Sunday, October 30, 2011

Niheshimu nikweshimu

Fanya nawe nitendee, unalopenda tendewa,
Maneno unisemee, unayopenda semewa,
Ikibidi nichekee, kama wapenda chekewa,
Niheshimu nikweshimu, unipende nikupende.

Jambo usilolitaka, nami usinifanyie,
Uniombee baraka, visa usinitilie,
Usiwe wa kuropoka, bali mema unambie,
Niheshimu nikweshimu, unipende nikupende.

Usiwe wa kulalama, jambo usipofanyiwa,
Bali uchunguwe vema, kama huwa wajitowa,
Kiasi unachopima, ndicho hicho tapimiwa,
Niheshimu nikweshimu, unipende nikupende.

Ukitaka sikilizwa, wengine wasikilize,
Ili kama ni kutuzwa, nawe wengine watuze,
Vinginevyo utalizwa, na watu wakuzeveze,
Niheshimu nikweshimu, unipende nikupende.

Cha kwangu ukikitaka, isiwe chako waficha,
Kwangu ukila nafaka, kwako sinilishe kucha,
Nikikupa vya kuoka, nigee japo mchicha,
Niheshimu nikweshimu, unipende nikupende.

Wepesi wa kupokea, uwe na kwenye kutoa,
Kitu mtu kikugea, wewe sibaki kodoa,
Nawe kimpelekea, upamoja hutopoa,
Niheshimu nikweshimu, unipende nikupende.

Heshima ninayokupa, nawe uitoe pia,
Siyo wewe unakwepa, huku yangu watakia,
Sinifanye kukwogopa, daima kunitishia,
Niheshimu nikweshimu, unipende nikupende.

Saturday, October 29, 2011

Kiburi si maungwana

“Sitaki mimi sitaki”, wakubwa wawaambia,
Mtoto haushikiki, huna unalo sikia,
Na wala huambiliki, ungali hujatulia,
Kiburi si maungwana.

Wauleta ukaidi, wakubwa kuwoneshea,
Kamwe huwezi faidi, wote watakukimbia,
Hata ingefika “Eid”, tabaki kuisikia,
Kiburi si maungwana.

Wakubwa husikilizi, wataka jiamulia,
Jambo hawakuelezi, kiambiwa wachukia,
Wajipa wewe ujuzi, huna usilolijua,
Kiburi si maungwana.

Maneno yako makali, daima wayatumia,
Nywelezo kipilipili, kucha unasimamia,
Hunayo ardhilhali, busara mekuishia,
Kiburi si maungwana.

Dunia rangi rangile, kama hukulitambua,
Dunia mwendo mwendole, takuja kukuumbua,
Dunia cheko chekole, hekima ukiijua,
Kiburi si maungwana.

Kiburi chako kiwache, hata Mungu achukia,
Tabiayo ipekeche, watu kuifurahia,
Mabayayo uyafiche, jalala kuyatupia,
Kiburi si maungwana.

