Saturday, July 30, 2011

Muwe kwangu marafiki

Nahitaji marafiki,
Ambao watanijali, bila unafiki,
Si kwa ajili ya mali, nami nina dhiki,
Bali kwa pendo la kweli, lisilo na taki,
Muwe kwangu marafiki.

Nahitaji marafiki,
Mie ninatawasali, wawe hata laki,
Sitofanya tasihili, kutaka lahiki,
Niombe ardhilhali, kukosa sitaki,
Muwe kwangu marafiki.

Nahitaji marafiki,
Ninamuomba Jalali, nipate lukuki,
Watoke kote mahali, iwe halaiki,
Nitawafanya halili, watatamalaki,
Muwe kwangu marafiki.

Nahitaji marafiki,
Ninawahitaji kweli, muwe marafiki,
Najua mtajamali, ‘sininyweshe hiyo siki,
Siyo maneno makali, nikiishindwa mikiki,
Muwe kwangu marafiki.

Nahitaji marafiki,
Tupendane kila hali, wenye tamaa sitaki,
Naahidi kuwajali, kwazo raha nazo dhiki,
Pamoja tustahimili, yayo maisha mikiki,
Muwe kwangu marafiki.

Nahitaji marafiki,
Nitawafanya aghali, fakhari kuwamiliki,
Duwa zangu mbili mbili, mpate kile na hiki,
Mola wangu tafadhali, wawe wengi halaiki,
Muwe kwangu marafiki.

3 comments:

 1. Rafiki akupendae, tamjuwa penye haja
  Ndo huyo akufaae, tena huja mara moja
  Shida mkalia nae, huku kikupa faraja
  Kisogo akurambae, hata mie sina haja!

  Ambae atakujali, kwa shida na zote raha
  Maudhi na idhilalii, mkapeana nasaha
  Ulivyo hakukubali, cheka tendana mizaha
  Ndio rafiki wa kweli, abadani huto haha.

  Lako halifanya lake, na moyoni likakaa
  Kusabili kilo chake, huridhi ukikitwaa
  Huyo ni wa peke yake, rafiki anaefaa
  Sio walo peke peke, penye kitu ndo hukaa.

  'Fadhy' muomba 'Mwenyezi', kujaliya wanofaa
  Kunusuru wachokozi, walokulia balaa
  Walioshiba malezi, katu hao wakataa
  Ndio wataokuenzi, kwa maombi na 'salaa'

  ReplyDelete
 2. Hallyie....

  Rafiki kitu muhimu, ndani ya haya maisha,
  Ndo maana yanilazimu, tungo kuziwakilisha,
  Ili nao wafahamu, ninavyowathaminisha,
  Rafiki kitu muhimu.

  Hallyie wewe muhimu, rafiki mwenye bashasha,
  Tangu nimekufahamu, wewe wanifurahisha,
  Una mwingi ufahamu, kwao ninajifundisha,
  Ahsante sana rafiki.

  ReplyDelete
 3. Tena katu kugharimu, mpata mwenye bashasha
  Si 'dola' si 'dirhamu', isirafu mara hwisha
  Rafiki mwaweza dumu, ndugu mkawa maisha!
  Ni kumuomba 'Rahimu', wa kheri kukuonyesha.

  Rafiki mwenye upendo, kikosa kufahamisha
  Si wale wenye vishindo, mara hovyo kuendesha
  Wasohimili 'ndo ndo ndo', chururu kulazimisha
  KIbaini huo mwendo, taratibu nampisha!

  Katu si wa maslahi, 'nikacha' yakijakwisha
  Yule wa 'hakki-lillahi', kukerana la-hasha!
  Tonifaa asubuhi, kimfika ntakesha
  Japo sipo nisabahi, najuwa ni wa maisha!

  ReplyDelete