Friday, October 28, 2011

Mungu akisema ndiyo

Maisha ni mbio mbio, hayanayo lelemama,
Ujapo uamkio, kujihimu kwa mapema,
Ushike kitafutio, usibaki kulalama,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Maisha ni harakati, riziki jitafutia,
Uchakarike ‘usweti’, mahali kupafikia,
Uchungu wa mkuyati, nao ukakuingia,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Katika mafanikio, hawakosi maadui,
Wale wafikiriao, kukutenda ubedui,
Wa mapembe masikio, nazo roho za utui,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Wa nukhsi nukhsani, mambo kukuharibia,
Wanoumia rohoni, mambo yakikunyokea,
Watemao mate chini, ukishaipita njia,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Wenye husuda rohoni, pindi ukifanikiwa,
Wenye kusema pembeni, ati umependelewa,
Daima wanotamani, wewe kuharibikiwa,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Wakeshao kwa waganga, kukufanyia mizungu,
Ili uweze boronga, maisha yawe machungu,
Wasochoka kusimanga, kukuwekea kiwingu,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Hakuna wa kuzuia, Mungu akishaamua,
Baraka kikujazia, wengine wajisumbua,
Watabaki kuumia, roho zikiwatufua,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Milango ‘kikufungia, siache kumwomba Mungu,
Yeye takufungulia, kokote chini ya mbingu,
Kheri atakujazia, hata iwe kwa mafungu,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Jifunze sana subira, ila sikose imani,
Omba sana kwa busara, umwombe yeye Manani,
Akwepushie madhara, na roho za wafitini,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Visa wakikufanyia, kamwe siwarudhishie,
Mola atakujalia, mabaya akwepushie,
Baya kikusingizia, Mola akusaidie,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Watahangaika bure, kama Mungu keshasema,
Vyao ni viherehere, na roho zikiwauma,
Waachie ziwafure, wewe zidi tenda mema,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Tayezuia ni nani, Mungu kishakuchagua,
Hawawezi abadani, wakeshe wakiagua,
Mungu siye Athumani, kila mtu amjua,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Usije kata tamaa, kisa wenye roho mbaya,
Waufanyao unaa, mambo kuharibikiya,
Wakwombeao balaa, waache waule chuya,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Hakuna wa kuzuia, Mungu akisema ndiyo,
Ukweli nimekwambia, kaziyo kujua hayo,
Yalo mema simamia, Mola ndiyo kimbiliyo,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

4 comments:

 1. Imani kitu cha ajabu!
  Na kwa waaminio MUNGU , MUNGU akisema ndio hiyo ni NDIO!

  Lakini si yasemekana majibu hupata wenye imani tu na ndio maana kuombewa au Kikombe cha sehemuhehemu kule sio tiba ya wote?

  ReplyDelete
 2. Ni kweli kabisa Mtakatifu Simon. Kwa wale waaminiyo kila litendekalo maishani mwao huhusianisha na mkono wa Mungu.

  Ndo maana kuna waliokwenda Loliondo wakapona, na wengine tofauti.

  ReplyDelete
 3. Imani! Bahati nzuri kila mtu ana yake!

  ReplyDelete
 4. @ Fadhy......

  MAISHA NI MBIO MBIO, HAYANAYO LELEMAMA
  Si maji kwa ufyagio, taka nyuma yasukuma
  MOLA akisema ndio, mja katu kweka nyuma
  Kwake KUN-FAYAKUNU, hana wa kumzuwia.

  MAISHA NI HARAKATI, RIZIKI JITAFUTIA
  Haziwindwi kwa manati, kila mtu ngetumia
  Sheti ujipinde ati, vyema uje kutulia
  Kwake KUN-FAYAKUNU, katu wa kumzuwia.

  KATIKA MAFANIKIO, HAWAKOSI MAADUI
  Wakakufanya mwenzao, mwao nyoyoni hujui
  Kumbe mbaya roho zao, hasidi na mabedui
  Kwake KUN-FAYAKUNU, katu wa kumzuwia.

  WA NUKHSI NUKHSANI, MAMBO KUKUHARIBIA
  Ndio hao mashetani, nyoyoni wanoumia
  Hukerekwa kama nini, yako kwendea sawia
  Kwake KUN-FAYAKUNU, katu wa kumzuwia.

  WENYE HUSUDA ROHONI, PINDI UKIFANIKIWA
  Wao lowanyima nani, hilo shindwa lielewa
  Ni mmoja RAHMANI, nochukuwa na kutowa
  Kwake KUN-FAYAKUNU, katu wa kumzuwia.

  WAKESHAO KWA WAGANGA, KUKUFANYIA MIZUNGU
  Hao hao ndio wanga, amini haki ya MUNGU
  Kiwa huna hukunanga, kipata kwao uchungu
  Kwake KUN-FAYAKUNU, katu wa kumzuwia.

  HAKUNA WA KUZUWIA, MUNGU AKISHAAMUA
  Kwake anokujalia, sekunde katu chukua
  Papo hapo latimia, mja hilo lamuua
  Kwake KUN-FAYAKUNU, katu wa kumzuwia.

  MILANGO KIKUFUNGIA, SIACHE KUMWOMBA MUNGU
  Makosa 'kughufiria', kulinda na walimwengu
  Riziki kukujalia, kwa yote saba mafungu
  Kwake KUN-FAYAKUNU, katu wa kumzuwia.

  JIFUNZE SANA SUBIRA, ILA SIKOSE IMANI
  Mbele yake alo bora, nohimili mitihani
  Akaivuta subira, fata nguzo za IMANI
  Kwake KUN-FAYAKUNU, katu wa kumzuwia.

  VISA WAKIKUFANYIA, KAMWE SIWARUDISHIE
  MOLA wako shitakia, katu siwalipizie
  Tulipa kwenye dunia, akhera atwisabie
  Kwake KUN-FAYAKUNU, katu wa kumzuiwa.

  WATAHANGAIKA BURE, KAMA MUNGU KESHASEMA
  Walodhamiri 'yarure', iwapasukie ngoma
  Kama kuku wachakure, sishindane na KARIMA
  Kwake KUN-FAYAKUNU, katu wa kumzuwia.

  TAYEZUIA NI NANI, MUNGU KESHAKUCHAGUWA
  Bure kwenda ugangani, kwanza wote laaniwa
  Pokonyeka abadani, alopewa keshapewa
  Kwake KUN-FAYAKUNU, katu wa kumzuwia.

  USIJE KATA TAMAA, KISA WENYE ROHO MBAYA
  "HAKKI-LILLAHI" kaa, omba MOLA kwitikiya
  Kwepushe zote balaa, kukidhi lodhamiriya
  Kwake KUN-FAYAKUNU, katu wa kumzuwia.

  HAKUNA WA KUZUWIA, MUNGU AKISEMA NDIYO
  Na 'aya' zimetwambia, "KUN-FAYAKUN" hiyo!
  "Kuwa papo latimia", maana yake ndo hiyo.
  Kwake KUN-FAYAKUNU, katu wa kumzuwia.

  Walimwengu hatuwezi, MUUMBA mvurugia
  Hilo twaamini wazi, ni ziro asilimia
  Ingilia zake kazi, ni 'kufuru' twafikia
  Kwake KUN-FAYAKUNU, katu wa kumzuwia.

  ReplyDelete