Friday, August 26, 2011

Moyoni unatawala

Nasema kila wasaa, maneno nitarudia,
Kamwe sitoyakataa, haya nayosimulia,
Moyoni ushanijaa, moyoni ushaingia,
Moyoni unatawala.

Moyoni mwangu wang'aa, tuli tuli watulia,
Nakupenda wewe maa, hakuna 'nokufikia,
Neno langu si hadaa, leo kweli nakwambia,
Moyoni unatawala.

Silali wala kukaa, pasina kufikiria,
Wewe ndo wewe haswaa, ndotoni naenijia,
Moyo tanienda paa, siku ukinikimbia,
Moyoni unatawala.

Wengine wote kataa, wache kukufatilia,
Mwambie wazi hataa, moyoni 'jakuingia,
Wabaki wakishangaa, sisi tukifurahia,
Moyoni unatawala.

Unatawala kiwaa, dobo na numbula pia,
Bora nikae na njaa, ila kwako kutulia,
Wewe hunayo mawaa, kwa raha nonipatia,
Moyoni unatawala.

7 comments:

 1. @ Fadhy.....

  Moyoni mwako kajaa, tena kina kazamia
  Sasa nini wazubaa, fumbata zako khisia
  Wengine kija mtwaa, na nani utaja lia?
  Moyoni nokutawala!

  Moyoni nokutawala, tena shinda 'malkia'
  Usokaa na kulala, wazimu keshakutia
  Sirefushe mjadala, 'kete' watakuzidia
  Moyoni nokutawala!

  'Wengine wote kataa, wache kukufatilia'
  Vyema awe kazubaa, mjini hajaingia
  Taachwa kwenye mataa, na vyako keshakulia
  Moyoni nokutawala!

  ReplyDelete
 2. Hallyie.....

  Moyoni mwangu kajaa, kwake ninajivunia,
  Ye kwangu ndie staa, hakuna nomfikia,
  Nilishasema ahaa, penzi nalonipatia,
  Jamani raha!

  ReplyDelete
 3. @ Fadhy....

  Kumbe mshazoweana, matendo pamwe tabia
  Raha mnazopeana, sinacho cha kuchangia
  Waombea 'Sub-hana', yenye kheri wajalia
  Kupenda mkapendana, ndipo penzi huvutia!

  ReplyDelete
 4. Ni furaha kusikia na kusoma kuwa una wako alojaa moyoni pia autawala moyo wako. Mtani ...Nakutakia kila la kheri.

  ReplyDelete
 5. Hallyie.....

  Japo namwona ndotoni, siachi kumuwazia,
  Niwapo usingizini, daima ye hunijia,
  Aniweke furahani, niyashinde ya dunia,
  Angali anatawala!

  ReplyDelete
 6. Yasinta....

  Mapenzi yana raha,
  Huleta nyingi furaha,
  Anayesema ni karaha,
  Kwa hakika hayajui.

  ReplyDelete
 7. wow! hakika umesema
  mapenzi ni kidonda
  na yana nguvu kuliko mauti
  Kweli kipenda roho hula nyama mbichi.

  ReplyDelete