Thursday, October 20, 2011

Mpenzi karibu Mbeya

Fanya hima fanya mwaya, uje kunitembelea,
Mie nakusubiriya, moyo wenda peapea,
Mpenzi ufike Mbeya, hamu nawe yazidia,
Mpenzi karibu Mbeya.

Ni kuzuri sana Mbeya, mwenyewe tafurahia,
Wacha maneno mabaya, eti hakujatulia,
Maneno yanowapwaya, mji wautamania,
Mpenzi karibu Mbeya.

Mbeya ni neema tupu, ukija utachanua,
Vyakula wajaza kapu, maradhi hutougua,
Hata ukipenda supu, kuipika ninajua,
Mpenzi karibu Mbeya.

Ardhi ina rutuba, mazao yajiotea,
Utavijaza vibaba, neema waogelea,
Kwetu wala na kushiba, mwenyewe kuchekelea,
Mpenzi karibu Mbeya.

Mbeya utakula ndizi, na makatapera pia,
Mihogo navyo viazi, matembele na bamia,
Wali usotaka nazi, wanoga ninakwambia,
Mpenzi karibu Mbeya.

Mbeya kila kitu kipo, hakika tafurahia,
Maembe hadi maepo, hata na kakao pia,
Na magimbi nayo yapo, wewe yakusubiria,
Mpenzi karibu Mbeya.

Miwa yake ni mitamu, na utaing'ang'ania,
Kwani haiishi hamu, hakika ninakwambia,
Kwakufaa sana humu, hima usijekawia,
Mpenzi karibu Mbeya.

Hali yake burudani, hewa iliyotulia,
Kijibaridi fulani, mwili kichosisimua,
Wala huhitaji feni, kifua kuharibia,
Mpenzi karibu Mbeya.

Mpenzi nakusubiri, Mbeya ndo panakufaa,
Njoo mji ni mzuri, na ukija utang'aa,
Hakika utanawiri, upendeze kila saa,
Mpenzi karibu Mbeya.

14 comments:

 1. @ Fadhy.....

  Tembelewa sio hoja, mie nnavyodhania
  Najuwa utamngoja, stendi ya abiria
  Vipi aja mara moja, au ndio kuhamia?
  Kumradhi yangu hoja, endapo taichukia.

  Naona umekazana, kampeni mpigia
  Hali mwenyewe kanena, huko hapajatulia
  Raha ya jambo kufana, siwe kulazimishia
  Na dalili taziona, kama mja mwenye nia!

  Neema haghilibiki, si makapu magunia!
  Kuuguwa siyo dhiki, kila mja mkutia
  Pengine mtu wa 'wiski', weye supu mtajia?
  Gharamia mishikaki, yeye 'ndafu' alilia.


  Huko alipo kadhofu, au njaa ajifia?
  Pengine shiba minofu, mahanjumati jilia
  Shuwarika hana khofu, ndipo 'nyodo' kufanyia!
  Hata kama u-kipofu, japo kharufu sikia!

  Bamia kunde na ndizi, na vingi lomtajia
  Si aghalabu mpenzi, sishangai kikwambia
  Chuku chuku viso nazi, mara jiko lisusia!
  Chapati mpa viazi, mashaka jitafutia.

  'Miwa yake ni mitamu', michungu wapi sikia?
  Mueleze ya muhimu, 'mandhari' mwisho fatia
  Sizidi nyunyiza sumu, sio wote 'wanobwia'
  Ukibaini ugumu, bado RABI lijalia.

  Wazidi kubembeleza, mithili lazimishia
  Siwe 'pachanga' wacheza, yeye 'boso' kupigia
  Kiwa hivyo hutoweza, Mbeya peke tabakia
  Vyema nalo lichunguza, ni ushauri natia.

  'Mpenzi nakusubiri, Mbeya ndio pakufaa'
  Sijetumia jeuri, taka sitake takaa!
  Nenda kwake mukhiyari, kama Mbeya au 'Daa'
  Huo ndio ushauri, upime kama tafaa.

  ReplyDelete
 2. Mtani Fadhy naona safari hii umekazani kweli. Aise sijui anakusikia kama anakusikia kwa kweli atakuja tu. Maana haya mavyakula mweee! na hali ya hewa inaonekana ni ile ambayo watu hawaumwi umwi kila wakati. Ingakuwa kama ....mmmhh usomapo shairi au mashairi yako mpaka raha kwa kweli: Ahsante kwa kutushirikisha.

  ReplyDelete
 3. Hallyie....

  Mbeya kuna kila kitu, mwenyewe utafurahi,
  Mjini si malikitu, wakosa stafutahi,
  Hata kiwe burungutu, hakuishi kukirihi,
  Bora uje huku Mbeya, ni raha mustarehe!

  Huku wala na kushiba, mjini mnahesabu,
  Hatupimii kibaba, huko ni kisebusebu,
  Mjini furaha haba, huku raha kwa irabu,
  Hallyie karibu Mbeya, utafurahi mwenyewe!

