Thursday, September 1, 2011

Moyo wangu

Usiuache mpweke, maumivu kuufika,
Siufanye uteseke, machozi yakanitoka,
Ufanye ufarijike, upe moyo uhakika,
Moyo wangu.

Upatie unafuu, upunguzie mawazo,
Uweke daima juu, sikalie matatizo,
Siupige kwa miguu, na kuupa mizevezo,
Moyo wangu.

Uondolee karaha, siuweke taabuni,
Ufanye kuwa na raha, sizamishe majonzini,
Utawalwe na furaha, cheko tupu maishani,
Moyo wangu.

Usiutendee hivyo, moyo wangu taumia,
Ukitenda ndivyo sivyo, kitanzi utautia,
Vyovyote vile iwavyo, elewa wakuzimia,
Moyo wangu.

2 comments:

  1. Kilio chako anakisikia
    Ondoa wasiwasi. Nadhani hangependa uumia moyo wako, tuliza moyo siku moja mtakuwa pamoja na mtacheka maisha yote...

    ReplyDelete