Wednesday, October 26, 2011

Nifanyeje uridhike?

Chonde chonde niambie, nini unachokitaka,
Kingine nikufanyie, ambacho utaridhika,
Niambie nitulie, nimechoka kuteseka,
Nifanyeje uridhike, nambie basi nijue.

Ulitaka yako nyumba, nyumba nayo nikajenga,
Mkopo nikaubamba, wewe uache kupanga,
Ukakataa Kibamba, hutaki wala Ukonga,
Ukataka Mikocheni, nikakopa uridhike.

Nikasema njoo Mbeya, haraka ukakataa,
Ukadai ni kubaya, wataka kuishi Dar,
Nami nikasema haya, nikuridhishe haswaa,
Bado wataka Ulaya, Dar hapajakufaa.

Mara ukataka gari, huzitaki daladala,
Tena gari la fahari, hutaki hizo Corolla,
Nikuridhishe vizuri, nikaenda kopa hela,
Gari umeshalipata, wasema hujaridhika.

Nguo nzuri uzipate, likawa lako sharti,
Tena Mlimani City, vinginevyo varangati,
Kabidi nijikung’ute, ‘sije kukuudhi switi,
Nami pesa nikakopa, nguo uweze nunua.

Ukataka simu kali, bei yake milioni,
Tena ukataka mbili, zote ziwe iPhone,
Waijua yangu hali, lakini hatwelewani,
Simu hizo nimekupa, bado wataka vingine.

Ukataka iPad, laptop huitaki,
Nami nikajitahidi, nikakopa pesa benki,
Nikuridhishe waridi, moyoni ‘lotamalaki,
Wasema huna furaha, bado sana kuridhika.

Ndege ukataka panda, tena ya Lufthansa,
Eti unachokipenda, kutalii Ufaransa,
Moyo sasa wanidunda, utadhani nina kansa,
Sikai nikatulia, mahabuba huridhiki.

Nimefanya kila jambo, nadhani nakuridhisha,
Kumbe wafata mkumbo, wapo wanokufundisha,
Nateseka joto tumbo, mwenzangu unajirusha,
Nini zaidi nifanye, nawe uache nitesa?

13 comments:

 1. Labda ni ule msemo wa binadamu hatusheki. Si unajua watu hata angakuwa na nyumba mia moja lakini bado anataka tu. Mtani natumani karibuni utakuwa safi..unakumbuka hii "mapenzi yana nguvu kuliko mauti"?

  ReplyDelete
 2. mtani naikumbuka sana hiyo kauli. niliiandika kwenye moja ya riwaya zangu. nakumbuka ipo kwenye riwaya ya "Kizungumkuti" pale msichana wa kazi alipomfuta machozi Hafsa kwa kipande cha kanga kutokana na kizungumkuti alichokuwa nacho katika mahusiano. nimekosea?

  ReplyDelete
 3. @ Fadhy......

  Bure sijipe wahaka, kwa kihoro ujifie
  Yasikufike mashaka, kaa moyo utulie
  Nyota njema huoneka, pasi kiza kiingie
  Mja hadi aridhike, ipo kazi nikwambie!

  Hiyo alotaka nyumba, madhilani akutie
  Mwisho uwe omba omba, madeni yakuzidie
  Leo jicho ukifumba, motoni ukaingie?
  Mja hadi aridhike, ipo kazi nikwambie!

  Bure sikupe shengesha, vizuri umwangalie
  Leo ataka Arusha, kesho ila apatie
  Shindwa nini mvurusha, mbali apeperukie
  Mja hadi aridhike, ipo kazi nikwambie!

  Mara kachagiza gari, na madoido atie
  Atataka manowari, nchi kavu atumie
  Ya nini kukuadhiri, uso kaa utulie?!
  Mja hadi aridhike, ipo kazi nikwambie!

  Nguo nzuri azipate, na nakshi uzitie
  Mengine usimfate, mwisho fika uumie
  Hebu chini tema mate, sifike ukufurie
  Mja hadi mridhisha, ipo kazi nikwambie!

  Mwisho atataka 'apple', laptop atumie
  Japo ujuzi haupo, pengine mwenzangu mie
  Ukimbilie mikopo, 'bad debtor' ufikie
  Mja hadi mridhisha, ipo kazi nikwambie!

  Akataka iPad, kundini nae angie
  Kukicha mambo huzidi, ee "MTUME" msalie!
  Lina miba 'uwaridi', hadhari macho singie
  Mja hadi mridhisha, ipo kazi nikwambie!

  Shampandisha 'Lufthansa', 'Emirate' alilie
  Kavinjari ufaranza, Dubai akasinzie
  Yake mambo ya hanasa, si wa nyumba atulie?!
  Mja hadi mridhisha, ipo kazi nikwambie!

  Umefanya kila jambo, kusudi umridhishe
  Kumbe afata mkumbo, kheri kwao mrudishe
  Atachukiza kiambo, nawe hovyo akwendeshe
  Mja hadi mridhisha, ipo kazi nikwambie!

  Hayo ni yangu maoni, japo rafu yapitie
  Sipongia mfukoni, japo chini niwachie
  Saa nyingine haoni, mwenye macho nikwambie
  Mja hadi mridhisha, ipo kazi nikwambie!