  ReplyDelete
 4. da Yasinta nawe nakushukuru sana kwa kuwa mfuatiliaji mzuri sana wa mashairi yangu. da Yasinta mashairi haya huwa nayaandika kila nipatapo hisia fulani, zaidi nafurahia kuandika mashairi.

  ReplyDelete
 5. nilitaka kusahau, da Yasinta nawe nakukaribisha sana Mbeya.

  ReplyDelete
 6. @ Fadhy.....

  'Mjini si mali kitu', uwache istizahi
  Tele kimbilia watu, ujanja mwenye kuwahi
  Ni maamuzi ya mtu, si wote wanokirahi
  Mote nomoishi watu, khabari ile na hii!

  Wala mpaka kinai, hakuna vya kuhesabu
  Mtu bakhili hafai, mjini kwake adhabu
  Kwa moja siku hakai, ona kama msulubu
  Mote nomoishi watu, mema mazuri sharabu.

  Akhsante nikaribisha, mie sinayo makuu
  Japo togwa kininywesha, kwangu ona siku kuu
  Chochote utonilisha, shukuru mikono juu
  Bora salama maisha, mengine tusinukuu!

  ReplyDelete
 7. Ahsante Fadhy huwezi kujua labda tayari tupo wote Mbeya maana Mbaye ni kubwa:-)

  ReplyDelete
 8. Hallyie....

  "Akhsante nikaribisha, mie sinayo makuu",
  Mbeya itakushibisha, uhemee juu juu,
  Kwenye mazuri maisha, yenye gharama nafuu,
  Niambie lini waja, niweze kukupokea.

  Ujapo aga kabisa, kwenu unakotokea,
  Wapo samaki wa Nyasa, nao watakunogea,
  Utasema hutoki hasa, mambo yeshakunyokea,
  Njoo basi fanya hima, mie ninakungojea.

  ReplyDelete
 9. da Yasinta ni furaha kama nawe upo Mbeya ukifaidi.

  ReplyDelete
 10. @ Fadhy.....

  Kushukuru ni wajibu, moja ya njema tabia
  "Shibe" katu nighilibu, si mtu wa kupapia
  Nimeridhi sina gubu, bukheri nimetulia
  Bajetizo siharibu, seuze nisubiria.

  "Niambie lini waja, niweze kukupokea"
  Katu usijeningoja, miadi sijakwekea
  Wala nako sina haja, nilipo jizowelea
  Sianze funga mkaja, yako bure kudodea!

  "Ujapo aga kabisa, kwenu unakotokea"
  Kikwazo siyo rukhusa, nyendoni sijazowea
  Sighilibiki wa Nyasa, Tanganyika Victoria
  Wa kuridhi nikikosa, kipata jishukuria!

  "Njoo basi fanya hima, mie ninakungojea"
  Na shughulizo jituma, kipato jiongezea
  Siikumbuki 'kalima', dai kwako elekea
  Siyo vyote vinozama, vingine vinaelea!

  ReplyDelete
 11. Hallyie...

  "Kushukuru ni wajibu, moja ya njema tabia",
  Miye sitokughilibu, mwenyewe tafurahia,
  Umeridhi huna gubu, bukheri umetulia,
  Kama umekwisha ridhi, niaje wasua kuja?

  "Katu usijeningoja, miadi sijakwekea",
  Mbona hivyo reja reja, mwenziyo nakungojea,
  Sianze tafuta hoja, za wewe kujitetea,
  Madhali ulisharidhi, fanya hima uje sasa.

  ReplyDelete
 12. @ Fadhy....

  Mjumbe umwelewe, ujumbe alokujia
  Maudhuwi uyajuwe, mjibu sijechupia
  Sijefika uzomewe, hadi na wapita njia
  Tunga si kama 'msewe', seruni hajivalia.

  'Sianze tafuta hoja, za wewe kujitetea"
  Kumbe hushiki kumoja, kokote waelekea?
  Mbona huishi vioja, sema wakakupepea!
  Jumla si reja reja, kamwe sije ningojea!

  ReplyDelete
 13. Hallyie....

  Naogopa kuzomewa, na hao wapita njia,
  Mjumbe nishamwelewa, ujumbe 'lonipatia,
  Huhitaji kungojewa, hivyo unaniambia,
  Kumbe tafika mwenyewe, usiache kuja Mbeya.

  ReplyDelete
 14. @ Fadhy....

  Wajifanya hamnazo, na hali zimetimia
  Cheza ngoma utakazo, macho twakuangalia
  Hilo halina kikwazo, chochote jicharazia
  Ungali kwenye mafunzo, lofuzu tawafikia.

  Hebu silete uzushi, na fani yako isiwe
  Sianze mambo kugushi, hadhari siumbuliwe
  Kinywani mwako hayeshi, hutaki ukaukiwe?
  Tangu ujuwe upishi, taka pika hata mawe!

  "Kumbe tafika mwenyewe, usiache kuja Mbeya"
  Husubiri upigiwe, cheza umeshawadiya
  Shughuli ina mwenyewe, nini sare ikatia?
  Ila hiyo siyo wewe, waache walozoweya!

  ReplyDelete