Tuesday, October 18, 2011

Mwenziyo sinayo khali

Muhashamu muhashamu, ujumbe nakutumia,
Pokea zangu salamu, za mashamshamu pia,
Nimepatwa na wazimu, siachi kukuwazia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Kama mapenzi ni sumu, basi imeniingia,
Nakesha mang’amung’amu, wewe kukufikiria,
Yanienda kasi damu, moyo h’utaki tulia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Moyo ‘ngekuwa na zamu, nawe ningekupatia,
Uzionje zilo humu, zilivyojaa hisia,
Halisi zilizo tamu, wewe nizo kupatia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Naganda kama sanamu, wewe ninakungojea,
Zingali siku zatimu, moyo khali wasemea,
Kwa pendo hili adhimu, wewe tuu kukupea,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Wao wanonituhumu, hawawezi nisumbua,
Kukupenda ‘melazimu, vinginevyo naugua,
Ungali yangu naumu, hapa chini yake jua,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Penzi lisilo awamu, kusema litapungua,
Penzi daima dawamu, moyo wangu we chukua,
Kukupenda ni swaumu, pendo nal’ombea dua,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Sihesabu tarakimu, penzi linavyozidia,
Bali ni mastakimu, hakuna ‘nokufikia,
Hakuna wa kukaimu, nafasi ‘nokupatia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Uzuri wako adimu, wengi wanaulilia,
Wazikoleza fahamu, daima nakuwazia,
Kukupenda ni jukumu, mwingine sitomwachia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Kwako siishiwi hamu, kila siku wazidia,
Mapishi yako matamu, mtu sito’bakishia,
Hakika wewe mwalimu, cheti nakutunukia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Beti kumi zimetimu, wewe nimekwandikia,
Nitapiga hata simu, maneno nikakwambia,
Daima nitajihimu, wimbo nikakuimbia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

7 comments:

 1. @ Fadhy....

  Muhashamu muhashamu, ujumbe wako sikia
  Zimeshafika salamu, na mbwembwe ulizotia
  Usikupande wazimu, nguo ukazichukia
  Ingawa hunayo hali, na subira chukulia!

  Mapenzi katu si sumu, ni wengi wangejifia
  Isiwe mang'amung'amu, wa 'pono' ngejilalia
  Sidunde kama 'kandimu', hebu moyo kutulia
  Ingawa hunayo hali, na subira chukulia!

  'Moyo ngekuwa na zamu', 'duru' zima ngemwachia
  Akayaonja matamu, khisi na zako hisia
  Singekuwepo ugumu, moja tungelisikia
  Ingawa hunayo hali, na subira chukulia

  Gandishwa kama sanamu, 'michelini' achilia
  Ni muda haujatimu, sikhofu siku kimbia
  Wewe nae dam-damu, madhali memridhia
  Ingawa hunayo hali, na subira chukulia!

  Wote wanokutuhumu, mbali wapuuzilia
  Midhali yako 'naumu', fofofo kujilalia
  Na kila penye ugumu, RABI tawaepushia
  Ingawa hunayo hali, na subira chukulia!

  Penzi daima dawamu, awali na akhiria
  Penzi lisilo awamu, hagombania raia
  Penzi mithili 'saumu', 'nawaytu' menuwia
  Ingawa hunayo hali, na subira chukulia!

  Hakuna wa kukaimu, nafasi hatarajia
  Si pokezana kwa zamu, kama kwalindwa doria
  Hadhiye ni maalumu, katu wa kuifikia
  Ingawa hunayo hali, na subira chukulia!

  Uzuri wake adimu, si 'mchina' loingia
  Wakukoleza fahamu, kutwa kucha muwazia
  Mpenda lako jukumu, kama 'jezi' mevalia
  Ingawa hunayo hali, na subira chukulia!

  Kwake huishiwi hamu, kila siku 'chapukia'
  Mapishi yake matamu, vidole wajing'atia
  Fika sifu ni mwalimu, na cheti mtunukia
  Ingawa hunayo hali na subira chukulia!

  Liwe penzi la amani, na imani kuzidia
  Isiwe tamu mwanzoni, mwisho chachu haingia
  Lisitoke uwanjani, La siri ndani bakia
  Ingawa hunayo hali, na sibira chukulia

  ReplyDelete
 2. Fadhy!Nina hakika salamu zako zimefika na zimepokelewa kwa furaha ile ya machozi yaani ya furaha. Ila mtani labda ushauri usipata na wazimu na pata usinginzi .Mvumulivu hula mbivu...Hakika watu wana vipaji..Namwonea wivu huyo aloandikiwa shairi..LOL

  Hallyie! nawe u-mshairi mzuri sana nimependa uliovyomjibu mtani wangu Fadhy:-)

  ReplyDelete
 3. @ Yasinta.....

  Yasinta nnashukuru, 'utunzi' nimo jaribu!
  Mapenzi yatamdhuru, 'mtani' wako mjibu
  Sikukuruke kukuru, ende nayo taratibu!
  Sivyo hatokuwa huru, kutwa kucha muadhibu.

  ReplyDelete
 4. @Yasinta, ahsante sana kwa kutochoka kunitembelea na kuyasoma mashairi yangu. usichoke.

  @Hallyie,

  Siku nyingi zimepita, wala sijakwandikia,
  Si kwamba nimekufuta, mambo yalinizidia,
  Hapa ningali natweta, pilika sijatulia,
  Sana ninakushukuru, diwani kutoichoka.

  Hakika nafarijika, daima napokusoma,
  Wajua kuziandika, tungo zizo kaa vema,
  Kipajicho chasifika, kwa wote wenye hekima,
  Karibu pasi kuchoka, tukikuze Kiswahili.

  ReplyDelete
 5. @ Fadhy.....

  Pirika huwa hazishi, kukicha zinazidia
  Nasi hatukuangushi, tumo kurasa pitia
  Nyuma hatukurejeshi, labda uje tukimbia
  Vaa gwanda kama jeshi, fani hadhi zidishia!

  Nami moja nakereka, kutunga ukikawia
  Tungo moja hadi mwaka, nyingine ndipo fatia
  Sivyo fani novyotaka, raha yake chapukia
  Maisha huzuni weka, zote zote changanyia.

  ReplyDelete
 6. @Hallyie...

  Nami ninafurahia, maisha ya changamoto,
  Mambo kuyapigania, na kuushinda msoto,
  Vema naiweka nia, ushairi kwangu wito,
  Sitochoka kuandika, ndiyo yangu burudani.

  ReplyDelete
 7. @ Fadhy.....

  "NAMI NINAFURAHIA, MAISHA YA CHANGAMOTO"
  Basi nyingi tutungia, na khasa zenye mvuto
  Sihamaki kizitia, za 'chawa' na 'viroboto'
  Wapenzi watachangia, mana 'fasihi' nzito.

  "MAMBO KUYAPIGANIA, NA KUUSHINDA MSOTO"
  Khasa ukitia nia, hutouona uzito
  Utawika TANZANIA, Lilongwe hadi Maputo
  Si mzaha ifanyia, fani hawa ya mpito.

  "VEMA NAIWEKA NIA, USHAIRI KWANGU WITO"
  Na wala hukuvamia, dhamiri tangu utoto
  Na MOLA kakujalia, kakwitika wako wito
  Mbali waweza fikia, kama 'Mjomba Mpoto'

  "SITOCHOKA KUANDIKA, NDIO YANGU BURUDANI"
  Tungo moja kiiweka, ndo basi huonekani
  Miezi itakatika, kirudi tena mgeni
  Juwa raha ya kupika, kila kitu kiwe ndani.

  ReplyDelete