  Katu huwa siyo sura, tabia uzingatie
  Huyo ndiyo huwa bora, shidani nyote mlie
  Kamwe kutia idhara, 'faragha' akufichie
  Mja hadi mridhisha, ipo kazi nikwambie!

  ReplyDelete
 4. Hallyie...

  Bure sijipe wahaka, kihoro nijifie,
  Maana nimeshateseka, ninakwambia Hallyie,
  Bora sasa kumwepuka, mwingine 'jitafutie,
  Vipi nikiruka kojo, kisha nikanyage nyesi?

  Ninataka jikwamua, kwingine nijiendee,
  Huyu atajaniua, umri ungali chechee,
  Awali sikumjua, mpenda upedezee,
  Moyo ushakuwa rojo, kheri tu nipate kesi.

  Nigeie basi mbinu, zipi nikazitumie,
  Kutwanga maji kwa kinu, sitaki ijirudie,
  Sitaki iwe fununu, ukweli niwaambie,
  Sipigi tena porojo, niyaamue upesi.

  ReplyDelete
 5. Mtani Fadhy hutakosea ilikuwa huko kwa "Kizungumkuti" .

  Duh! kumwacha huyo itakuwa huzuni kweli. ila lililoamuliwa ndilo.

  ReplyDelete
 6. Mtani ni kweli kabisa, nadhani hata mazingira ya Hafsa kusema vile yalimlazimu aseme vile.

  Hili la kumwacha huyu mpenzi linalazimishwa na tabia yake ya kutoridhika kila afanyiwacho.

  ReplyDelete
 7. Nimekukubali Fadhili sikujua umefanikiwa kufika level hiz JAH bless u brother go much higher.

  ReplyDelete
 8. Anon hapo juu nakushukuru mno kwa kuitembelea blog hii na kuweka maoni. Pia nitashukuru sana ukinifahamisha jina lako maana nina hakika wewe ni mtu ninayefahamiana naye sana.

  Karibu tena na tena blogini humu.

  Alamsiki.

  ReplyDelete
 9. @ Fadhy......

  "Vipi nikiruka kojo, kisha nikanyage nyesi?"
  Taendea mkongojo, takuzeesha upesi
  Matumiziye ya fujo, isitoshe 'muflisi'
  Hana cha kusema 'bojo', wala huruma hakhisi.

  Awali hukumjuwa, haghilibika upesi
  Kwake ukajishauwa, 'malavi-davi na visi'
  Sasa taka kukuuwa, kakukamata ukosi
  Mbali ya kukuzinguwa, madeni subiri kesi.

  "Kutwanga maji kwa kinu, sitaki ijirudie"
  Hapo hakuna cha mbinu, 'naga ubaga' mwambie
  'Bibie urudi kwenu', talaka mvungashie
  Ni wawili kati yenu, ukiridhi abakie.

  "Sipigi tena porojo, niyaamuwe upesi"
  Tepwereshwa rojo-rojo, amuwa tasema basi
  Kesize bwana Kitojo, tamwambia 'dis-misi'
  Atakutowa mikojo, takuchuruza kamasi.

  ReplyDelete
 10. Hallyie...

  Bora sasa niamue, nisije kufa kihoro,
  Uamuzi nichukue, siyo ningoje 'tomorrow',
  Ni bora nijinasue, sitaki kubaki doro,
  Nafungasha zangu miye, sitaki tena taabu!

  ReplyDelete
 11. @ Fadhy......

  Japo yameshwamwagika, ndo hivyo hayazoleki
  Mwenyewe uliyataka, yetu macho yakabaki
  Idhilali lokufika, 'mesarenda' humtaki
  Ona livyo dhoofika, mbavu tupu umebaki!

  "Bora sasa niamuwe, nisije kufa kihoro"
  Vilo vyako achukuwe, haachi hata kiporo
  Ndipo ngebe zikutuwe, ukome ubishororo
  'Mkakasi' usifiwe, ndani zi tele kasoro.

  "Uamuzi nichukuwe, siyo ningoje 'tomorrow'"
  Mbivu na mbichi zijuwe, tena sije 'feel sorrow'
  Huyo mwisho akuuwe, kurembea kwenye karo
  Hiki kile kanunuwe, na pesa hwishi ku-'borrow'

  "Ni bora nijinasuwe, sitaki kubaki doro"
  Kama 'kozi' ichukuwe, usiwe tena wa 'tiro'
  Wengine sikuzuzuwe, wakakufanya ngumbaro
  Kama moja uamuwe, usije ambuwa ziro.

  "Nafungasha zangu miye, sitaki tena taabu!"
  Na 'bai-bai' mwambiye, sijetoka kama bubu
  Wenye moyo waachie, tohimili zake tabu
  Chunguza na utulie, watele wenye adabu.

  ReplyDelete
 12. Hallyie....

  Sasa nimeshafungasha, kigulu na njia miye,
  Kwani alishanichosha, kunifanya nijutiye,
  Sasa pumzi naishusha, wala simhurumiye,
  "Bai-bai" nishasema, nishashika hamsini.

  ReplyDelete
 13. @ Fadhy....

  Wendako wende salama, bukheri ukatulie
  Kutakia kila jema, ya kheri yakushukie
  Atakulinda KARIMA, shari mbali kwepushie
  Kuyamaliza salama, si haba ushukurie.

  ReplyDelete