Friday, October 28, 2011

Mungu akisema ndiyo

Maisha ni mbio mbio, hayanayo lelemama,
Ujapo uamkio, kujihimu kwa mapema,
Ushike kitafutio, usibaki kulalama,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Maisha ni harakati, riziki jitafutia,
Uchakarike ‘usweti’, mahali kupafikia,
Uchungu wa mkuyati, nao ukakuingia,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Katika mafanikio, hawakosi maadui,
Wale wafikiriao, kukutenda ubedui,
Wa mapembe masikio, nazo roho za utui,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Wa nukhsi nukhsani, mambo kukuharibia,
Wanoumia rohoni, mambo yakikunyokea,
Watemao mate chini, ukishaipita njia,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Wenye husuda rohoni, pindi ukifanikiwa,
Wenye kusema pembeni, ati umependelewa,
Daima wanotamani, wewe kuharibikiwa,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Wakeshao kwa waganga, kukufanyia mizungu,
Ili uweze boronga, maisha yawe machungu,
Wasochoka kusimanga, kukuwekea kiwingu,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Hakuna wa kuzuia, Mungu akishaamua,
Baraka kikujazia, wengine wajisumbua,
Watabaki kuumia, roho zikiwatufua,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Milango ‘kikufungia, siache kumwomba Mungu,
Yeye takufungulia, kokote chini ya mbingu,
Kheri atakujazia, hata iwe kwa mafungu,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Jifunze sana subira, ila sikose imani,
Omba sana kwa busara, umwombe yeye Manani,
Akwepushie madhara, na roho za wafitini,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Visa wakikufanyia, kamwe siwarudhishie,
Mola atakujalia, mabaya akwepushie,
Baya kikusingizia, Mola akusaidie,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Watahangaika bure, kama Mungu keshasema,
Vyao ni viherehere, na roho zikiwauma,
Waachie ziwafure, wewe zidi tenda mema,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Tayezuia ni nani, Mungu kishakuchagua,
Hawawezi abadani, wakeshe wakiagua,
Mungu siye Athumani, kila mtu amjua,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Usije kata tamaa, kisa wenye roho mbaya,
Waufanyao unaa, mambo kuharibikiya,
Wakwombeao balaa, waache waule chuya,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Hakuna wa kuzuia, Mungu akisema ndiyo,
Ukweli nimekwambia, kaziyo kujua hayo,
Yalo mema simamia, Mola ndiyo kimbiliyo,
Mungu akisema ndiyo, hakuna wa kuzuia.

Thursday, October 27, 2011

Ukipenda boga

Pendo pendo mwapendana, nyie ni nyie wawili,
Pendo pendo mwashibana, lenu la jambo muhali,
Mwanoga mwaambiana, mwingine hatobadili,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Mapenzi yake matamu, wanogewa na mumeo,
Kamwe haiishi hamu, ana upya kila leo,
Penzi lashika hatamu, huwajali visemeo,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Mumeo umemkuta, anao na ndugu zake,
Binti unafurukuta, hutaki kwako wafike,
Wataka mume kufyata, lako tu nd’o alishike,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Siyo vema mwanakwetu, si tabia yenye sudi,
Nao waoneshe utu, upendo kwao si budi,
Mabezo si malikitu, siwoneshe ukaidi,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Kwa mumeo umekuta, tayari alishazaa,
Kabla hajakupata, akupe wake wasaa,
Mtoto wamkorota, zaidi wamkataa,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Nawe umepata mke, tayari ana mtoto,
Simfanye ateseke, kuiweka nyumba joto,
Haki yake apendeke, siyo kuleta fukuto,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Usipende nusu nusu, nani tena wamwachia,
Yake yote yakuhusu, nayo uyapende pia,
Sisite kumruhusu, nduguze kutembelea,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Mapenzi huleta raha, kwa dhati mkipendana,
Tena huipata siha, kama mwasikilizana,
Siyafanyie mzaha, mkaja kuumizana,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Cha mwenziyo kyone chako, halafu ukithamini,
Kipende moyoni mwako, sikitenge asilani,
Sikifanyie vituko, kamwe kamwe abadani,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Ya kusema nimesema, ni vema kuyasikia,
Yatunze yaliyo mema, kazi ukayafanyia,
Pendo lijae hekima, nyote kulifurahia,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Wednesday, October 26, 2011

Nifanyeje uridhike?

Chonde chonde niambie, nini unachokitaka,
Kingine nikufanyie, ambacho utaridhika,
Niambie nitulie, nimechoka kuteseka,
Nifanyeje uridhike, nambie basi nijue.

Ulitaka yako nyumba, nyumba nayo nikajenga,
Mkopo nikaubamba, wewe uache kupanga,
Ukakataa Kibamba, hutaki wala Ukonga,
Ukataka Mikocheni, nikakopa uridhike.

Nikasema njoo Mbeya, haraka ukakataa,
Ukadai ni kubaya, wataka kuishi Dar,
Nami nikasema haya, nikuridhishe haswaa,
Bado wataka Ulaya, Dar hapajakufaa.

Mara ukataka gari, huzitaki daladala,
Tena gari la fahari, hutaki hizo Corolla,
Nikuridhishe vizuri, nikaenda kopa hela,
Gari umeshalipata, wasema hujaridhika.

