Thursday, August 25, 2011

Sauti yangu

Ninataka kuipaza, ilokaza,
Kotekote kueneza, nacho waza,
Wote muje kusikiza, mkiweza,
Nayoeleza!

Kuna mambo yanikwaza, yanumiza,
Kukimya sitokuweza, tonyamaza,
Silali kucha nawaza, nahasiza,
Wanichagiza!

Niaje yazidi oza, yachakaza,
Vyote vyema wamaliza, wakombeza,
Ni lini watabakiza, wandekeza,
Mauzauza!

Sauti yangu napaza, nakataza,
Mola fimbo wacharaza, tena kaza,
Wajutie wao kwanza, wamaliza,
Wavokombeza!

4 comments:

 1. Sautiyo imesikika, hata ile iliyokaza'
  Kwa hiyo sasa hutoumia sana
  kwani marafiki na wengine wamekusikia
  Ahsante kwa kupaza sauti yako.

  ReplyDelete
 2. @ Fadhy....

  Sautiyo ilokaza, ipaze wakusikie
  Uwazayo yaeleza, hata chembe sibanie
  Vipenuni lojibanza, ujumbe uwafikie
  Ipaze tukusikie!

  Yote yanayo kukwaza, hadharani jinadie
  Sijipe kucha kuwaza, ndani ndani uumie
  Sema wanokuchagiza, 'jalada' wafungulie
  Ipaze tukusikie!

  'Baragumu' lipuliza, pande zote wasikie
  Bayana kuwaeleza, mafumbo usitumie
  Jiamini utaweza, siyo 'nyau' utishie
  Ipaze tukusikie!

  ReplyDelete
 3. Yasinta....

  Sauti imesikika, tena imekufikia,
  Ndo sababu hujachoka, mwingine ukamwambia,
  Naye kwingine peleka, ujumbe lokusudia,
  Sauti imesikika!

  ReplyDelete
 4. Hallyie....

  Sauti ninaikaza, mbali iweze fikia,
  Kwa nguvu ninaipaza, wote wapate sikia,
  Haya nayo waeleza, yaweze kuwaingia,
  Sauti yangu!

  ReplyDelete