Wednesday, July 20, 2011

Usingizi siupati

Usiku mie silali, sina hali,
Mwenziyo sinayo khali, hata sili,
Chakula mwenziyo sili, ni ukweli,
Nakuwaza wewe!

Usingizi siupati, wa manati,
Zito langu blanketi, bati bati,
Nawaza kila wakati, varangati,
Wewe upo mbali!

Bora 'ngekuwa karibu, eeh muhibu,
Yatoke yan'onisibu, masahibu,
Penzi lisiniadhibu, kwa irabu,
Kwako nimefika!

Mwingine mie simwoni, hakya nani,
Watawala mawazoni, na moyoni,
Nikutunze kama mboni, ya thamani,
Uwe furahani!

12 comments:

 1. Kisa nini kujidhili, yupo mbali
  Mpaka ukawa huli, dhofu hali
  Na usingizi hulali, sema kweli!
  Juwa kikosa kauli, kwisha 'dili'

  Walala kiweweseka, kosa njozi
  Huku kule kigeuka, macho wazi
  Yupo mbali metamka, kaza uzi
  Muda wakati kifika, tabarizi!

  Lau ngekuwa karibu, na muhibu
  Penginge ngekusulubu, ukatubu!
  Hubalo ngekuadhibu, si ajabu
  Hebu nenda taratibu, sijilabu.

  Mwengine katu oneka, ila huyo
  Mawazoni katu toka, na kumoyo
  Ja 'mboni' livyomuweka, au siyo?!
  Mathalani kugeuka, vipi hiyo?

  Mwisho lala kikoroma, kuusia
  Shughulizo kijituma, mara mia
  Tunda lako hatochuma, novizia
  Zidi muomba KARIMA. kutunzia!

  ReplyDelete
 2. Hallyie....

  Mawazo yananijaa, ni balaa,
  Hofu inanivagaa, kama njaa,
  Nahofu 'kija kataa, 'tachakaa,
  Ni balaa!

  Namhitaji mpenzi, sijiwezi,
  Asiwe wa kwenye njozi, bali wazi,
  Moyowe niubarizi, 'eje ezi,
  Kama kazi!

  Wenzake awaambie, wasikie,
  Pendole anipatie, lizidie,
  Kwake ye' nijivunie,'furahie,
  Wangu mie!

  ReplyDelete
 3. Mawazo yasikuzonge,fanya yako
  Mpweke usijitenge, sende huko
  Tawiva ule matonge, mlo wako
  Vumilia!

  Zidi muomba MWENYEZI, kwangazia
  Lopata mema malezi, kujalia
  Maishani akuenzi, nawe pia
  Ni subira!

  Muda siku tafikia, omba duwa
  Njozizo zitatimia, kijaliwa
  Vilo vyako tajilia, kwa muruwa!
  Ipo siku!

  Mazuri siyo haraka, yafanyia
  Yataka kushuwarika, fikiria
  Kasi ukikurupuka, meumia!
  Taratibu!

  'Mpewa hapokonyeki', litwambia
  Kama chako kitabaki, kikutia
  Katu hutopata feki, tia nia
  Furahia!

  ReplyDelete
 4. Maneno umeyasema, ya hekima,
  Yan'oujaza mtima, yote mema,
  Ni raha napoyasoma, siku nzima,
  Chenye chema!

  Sihemi na sikohoi, sijijui,
  Na wala sijichukii, si adui,
  Bali moyo ujidai, hui hui,
  Sipumui!

  Mawazoni amenata, ninamwota,
  Mikono naifumbata, ninamwita,
  Chozi aje kunifuta, pata pata,
  Sije pweta!

  ReplyDelete
 5. Huhemi na hukohoi, waishije?
  Na ulipo hujijuwi, wafanyaje
  Si kifo hujazirai, tusemeje?
  Tahadhari!

  Zisiwe za alinacha, nazoota
  Mataani hakuacha, haja juta
  Akautupa m'bacha, kwa unopita
  Tafakari!

  Zidi muomba QAHARI, kuitika
  Mipango iwe mizuri, lonyooka
  Bayana isiwe siri, tualika
  Ni fakhari!

  ReplyDelete
 6. Homa hainishi panda, ninakonda,
  Maana pendo napenda, kama kinda,
  La ubani si kuvunda, ye' ni tunda,
  Tonishinda!

