Saturday, October 29, 2011

Kiburi si maungwana

“Sitaki mimi sitaki”, wakubwa wawaambia,
Mtoto haushikiki, huna unalo sikia,
Na wala huambiliki, ungali hujatulia,
Kiburi si maungwana.

Wauleta ukaidi, wakubwa kuwoneshea,
Kamwe huwezi faidi, wote watakukimbia,
Hata ingefika “Eid”, tabaki kuisikia,
Kiburi si maungwana.

Wakubwa husikilizi, wataka jiamulia,
Jambo hawakuelezi, kiambiwa wachukia,
Wajipa wewe ujuzi, huna usilolijua,
Kiburi si maungwana.

Maneno yako makali, daima wayatumia,
Nywelezo kipilipili, kucha unasimamia,
Hunayo ardhilhali, busara mekuishia,
Kiburi si maungwana.

Dunia rangi rangile, kama hukulitambua,
Dunia mwendo mwendole, takuja kukuumbua,
Dunia cheko chekole, hekima ukiijua,
Kiburi si maungwana.

Kiburi chako kiwache, hata Mungu achukia,
Tabiayo ipekeche, watu kuifurahia,
Mabayayo uyafiche, jalala kuyatupia,
Kiburi si maungwana.

8 comments:

 1. KIBURI SI MAUNGWANA (MKAZO)

  Uwe vipi muungwana, hadhiyo hukushushia
  Jeuri wakakuona, mtaani kuchukia
  'Pesa mbili huna mana', semwa na wapita njia
  Si mali hafumbatia, kiburi si maungwana.

  Kiburi si maungwana, si malezi hakulia
  Jabari ukajiona, hovyo watu fyatukia
  Ukaidi kushindana, wakubwa katu sikia
  Si mali hafumbatia, kiburi si maugwana.

  Kila kitu ujuwaji, midomo kibenulia
  Huku jifanya wa mji, 'cheo' kuking'ang'ania
  Stahamili hungoji, na subira huna pia
  Si mali hafumbatia, kiburi si maungwana.

  Usojuwa inswafu, wala vya kuitumia
  Kalima zako ni chafu, 'lindi' kheri mara mia
  Mithili 'gundu' kharufu, kote mehanikizia
  Si mali hafumbatia, kiburi si maungwana.

  Wala siyo ufakhari, sidhani wakusifia
  Kamwe sio uhodari, tuzo ngekuandalia
  Randiamo wakunyari, mate kikutema pia
  Si mali hafumbatia, kiburi si maungwana.

  Urekebishe mwenendo, mapema hujakawia
  Ujijengee upendo, utu kuuzingatia
  Ukuepuke uvundo, sifa njema kunukia
  Si mali hafumbatia, kiburi si maungwana.

  ReplyDelete
 2. hivi kiburi na ubishi ni sawa? nimewaza tu kwa sauti...

  ReplyDelete
 3. @ Yasinta....

  KIBURI na UBISHI kwa nnavyofaham mie siyo sawa.

  Mfano wa KIBURI, mathalan unapita pahala fulani na unawakuta watu ambao ni wakubwa zako ambao unawafaham kwa njia moja au nyingine, huku unajuwa fika, watu hao wangestahili kusalimiwa au kuwajulia hali kwa namna moja au nyingine. Badala yake ukawapita kimya kimya hali umewaona hivi! Badala yake ukajifanya kama vile huna macho na kuwapita kimya! Sasa hicho ndio naweza kusema ni KIBURI, au mtu anaweza kusema.....fulani ana KIBURI, mana kawapita wakubwa zake pale kama vile hajawaona, mana hata salam tu imemshinda kutowa.

  Kwa mfano unaambiwa miguu ya Kuku haifanani na ya Bata, lakini ukawa umeshikilia na kulazimisha kuwa inafanana, hukubali kushindwa juu ya hilo, il-hali kila mtu anaiyona wazi kuwa kuna tofauti kati ya miguu hiyo, lakini wewe tu peke yako ukawa umeshikilia kuwa haina tofauti yeyote na kudai kuwa inafanana, sasa huo ndio tunaweza kusema ni UBISHI. Mana hutaki kushindwa wakati ukweli upo wazi kabisa!

  ReplyDelete
 4. Hallyie...

  Shukuriya kwa mkazo, ambao umeuweka,
  Hakika metowa funzo, ambalo laeleweka,
  Kiburi ni matatizo, ni vema kukiepuka,
  Kiburi si maungwana.

  ReplyDelete
 5. da Yasinta, nadhani Hallyie amekuondolea utata juu ya Kiburi na Ubishi. nami nimejifunza jambo kubwa hapa.

  Ahsante sana Yasinta.

  Ahsante sana Hallyie.

  ReplyDelete
 6. @ Fadhy.....

  SHUKURIA KWA MKAZO, AMBAO UMEUWEKA
  Nawe pia lako wazo, shairi hilo andika
  Maudhuwi si mchezo, ambayo limetutika
  KIBURI jama si nguzo, siegame taanguka!

  ReplyDelete
 7. @ Yasinta....

  Nawe kadhalika, shukran!

  ReplyDelete