Sunday, October 30, 2011

Niheshimu nikweshimu

Fanya nawe nitendee, unalopenda tendewa,
Maneno unisemee, unayopenda semewa,
Ikibidi nichekee, kama wapenda chekewa,
Niheshimu nikweshimu, unipende nikupende.

Jambo usilolitaka, nami usinifanyie,
Uniombee baraka, visa usinitilie,
Usiwe wa kuropoka, bali mema unambie,
Niheshimu nikweshimu, unipende nikupende.

Usiwe wa kulalama, jambo usipofanyiwa,
Bali uchunguwe vema, kama huwa wajitowa,
Kiasi unachopima, ndicho hicho tapimiwa,
Niheshimu nikweshimu, unipende nikupende.

Ukitaka sikilizwa, wengine wasikilize,
Ili kama ni kutuzwa, nawe wengine watuze,
Vinginevyo utalizwa, na watu wakuzeveze,
Niheshimu nikweshimu, unipende nikupende.

Cha kwangu ukikitaka, isiwe chako waficha,
Kwangu ukila nafaka, kwako sinilishe kucha,
Nikikupa vya kuoka, nigee japo mchicha,
Niheshimu nikweshimu, unipende nikupende.

Wepesi wa kupokea, uwe na kwenye kutoa,
Kitu mtu kikugea, wewe sibaki kodoa,
Nawe kimpelekea, upamoja hutopoa,
Niheshimu nikweshimu, unipende nikupende.

Heshima ninayokupa, nawe uitoe pia,
Siyo wewe unakwepa, huku yangu watakia,
Sinifanye kukwogopa, daima kunitishia,
Niheshimu nikweshimu, unipende nikupende.

10 comments:

 1. NIHESHIMU NIKUHESHIMU (UKWELI)

  Kitu cha bure heshima, hilo mote fahamika
  Watoto watu wazima, inagusa kila rika
  Kuwekeana lazima, sivukiane mipaka
  Heshima kitu cha bure, heshimu uheshimiwe!

  Silopenda utendewe, na kwa wenzio lipima
  Siwe ukitenda wewe, kitendewa walalama
  Sifu nawe usifiwe, katu tendana dhuluma
  Heshima kitu cha bure, heshimu uheshimiwe!

  Haijalishi umbile, wala rika kutazama
  Cheo hadhi vile vile, si kigezo cha kupima
  Heshima ipale pale, yeyote sije mnyima
  Heshima kitu cha bure, heshimu uheshimiwe!

  Kwa wengi takubalika, heshimayo kiitunza
  Hadhiyo juu taweka, hakuna wa kukubeza
  Nyuma ukiifutika, yaweza ikakuliza
  Heshima kitu cha bure, heshimu uheshimiwe!

  Heshimu kubwa na dogo, lolote litokufika
  Hilo sione mzigo, haja choka kujitwika
  Jepesi ila si dogo, pazuri litakuweka
  Heshima kitu cha bure, heshimu uheshimiwe!

  ReplyDelete
 2. Heshima ni kitu bora. Swali je kama mtu hakuheshimu basi naWE USIMWESHIMU? KWANI UKIMWESHIMU UTAPUNGUKIWA KITU?

  ReplyDelete
 3. @ Yasinta......

  Binafsi naona kama mtu asipokuheshimu, sioni sababu ya wewe kutokumuheshimu, endelea kumuheshimu kama kawaida. Mana tunafaham dhahir kuwa, HESHIMA NI KITU CHA BURE, hakigharimu chochote na wala mtu halazimishwi, Tukumbuke kila mtu na 'silka' yake. Ispokuwa tu, uungwana na ustaarabu, nadhani ni vyema kuendelea kumuheshimu tu! Pasina kutaraji chochote in 'return' na khasa ukizingatia kuwa, hakuna chochote utakachokuwa umepungukiwa.

  ReplyDelete
 4. Ahsante sana kwa maelezo yako Hallyie. Maana nilikuwa najiuliza na mwisho nikaona afadhali nipata msaada. Kama wasemavyo ukiuliza basi utajua mengi.

  ReplyDelete
 5. Hallyie na Yasinta, nakubaliana nanyi kuwa hata kama mtu hatokuheshimu wewe endelea kumheshimu. Maana ya shairi hili si kusema tusiwaheshimu wasiotuheshimu, bali kuwaambia watu endapo wanataka kuheshimiwa, basi nao wajifunze kuheshimu wengine.

  Ahsanteni sana kwa kutonichoka.

  ReplyDelete
 6. @ Fadhy......

  Nanukuu "....Maana ya shairi hili si kusema tusiwaheshimu wasiotuheshimu, bali kuwaambia watu endapo wanataka kuheshimiwa, basi nao wajifunze kuheshimu wengine"

  Fadhy, MAANA ya shairi lako IMEFAHAMIKA sana! Hapo nadhani Yasinta alitaka kufahamu tu inakuwa kuwaje, kufuatia hilo la "Niheshimu nikuheshimu" endapo hali aliyoieleza yeye ikajitokeza, ndio mana akauliza hayo masuali yake hapo juu.

  ReplyDelete
 7. Oh! naona Hallyie umewahi kumjibu Fadhy..Ni kweli sikuwa na maana kwamba sijaelewa shairi HAPANA. Nilichotaka kujua ni hizo tofauti tu. Nashukuru Hallyie!!
  Kapulya

  ReplyDelete
 8. He hee heee, nimeyasoma mashairi yote mawili. Sina swali kama Kapulya

  ReplyDelete
 9. @ Yasinta......

  Akhsante kushkuru! Mana imeibidi nirekebishe huo 'utata' uliojitokeza kwa mujib wa melezo yake alivyojibu (hapo nlipopanukuu).

  ReplyDelete
 10. Ahsanteni sana nyote Hallyie, Yasinta na Chib.

  ReplyDelete