, nipo hoi taabani,
Chakula kinanishinda, hakinipiti kooni,
Fanya hima kunikanda, unondowe taabuni,
Ningoje hadi lini?

Nieleze yako nia, unondoe wasiwasi,
Nini unadhamiria, mana moyo wenda kasi,
Mwenzio nasubiria, chonde nijibu upesi,
Nimeshangoja sana.

4 comments:

 1. Shairi la laeo mtani bonge la ujumbe kiasi kwamba mtu unasoma mpaka chozi ladondoka. Natumaini utajibiwa karibuni. Kazi nzuri sana NIMELIPENDA...

  ReplyDelete
 2. Kungoja MAUMIVU aisee!Na hata kama kingojewacho ni muda tu ufike kitukiwezachokugeuza DAKIKA kuiona kama mwaka!:-(

  ReplyDelete
 3. da Yasinta najua wewe ni shabiki mkubwa wa mashairi yangu. Ahsante kwa kutonichoka. Yapo mengi yanakuja.

  Mtakatifu Simon ni kweli kabisa ukisemacho!

  ReplyDelete
 4. @ Fadhy.....

  'Subira yavuta kheri', wahenga walitwambia
  Endelea kusubiri, kwa MOLA tumainia
  Omba DUA sighairi, INSHA ALLAH taqabalia
  Ni muda bado timia, usichoke kusubiri.

  Usichoke kusubiri, kama kweli una nia
  Ni mipango ya QAHARI, tupima keshatwambia
  Kwa mabaya na mazuri, imani tuangalia
  Ni muda bado timia, usichoke kusubiri.

  Japo mesubiri sana, sichoke lipobakia
  Vumilia kiungwana, akhiri itafikia
  Shwari uje tulizana, ubaki kukhadithia
  Ni muda bado timia, usichoke kusubiri.

  Jibule sikuhadae, 'tashwishwi' ikakwingia
  Ukatamani upae, alipo kumfikia
  Taratibu jiandae, malengo yatatimia
  Ni muda bado timia, usichoke kusubiri.

  Sijidhuru yako hali, moyoni ukaumia
  Siku haziona mbali, moja ukadhani mia
  Siseme lile na hili, ndo kupenda nakwambia
  Ni muda bado timia, usichoke kusubiri.

  Bure usijikondeshe, taabani hafikia
  Ya nini kucha ukeshe, mchana kijiwazia
  Kwake 'huba' uonyeshe, nung'unu zako achia!
  Ni muda bado timia, usichoke kusubiri.

  'Chonde nijibu upesi', mbona wamkomalia?
  Moyo wako kwenda kasi, mwenyewe wajitakia
  Hebu towa wasi wasi, ni chako kisubiria!
  Ni muda bado timia, usichoke kusubiri.

  Usichoke kusubiri, nazidi kukuusia
  Japo zipite 'dahari', tamati itafikia
  Bora nosubiri kheri, si wa shari harakia
  Ni muda bado timia, usichoke kusubiri.

  ReplyDelete