Nguo nzuri uzipate, likawa lako sharti,
Tena Mlimani City, vinginevyo varangati,
Kabidi nijikung’ute, ‘sije kukuudhi switi,
Nami pesa nikakopa, nguo uweze nunua.

Ukataka simu kali, bei yake milioni,
Tena ukataka mbili, zote ziwe iPhone,
Waijua yangu hali, lakini hatwelewani,
Simu hizo nimekupa, bado wataka vingine.

Ukataka iPad, laptop huitaki,
Nami nikajitahidi, nikakopa pesa benki,
Nikuridhishe waridi, moyoni ‘lotamalaki,
Wasema huna furaha, bado sana kuridhika.

Ndege ukataka panda, tena ya Lufthansa,
Eti unachokipenda, kutalii Ufaransa,
Moyo sasa wanidunda, utadhani nina kansa,
Sikai nikatulia, mahabuba huridhiki.

Nimefanya kila jambo, nadhani nakuridhisha,
Kumbe wafata mkumbo, wapo wanokufundisha,
Nateseka joto tumbo, mwenzangu unajirusha,
Nini zaidi nifanye, nawe uache nitesa?

Tuesday, October 25, 2011

Pole sana Shaaban

Salamu zangu natuma, kwako kipenzi rafiki,
Hali yangu mimi njema, nipo katika mikiki,
Ninamwomba Mungu mwema, akutoe kwenye dhiki,
Pole sana Shaaban, ajali ilokufika.

Hakika nimeshituka, habari kuisikia,
Jasho tele kunitoka, nikatamani kulia,
Kweli nimesikitika, hilo lililotukia,
Pole sana Shaaban, ajali ilokufika.

Rafiki nimeumia, siwezi kuelezea,
Pindi niliposikia, haya yaliyotokea,
Mola ‘takusaidia, twazidi kukuombea,
Pole sana Shaaban, ajali ilokufika.

Twashukuru umepona, ingawa umeumia,
Twafurahi kukuona, hasa yako familia,
Tunamwomba Maulana, afya akakujalia,
Pole sana Shaaban, ajali ilokufika.

Uzima ndiyo muhimu, ndani ya hii dunia,
Daima yatulazimu, huo kuupigania,
Tutimize majukumu, yanayotuangalia,
Pole sana Shaaban, ajali ilokufika.

Mola atakujalia, uweze pona haraka,
Maisha kupigania, kwa kuzidi chakarika,
Mola twa’tumainia, akupe zake baraka,
Pole sana Shaaban, ajali ilokufika.

Shairi hili ni maalumu kwa rafiki yangu na mwanablog mwenzangu Shaban Kaluse aliyepata ajali ya kugongwa na gari leo asubuhi wakati akielekea kazini. Ninamwombe kupona haraka kwa mkono aliovunjika na maumivu mengine aliyoyapata.

Thursday, October 20, 2011

Mpenzi karibu Mbeya

Fanya hima fanya mwaya, uje kunitembelea,
Mie nakusubiriya, moyo wenda peapea,
Mpenzi ufike Mbeya, hamu nawe yazidia,
Mpenzi karibu Mbeya.

Ni kuzuri sana Mbeya, mwenyewe tafurahia,
Wacha maneno mabaya, eti hakujatulia,
Maneno yanowapwaya, mji wautamania,
Mpenzi karibu Mbeya.

Mbeya ni neema tupu, ukija utachanua,
Vyakula wajaza kapu, maradhi hutougua,
Hata ukipenda supu, kuipika ninajua,
Mpenzi karibu Mbeya.

Ardhi ina rutuba, mazao yajiotea,
Utavijaza vibaba, neema waogelea,
Kwetu wala na kushiba, mwenyewe kuchekelea,
Mpenzi karibu Mbeya.

Mbeya utakula ndizi, na makatapera pia,
Mihogo navyo viazi, matembele na bamia,
Wali usotaka nazi, wanoga ninakwambia,
Mpenzi karibu Mbeya.

