Tuesday, July 26, 2011

Hadi lini?

Ahadi mtazitowa, msizo zitekeleza?
Mambo mtayazodowa, na kisha kuyachagiza?
Tazidi pata madowa, kisha kujibaraguza?
Hadi lini, mtwambie!

Takumbata mafisadi, maovu mkayakuza?
Mtafanya makusudi, wananchi kuwapuza?
Mtaacha ukaidi, ukweli kutueleza?
Hadi lini, mtwambie!

Taleta maendeleo, siyo kujilimbikiza?
Takemea nyendo zao, wale wanotuumiza?
Taviondoa vilio, wagonjwa wan'oj'uguza?
Hadi lini, mtwambie!

Tuwangoje hadi lini, maana mwatuchokeza,
Semeni haya semeni, twataka wasikiliza,
Mwatutesa mioyoni, vidonda vazidi oza,
Hadi lini, mtwambie!

Hadi lini mtwambie, sana 'metunyong'onyeza,
Msitwache tuumie, siku tawatokomeza,
Yafaa mtusikie, nasi mkaja tuguza,
Hadi lini, mtwambie!

Mbona hamna huruma, tamaa tawamaliza,
Mwachota bila kupima, hamjui kubakiza,
Lini mtakuwa wema, taifa kutongamiza,
Hadi lini, mtwambie!

Hatukufundishwa hivyo, Mwalimu 'livyo'lekeza,
Hivyo sasa mfanyavyo, somo mshalipuuza,
Hivi ndivyo mpendavyo, maadili yalooza,
Hadi lini, mtwambie!

Kila siku twawambia, mngali mwajendekeza,
Mmeharibu tabia, watot'wenu mwawafunza,
Nao weharibikia, kila kitu wakombeza,
Hadi lini, mtwambie!

Nani huyo kawaroga, tuje tukamcheteza,
Maana mwamwaga mboga, ugali mwahanikiza,
Mtamaliza maboga, mkabaki mwamwagaza,
Hadi lini, mtwambie!

Hadi lini mtwambie, tumechoka kungojeza,
Hadi lini twandikie, msopenda kusikiza,
Aibu iwaingie, ili muje kutweleza,
Hadi lini, twambieni!

8 comments:

 1. Hapa 'takhuruju' yote, ni nani akusikize?
  Hakifanyiki chochote, bora hilo nikweleze
  Japo wakusanya wote, baragumu upulize
  'Mila' zao rithi yote, ndipo 'ndani' wakwingize!

  ReplyDelete
 2. Hallyie.....

  Bora tu niwakumbushe, japo hawanisikizi,
  Pengine wajekebishe, wawe safi kwenye kazi,
  Wasijisahaulishe, wanakitesa kizazi,
  Leo wanakula vyote, kesho wataishi vipi?

  Tawi mti wakalia, wangali wanalikata,
  Mbona litawangukia, wajitie farang'ata,
  Japo wanafurahia, hawajui nachofata,
  Miye yangu nitasema, kisha namwachia Mola.

  ReplyDelete
 3. @ Fadhy....

  Hayo ya 'Abunuwasi', nini kuyakumbushia?
  Ngeitumia nafasi, shughulizo jifanyia
  Kwa wino na karatasi, nani atakusikia?
  Utapoteza risasi, winda 'vilivyojifia'.

  ReplyDelete
 4. Hallyie.....

  Siwezi nikajighasi, mate kuyamezea,
  Natoa yangu nafsi, ukweli kuusemea,
  Wao wakyona nukusi, wanaweza endelea,
  Ila saa ikifika, hakuna pa kutokea.

  Wazidishe mitikasi, puani tawatokea,
  Wajijazie ukwasi, watashindwa utumia,
  Taposema sasa basi, muda ushawakimbia,
  Ni bora wafanye hima, kabla hawajachelewa.

  ReplyDelete
 5. @ Fadhy...

  Sinalo la kuchangia, nnakhisi 'kuboreka'
  Za visa ngetutungia, na vituko tukacheka
  Siasa mi nasinzia, mara nna weweseka
  Mejaribu kuchangia, sasa 'mtima' chefuka.

  Wenyewe kuwaachia, ingawaje waudhika
  Japo njema yako nia, peke yako hutofika
  'Kimoja' utamumia, na 'chawa' hatobanjika
  Ngeungana kwa mamia, adui ngetetereka!

  Ni kali zako hisia, tena nia umeweka
  Ingawa kinadharia, ramani inasomeka
  Msituni kiingia, hata panzi hatoruka
  Ni muda bado wadia, hapo subira yataka!

  Uzalendo asilia, damuni unachemka
  Haki umo pigania, upendo kuusimika
  Amani sisitizia, kamwe isijetoweka
  Ni wachache tufujia, umma ukaadhibika.

  ReplyDelete
 6. Hallyie.....

  Hunalo la kuchangia, unahisi kuboreka,
  Ingawa unayo nia, mambo kurekebishika,
  Kuna mambo waumia, lakini usharidhika,
  Amka sasa amka, tetea kizazi chako.

  Tetea kizazi chako, na kile kinachokuja,
  Huu ni wajibu wako, jamii inoungoja,
  Kokote kule wendako, sikubali reja reja,
  Amka sasa amka, tetea kizazi chako.

  ReplyDelete
 7. Piga mbizi nchi kavu, nini jilazimishia
  Uweje mkakamavu, juwa hilo taumia
  Wengi wetu si wavivu, khasa tukidhamiria
  Palipo hoja 'chakavu', huna utoambulia!

  ReplyDelete
 8. Hallyie....

  Nitazidi sema wazi, siku watanisikia,
  Wakifanya ubazazi, Mola 'tamshitakia,
  Haki kwetu kama kazi, lazima kupigania,
  Wasaa umeshafika!

  ReplyDelete