Friday, August 26, 2011

Moyoni unatawala

Nasema kila wasaa, maneno nitarudia,
Kamwe sitoyakataa, haya nayosimulia,
Moyoni ushanijaa, moyoni ushaingia,
Moyoni unatawala.

Moyoni mwangu wang'aa, tuli tuli watulia,
Nakupenda wewe maa, hakuna 'nokufikia,
Neno langu si hadaa, leo kweli nakwambia,
Moyoni unatawala.

Silali wala kukaa, pasina kufikiria,
Wewe ndo wewe haswaa, ndotoni naenijia,
Moyo tanienda paa, siku ukinikimbia,
Moyoni unatawala.

Wengine wote kataa, wache kukufatilia,
Mwambie wazi hataa, moyoni 'jakuingia,
Wabaki wakishangaa, sisi tukifurahia,
Moyoni unatawala.

Unatawala kiwaa, dobo na numbula pia,
Bora nikae na njaa, ila kwako kutulia,
Wewe hunayo mawaa, kwa raha nonipatia,
Moyoni unatawala.

Thursday, August 25, 2011

Sauti yangu

Ninataka kuipaza, ilokaza,
Kotekote kueneza, nacho waza,
Wote muje kusikiza, mkiweza,
Nayoeleza!

Kuna mambo yanikwaza, yanumiza,
Kukimya sitokuweza, tonyamaza,
Silali kucha nawaza, nahasiza,
Wanichagiza!

Niaje yazidi oza, yachakaza,
Vyote vyema wamaliza, wakombeza,
Ni lini watabakiza, wandekeza,
Mauzauza!

Sauti yangu napaza, nakataza,
Mola fimbo wacharaza, tena kaza,
Wajutie wao kwanza, wamaliza,
Wavokombeza!

Wednesday, August 3, 2011

Waambie

Ukiwa nao waambie, maneno yawafikie,
Jitahidi wasikie, ujumbe uwafikie,
Ili wasiulizie, bure wasijisumbue,
Waambie hao wote, umenichagua mie.

Wakate vyao vilimi, ikibidi waumie,
Sema wanipenda mimi, waambie wasikie,
Sema mara kumi kumi, sauti iwafikie,
Waambie hao wote, kuwa wanipenda mie.

Hawapendi ninajua, we’ waache waumie,
Wivu unawasumbua, watamani watibue,
Sie tunaomba dua, Muumba atujalie,
Waambie hao wote, umenichagua mi.

Waambie wafitini, na chuki zao walie,
Na wala wasijihini, hawatotuweza sie,
Tumeshazama dimbwini, tumeshanogewa sie,
Waambie hao wote, kuwa wanipenda mie.

We’ waambie mpenzi, yawachome waumie,
Na zidisha kunienzi, ili nifaidi mie,
Niyafaidi mapenzi, pendolo nijivunie,
Waambie hao wote, umenichagua mie.

Mpenzi we’ u mzuri, yeyote asikwambie,
Unanipa ufahari, na raha usisikie,
Nasi twombeane kheri, mapenzi yetu yakue,
Waambie hao wote, kuwa wanipenda mie.

Waseme hata wachoke, wacha tupendane sie,
Kote kote wazunguke, watashindwa wajijue,
Na watake wasitake, siye tuyafurahie,
Waambie hao wote, umenichagua mie.

Hata washikwe na wivu, wenyewe nd’o waumie,
Sie twala zetu mbivu, watwache tufurahie,
Wayapate maumivu, mioyoni waumie,
Waambie hao wote, kuwa wanipenda mie.

Watayasema mchana, ngoja giza liingie,
Watalala tena sana, na ndoto ziwasumbue,
Tutazidi kupendana, watakoma wakomae,
Waambie hao wote, umenichagua mie.

Hujachagua mwingine, isipokuwa ni mie,
Hivyo nasi tupendane, raha na tujipatie,
Wao wahangaishane, sie wasitufikie,
Waambie hao wote, kuwa wanipenda mie.

Waambie wasikie, nenolo liwainngie,
Tena wasijisumbue, mapenzi ni yetu sie,
Waumie siumie, tunajivinjari sie,
Waambie hao wote, umenichagua mie.

Waambie wasikie!