Mbeya kila kitu kipo, hakika tafurahia,
Maembe hadi maepo, hata na kakao pia,
Na magimbi nayo yapo, wewe yakusubiria,
Mpenzi karibu Mbeya.

Miwa yake ni mitamu, na utaing'ang'ania,
Kwani haiishi hamu, hakika ninakwambia,
Kwakufaa sana humu, hima usijekawia,
Mpenzi karibu Mbeya.

Hali yake burudani, hewa iliyotulia,
Kijibaridi fulani, mwili kichosisimua,
Wala huhitaji feni, kifua kuharibia,
Mpenzi karibu Mbeya.

Mpenzi nakusubiri, Mbeya ndo panakufaa,
Njoo mji ni mzuri, na ukija utang'aa,
Hakika utanawiri, upendeze kila saa,
Mpenzi karibu Mbeya.

Tuesday, October 18, 2011

Mwenziyo sinayo khali

Muhashamu muhashamu, ujumbe nakutumia,
Pokea zangu salamu, za mashamshamu pia,
Nimepatwa na wazimu, siachi kukuwazia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Kama mapenzi ni sumu, basi imeniingia,
Nakesha mang’amung’amu, wewe kukufikiria,
Yanienda kasi damu, moyo h’utaki tulia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Moyo ‘ngekuwa na zamu, nawe ningekupatia,
Uzionje zilo humu, zilivyojaa hisia,
Halisi zilizo tamu, wewe nizo kupatia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Naganda kama sanamu, wewe ninakungojea,
Zingali siku zatimu, moyo khali wasemea,
Kwa pendo hili adhimu, wewe tuu kukupea,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Wao wanonituhumu, hawawezi nisumbua,
Kukupenda ‘melazimu, vinginevyo naugua,
Ungali yangu naumu, hapa chini yake jua,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Penzi lisilo awamu, kusema litapungua,
Penzi daima dawamu, moyo wangu we chukua,
Kukupenda ni swaumu, pendo nal’ombea dua,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Sihesabu tarakimu, penzi linavyozidia,
Bali ni mastakimu, hakuna ‘nokufikia,
Hakuna wa kukaimu, nafasi ‘nokupatia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Uzuri wako adimu, wengi wanaulilia,
Wazikoleza fahamu, daima nakuwazia,
Kukupenda ni jukumu, mwingine sitomwachia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Kwako siishiwi hamu, kila siku wazidia,
Mapishi yako matamu, mtu sito’bakishia,
Hakika wewe mwalimu, cheti nakutunukia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Beti kumi zimetimu, wewe nimekwandikia,
Nitapiga hata simu, maneno nikakwambia,
Daima nitajihimu, wimbo nikakuimbia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.

Tuesday, October 11, 2011

Ningoje hadi lini?

Mwenzio bado nangoja, ahadi uliyonipa,
Hali yangu reja reja, wala si ya kuchumpa,
Nilishazitowa hoja, basi sinitowe kapa,
Ningoje hadi lini?

Nambie lini wakati, utaponipa majibu,
Moyo kizungumkuti, kwani waupa adhabu,
Hauna tena ukuti, wakusubiri tabibu,
Ningoje hadi lini?

Kwamba nivute subira, nishasubiria sana,
Hadi hali yadorora, usiku nao mchana,
Nitoe kwenye madhara, nishazama kwacho kina,
Ningoje hadi lini?

Jibulo lanipa hamu, hamu ya kulisikia,
Ila sinipe wazimu, chonde sinipe umia,
Likoleze uhashamu, nifurahie dunia,
Ningoje hadi lini?

Usiku wote silali, wewe nakufikiria,
Mwenzio sinayo hali, jibu ninaliwazia,
Chonde mara mbili mbili, niepushie kulia,
Ningoje hadi lini?

Ninakonda ninakonda, nipo hoi taabani,
Chakula kinanishinda, hakinipiti kooni,
Fanya hima kunikanda, unondowe taabuni,
Ningoje hadi lini?

Nieleze yako nia, unondoe wasiwasi,
Nini unadhamiria, mana moyo wenda kasi,
Mwenzio nasubiria, chonde nijibu upesi,
Nimeshangoja sana.