Thursday, July 28, 2011

Mimi kwako nimetuwa

Ndege daima hutua, kwenye mti apendao,
Ndege hatojisumbua, mti auchukiao,
Ndege yeye huchagua, mmea autakao,
Mimi kwako nimetuwa.

Nimeruka miti yote, nimetuwa kwako wewe,
Nipe moyo wako wote, ili kwangu uchanuwe,
Raha kamili nipate, nisiende kwinginewe,
Mimi kwako nimetuwa.

Kwako wewe nimetuwa, mi’ sijamwona mwingine,
Wewe nimekuchaguwa, nahitaji tupendane,
Moyo wangu nautowa, siupeleki kwingine,
Mimi kwako nimetuwa.

Kutuwa nimeridhika, nimeamua mwenyewe,
Ninasema kwa hakika, napenda unielewe,
Mimi kwako nimefika, sifikiri kwinginewe,
Mimi kwako nimetuwa.

Kwako wewe sina shaka, moyo umenituwama,
Namwomba wetu Rabuka, atujalie salama,
Tufurahi na kucheka, pote panapo uzima,
Mimi kwako nimetuwa.

Nawe pia usihofu, kwani u chaguo langu,
Nikupende maradufu, wewe u sehemu yangu,
Naahidi hutokifu, kwenye huu ulimwengu,
Mimi kwako nimetuwa.

Wazia kuhusu mimi, ukihitaji furaha,
Lilo langu sikunyimi, nitakupa lilo weha,
Makumi kwayo makumi, daima uwe na raha,
Mimi kwako nimetuwa.

Mimi nd’o unieleze, yale yanaokusibu,
Kwa upendo nisikize, nitowe yalo majibu,
Njia nikuelekeze, we’ ulo wangu muhibu,
Mimi kwako nimetuwa.

Mimi ndiye ndege wako, kwako nimekwisha tuwa,
Kokote kule twendako, tupendane tavyokuwa,
Tuzishinde chokochoko, zao wanojisumbuwa,
Mimi kwako nimetuwa.

8 comments:

 1. Ndege kafuma kiota, taamaki keshatuwa
  Humo katu hatojuta, kashindwa kujitambuwa
  Haruki kasema hata, nje hendi kudonowa
  Ndege hapo keshatuwa!

  Si Kunguru si Kasuku, hao msije elewa
  Huyu si mfano Kuku, jaani kutwa 'chakuwa'
  Simithilishi Chiriku, kaa kimya asojuwa
  Ndege hapo keshatuwa!

  Ndege mti kupata, kama vile alojuwa!
  Si urimbo akanata, vicheko ingelikuwa
  Anga zote kazipita, madhila keshapumuwa
  Ndege hapo keshatuwa!

  Sasa tena hategeki, msije kujisumbuwa
  Kwa 'manati' hapigiki, katu weza mtunguwa
  Kuruka tena hataki, kama 'kinda' alelewa
  Ndege hapo keshatuwa!

  ReplyDelete
 2. Hallyie....

  Ndege kiota ninacho, moyo umekwisha tuwa,
  Kiota nikipendacho, sina la kunisumbuwa,
  Chema changu chambilecho, sinalo la kuuguwa,
  Ndege hapa nishatuwa!

  Kuruka tena sitaki, kama kinda nalelewa,
  Kujivuna nina haki, maana ninanogewa,
  Furaha ninailaki, ni raha ninapatiwa,
  Ndege hapa nishatuwa!

  ReplyDelete
 3. Endeleeni endeleeeni !

  Hallyie upo?

  ReplyDelete
 4. @ Simon....

  Nipo nimejaa tele, pishi imesingiziwa
  Burudika hili lile, kurasani linotiwa
  Karibishwa vile vile, 'bukheri' utapokewa
  Ndo tumo kuendelea!

  ReplyDelete
 5. @ Fadhy...

  Ndege powa kiotani, ruka kwa kuruhusiwa
  Kama kinda mdomoni, chakula kutafuniwa
  Kinywa katu ona 'soni', kwa mapana kifunuwa
  Kija toweka tunduni, ndege ushajiumbuwa!

  Ndege hadhari vipanga, chochote wanonyakuwa
  Tamba kwenye yako anga, tawi hili lile tuwa
  Huna cha kumanga manga, punje zote mejaziwa
  Leo donowa mpunga, kesho 'uwele' mwagiwa.

  Ndege katu si Kunguru, sofugika noambiwa
  Anoliya 'kwaru-kwaru', sochaguwa pa kutuwa
  Sojuwa kinomdhuru, kumoja asochaguwa
  Ndege jisikie huru, 'kiota' mesabiliwa!

  Ndege mbawa sitanuwe, manyoya hapururuwa
  Kiota chako mwenyewe, vyovyote jifaraguwa
  Humo 'makinda' utowe, sivyo chinjwa nyama liwa
  'tundulo' walibomolewe, 'khalas' ikaja kuwa.

  ReplyDelete
 6. Mtakatifu Simon...

  Kuandika twendelea, nawe furahi moyoni,
  Hujaacha tembelea, tena kutoka zamani,
  Tungo twazokuletea, ni vile twawathamini,
  Nasi tunaendelea!

  Kutusoma usichoke, asubuhi na jioni,
  Watufanya tuandike, tuandike kwa makini,
  Kiswahili kisikike, kote kote duniani,
  Nasi tunaendelea!

  ReplyDelete
 7. Hallyie…

  Ndege miye si kunguru, sinayo damu chachuwa,
  Miye ninao uhuru, uhuru usochezewa,
  Sifanyi nikakufuru, kesho ‘shindwe aminiwa,
  Ndege najiona huru, kiota ‘mesabiliwa!

  Ndege sinayo makuu, japo ‘pepo napepewa,
  Daima ningali juu, vyote vyote hudumiwa,
  Na wala sinayo fluu, ingawa ninatibiwa,
  Ndege nabakia juu, raha zote napatiwa!

  Ndege sishindi na njaa, milo yote napikiwa,
  Ni raha kila wasaa, hadi gere naonewa,
  Mahaba tele kujaa, hadi miye kunogewa,
  Nafurahi kila saa, kwani nimebarikiwa!

  ReplyDelete
 8. Sina tena la nyongeza, isije kuwa balaa
  Tosha nilivyomweleza, sifa sije muhadaa
  Ndege hebu jituliza, kiotani limokaa
  Kunguru kimuigiza, utakosa pa kukaa!

  ReplyDelete