Wednesday, August 3, 2011

Waambie

Ukiwa nao waambie, maneno yawafikie,
Jitahidi wasikie, ujumbe uwafikie,
Ili wasiulizie, bure wasijisumbue,
Waambie hao wote, umenichagua mie.

Wakate vyao vilimi, ikibidi waumie,
Sema wanipenda mimi, waambie wasikie,
Sema mara kumi kumi, sauti iwafikie,
Waambie hao wote, kuwa wanipenda mie.

Hawapendi ninajua, we’ waache waumie,
Wivu unawasumbua, watamani watibue,
Sie tunaomba dua, Muumba atujalie,
Waambie hao wote, umenichagua mi.

Waambie wafitini, na chuki zao walie,
Na wala wasijihini, hawatotuweza sie,
Tumeshazama dimbwini, tumeshanogewa sie,
Waambie hao wote, kuwa wanipenda mie.

We’ waambie mpenzi, yawachome waumie,
Na zidisha kunienzi, ili nifaidi mie,
Niyafaidi mapenzi, pendolo nijivunie,
Waambie hao wote, umenichagua mie.

Mpenzi we’ u mzuri, yeyote asikwambie,
Unanipa ufahari, na raha usisikie,
Nasi twombeane kheri, mapenzi yetu yakue,
Waambie hao wote, kuwa wanipenda mie.

Waseme hata wachoke, wacha tupendane sie,
Kote kote wazunguke, watashindwa wajijue,
Na watake wasitake, siye tuyafurahie,
Waambie hao wote, umenichagua mie.

Hata washikwe na wivu, wenyewe nd’o waumie,
Sie twala zetu mbivu, watwache tufurahie,
Wayapate maumivu, mioyoni waumie,
Waambie hao wote, kuwa wanipenda mie.

Watayasema mchana, ngoja giza liingie,
Watalala tena sana, na ndoto ziwasumbue,
Tutazidi kupendana, watakoma wakomae,
Waambie hao wote, umenichagua mie.

Hujachagua mwingine, isipokuwa ni mie,
Hivyo nasi tupendane, raha na tujipatie,
Wao wahangaishane, sie wasitufikie,
Waambie hao wote, kuwa wanipenda mie.

Waambie wasikie, nenolo liwainngie,
Tena wasijisumbue, mapenzi ni yetu sie,
Waumie siumie, tunajivinjari sie,
Waambie hao wote, umenichagua mie.

Waambie wasikie!

2 comments:

 1. Wambie yenye maana, vichwani yawaingie
  Waeleze kiungwana, 'chonde' siwahamakie
  Msije hasimiana, na dhambini wakutie
  Wambie metulizana, tena huru wakwachie!

  Waeleze kwa upole, kelele siwapigie
  Wape kweli vile vile, bayana waanikie
  Mempata wa milele, 'INSHA ALLAH' na mtulie
  Wambie metulizana, tena huru wakwachie!

  Wivu sikushughulishe, lazima wakulilie
  Vidonda siwatoneshe, siwafanye waumie
  Na zogo lao wapishe, bukheri vyako jilie
  Wambie metulizana, tena huru wakwachie!

  Sana tasema mchana, usiku wajilalie
  Jilia vyako kazana, wao nawa waishie
  Atakulinda 'Rabana', husuda akwepushie
  Wambie metulizana, tena huru wakwachie!

  ReplyDelete
 2. Hallyie....

  Waambie waambie, waambie wasikie,
  Maneno yawaingie, wivu wao waumie,
  Wenzao wa'simulie, kijicho watuonee,
  Waambie, wache ulizana!

  Maneno yawakolee, wache watufikirie,
  Nasi tuyazidishie, kamwe wasitwingilie,
  Wakeshe wasisinzie, hata mbali w'ulizie,
  Waambie, wache ulizana!

  ReplyDelete