  Usingizi usingizi, wa ajizi,
  Yamenijaa mapenzi, kikohozi,
  Tena sijibaraguzi, nabarizi,
  Kama kazi!

  Na hisia sizichoki, nazikoki,
  Moyo hauelezeki, h'ukwepeki,
  Kwingine tena sitaki, kwa bunduki,
  Kheri nduki!

  ReplyDelete
 7. Kupenda huwa maradhi, kifurutu
  Ukawa mwenye kuridhi, kila kitu
  Sema yanayokuudhi, huthubutu
  Ushapenda!

  Mapenzi yamekujaa, hujiwezi
  Mpofu umepumbaa, kama chizi
  Kesha macho umeng'aa, kweli kazi!
  Ndo kupenda!

  Kweli mapenzi upofu, kichunguza
  Khasa ndo kwanza 'alifu', noyaanza
  Mpaka yakija kifu, keshaoza!
  Shughuli!

  Hisia sikupumbaze, sije feli
  Chochoroni sijibanze, mkabili
  Nokudhili mueleze, mpe kweli
  Jiamini!

  ReplyDelete
 8. Kupenda ndiyo ugonjwa, wa moyoni,
  Kwingine waweza punjwa, si penzini,
  Wengine hata wachinjwa, duniani,
  Naamini!

  Kupenda huleta raha, ukipendwa,
  Tena h'ongeza furaha, moyo kendwa,
  Lakini kuna karaha, ukitendwa,
  Pondwa pondwa!

  Mapenzi yanaadhibu, makusudi,
  Mtu akikughilibu, ukaidi,
  Hayafai mwenye gubu, kedi kedi,
  Si mweledi!

  Si vema nikawa moja, bora 'wili,
  Siachi kujikongoja, 'tawasili,
  Kungoja ngoja si hoja, kwa akili,
  Tawasali!

  ReplyDelete
 9. Nakuombea salama, awali na akhiria
  Wendako usijekwama, RABI akwangaze njia
  Ni hayo leo nasema, mengi ushamalizia
  Fursa watoyasoma, pengine nao changia.

  ReplyDelete
 10. Hallyie....

  Niyaseme yepi tena, kuonesha shukurani,
  Hakika wewe mwungwana, kakuj'alia Manani,
  Wewe mkali wa vina, pamoja nazo mizani,
  Karibu tena na tena, hapa kwangu jamvini.

  Hakika tuna jukumu, kukikuza Kiswahili,
  Ni lugha yetu adhimu, tuifanye 'fike mbali,
  Utambulisho muhimu, tena ni wenye amali,
  Karibu tena na tena, hapa kwangu jamvini.

  ReplyDelete
 11. Jamvini mekaribia, na kitako nshakaa
  Na ubani ushatia, naitikia 'duwaa'
  Abadani pakimbia, kiwa penye manufaa
  Ila tungo kazania, sio moja mwezi kaa!

  Umenifanya nirudi, moja ombi taka nena
  Kuvutia huna budi, diwaniyo ikafana
  Tungo nyingi jitahidi, mwaga wapenzi ziona
  Hii kichangia 'Iddi', ile changia 'Haruna'

  Ndio raha ya ulumbi, hasa wengi kikutana
  Pakatimka kivumbi, mithili tapapurana
  Ndipo la utunzi wimbi, 'kidau' kikakazana
  Hilo ndilo langu ombi, umuhimu kiliona!

  Nimalize wasalamu, 'alifu' sianzi tena
  Ingawa sijakhitimu, 'kudodosa' takazana
  Kurudi kinilazimu, kwa hili utaniona.
  Nakuombea WADUDI, azma yako kufana.

  ReplyDelete
 12. Hallyie.....

  Hakika nimefurahi, kuona 'merudi tena,
  Tungo zi stafutahi, zingali tele zafana,
  N'amkapo usubuhi, ninawaza kwacho kina,
  Ndiicho chakula changu.

  Sitokuwa nacho choyo, tungo zibaki kichwani,
  Daima niandikayo, yatoka mwangu moyoni,
  Ili yale usomayo, yakuweke furahani,
  Kiiwe chakula chako.

  ReplyDelete