Sunday, July 10, 2011

Yangu kalamu

Nimeshikwa na wazimu, jambo gumu,
Nahitaji kufahamu, mumu humu,
Ni nani nimtuhumu, ana sumu,
I wapi yangu kalamu?

Kitambo sijaandika, kwa hakika,
Kalamu wapi 'meweka, 'taka saka,
Ama ilikwishachoka, takataka,
I wapi yangu kalamu?

Njoo wewe nikwulize, nieleze,
Ilipo nielekeze, 'sin'cheze,
Jambo nataka juze, wasi'kize,
I wapi yangu kalamu?

Isake kwa'yo busara, si hasira,
Visiwani ama Bara, wastara,
Nataka ile imara, ilo bora,
I wapi yangu kalamu?

Iletwe kalamu hima, n'weze sema,
Ifike hapa mapema, 'sije goma,
Sitaki kupata homa, hujasoma,
I wapi yangu kalamu?

5 comments:

 1. Kalamu uliitupa,
  Kadhan' metupa chupa
  Sasa ndo akili imekupa
  Kukumbuka kalamu ulotupa!

  Nenda pale jalalani
  Karibu na pale njiani
  Fukua mle pipani
  Chukua kalamuyo kiganjani!

  ReplyDelete
 2. Nilisoma kichwa cha habari haraka haraka nikifikiri umeandika Yanga Kalamu, nikajiuliza kulikoni, kusoma shairi alaaaaa

  ReplyDelete
 3. Kwa mie wangu uono, sitoapa
  Pengine liisha wino, haitupa
  Au ishiwa maneno, ukakwepa
  Fikiri lipoiweka, kalamuyo!

  ReplyDelete
 4. Naminajiuliza kalamu ya Fadhy Iwapi?

  ReplyDelete
 5. Huna wa kumtuhumu, kati yetu
  Mwenyewe ujilaumu, kila kitu
  La kudhani kuna sumu, sithubutu
  Ilipo yako kalamu, juwa weye!

  Pengine likwisha choka, kuandika
  Hovyo pengine iweka, ikafoka
  Au winowe kauka, wazi weka!
  Ilipo yako kalamu, juwa weye!

  Huna wa kumuuliza, chakarika!
  Mwenyewe unoitunza, uhakika
  Limorandia angaza, kuponyoka
  Ilipo yako kalamu, juwa weye!

  Kwa visiwani na bara, tasumbuka
  Ni kiwango na ubora, vya kushika
  Juwa wake uimara, 'pepa' weka
  Ilipo yako kalamu, juwa weye!

  Himiza letwe kalamu, na haraka
  Sijetunyima utamu,loyasuka
  Kuombea kwa 'RAHIMU', taoneka
  Ilipo yako kalamu, juwa weye!

  ReplyDelete