Monday, July 25, 2011

Duuh!

Sitaraji jambo jema,
Kama hujawa makini,
Singoje yao huruma,
Jiulize ni ya nini?

Wala usijidanganye,
Ukadhani umefika,
Tena usijichanganye,
Pamoja nao vibaka.

Wao siyo watu wema,
Ni vema kujihadhari,
Kwao wala si salama,
Kumejaa nayo shari.

Sitaraji ihsani,
Kwani hawana fadhila,
Wamejaa nuksani,
Ha’mwogopi hata Mola.

Tuliwapa madaraka,
Kwa hizo ahadi zao,
Wameguka vibaka,
Kujali matumbo yao.

Wameuleta ugumu,
Katika maisha yetu,
Lazima tuwalaumu,
Tuliwapa kura zetu.

Leo wala hawajali,
Watwona hatuna ma’na,
Lazima tuseme kweli,
Kwa marefu na mapana.

Tunataka nani aseme,
Ndipo wao wasikie?
Ama hadi twandamane,
Ndipo wakatufyatue?

Ukweli huwa ukweli,
Hata ungefichwa vipi,
Uwekwe marashi ghali,
Ungali haukwepeki.

Kweli wametuangusha,
Tena kwa anguko kuu,
Bora kujirekebisha,
Majuto ni mjukuu!

13 comments:

 1. Nilidhani maajabu, ona kichwa cha khabari
  Kukifunguwa kitabu, menichanganya mandhari
  Kheri ngetaja 'madubu', sio wapiga kabari
  Kesho hao kwenye nari, dhuluma walosharabu.

  Dhuluma walosharabu, wafisidi mafakiri
  Wasokuwa na aibu, kipanda kwenye viriri
  Huahidi maajabu, tena kwa MOLA hukiri
  Kesho hao kwenye nari, dhuluma waloshamiri.

  Nojali yao matumbo, wasokuwa na khabari
  Wakawapiga vikumbo, juu chini kiwanyari
  Mithili mwanuka shombo, chefukwa wajihadhari
  Kesho hao kwenye nari, dhuluma waloshamiri.

  Hunoga zao 'kalima', msimu ukisha jiri
  Haya yale huyasema, matamu kama sukari
  Nyingi wakishazigema, 'hekaluni' huvinjari
  Kesho hao kwenye nari, dhuluma walokithiri.

  ReplyDelete
 2. Hunoga zao 'kalima', msimu ukisha jiri
  Haya yale huyasema, matamu kama sukari
  Nyingi wakishazigema, 'hekaluni' huvinjari
  Kheri Hallyie mesema, nami naunga mkono.

  Nami naunga mkono, hunikera mafisadi,
  Wenye mioyo sonono, wasozitimiza ahadi,
  Waloyakosa maono, na kujaa ukaidi,
  Wamelala kama pono.

  ReplyDelete
 3. nakubari haya mashairi yametuli. sijui tufanye nini yawafikie wengi

  ReplyDelete
 4. @ Kamala

  Kwani hayawafikii, hujitia hamnazo
  Tuseme hawasikii, juwa zao ndiyo hizo
  Tuahidi watatii, wapate zetu za dezo
  Kishiba vitumbo 'bwii', tukejeli na 'mifyonzo'.

  ReplyDelete
 5. @ Fadhy....

  Wasotambuwa ahadi, kesho zenye kuulizwa
  Tukaulizwa miadi, ni vipi ilitimizwa
  Si yangu ni ya WADUDI, vitabuni meelezwa
  Fisadi sawa gaidi, wote wanateketeza!

  ReplyDelete
 6. @ Kamala....

  Samahani, nadhani ulikusudia...tufanye nini ili yawafikie wengi (Mashairi) au siyo? Kama ni hivyo, nimeghafilika nikajibu kufuatia hayo yaliyoelezwa hapo na Fadhy. Samahani kwa hilo.

  ReplyDelete
 7. Hallyie na Kamala.....

  Twapaza sana sauti, lakini hawasikii,
  Labda kwa manati, ila haisaidii,
  Kuwa 'jumbe hawapati, wala hainiingii,
  Jeuri imewajaa!

  Wananchi wasikie, hilo lina umuhimu,
  Kisha wao waamue, lililo kwao muhimu,
  Haiji wavumilie, wajitie uwazimu,
  Umefikia wasaa!

  Hima hima waamke, la mgambo limelia,
  Kokote wakusanyike, Muumba kumlilia,
  Miujiza itendeke, Mola atavyosikia,
  Atwepushie balaa!

  Atwepushie balaa, lao hawa watawala,
  Wanaozidi kung'aa, kwa neema wan'okula,
  Ilhali twachakaa, tulogeuzwa maghala,
  Wao wapate misaa!

  ReplyDelete
 8. @ Fadhy....

  'Fadhy' sinipe kucheka, il-hali yanaudhi
  Wenyewe tunawavika, majoho si yao hadhi
  Wapisha kwenye 'mikeka', sie chini tukaridhi
  Kumbe wote ni vibaka, hakuna cha 'ustadhi'

  ReplyDelete
 9. Hallyie......

  Nje waweza kucheka, na moyoni unalia,
  Mambo yameharabika, hawanazo tena nia,
  Wamelewa madaraka, imani 'mewaishia,
  Hao viongozi wetu!

  Sitowapa tena kura, kwa uchaguzi ujao,
  Mambo yameshadorora, hakuna maendeleo,
  Twateswa kwa ufukara, kwa hizo tamaa zao,
  Hao viongozi wetu!

  ReplyDelete
 10. Hilo halina papara, wazi ushalieleza
  Siwe wachimba mkwara, shere ukaja 'tuteza'
  Ni msimamo imara imara, hilo kitaka liweza
  Sivyo kamwe ufukara, abadan tokomeza!

  ReplyDelete
 11. Hallyie.....

  Wala sichimbi mkwara, bali nasema ukweli,
  Huwa najawa hasira, hasira zilizo kali,
  Wagenzi sasa warara, waukuu utapeli,
  Kwenye kura walilia, wamepata hawajali.

  Siwataki siwataki, siwataki hata bure,
  Wamejaa uzandiki, hali zetu zidorore,
  Wao wanatamalaki, kwa nini mi nisifure?
  Kura tena sitowapa, wazopata zimetosha.

  ReplyDelete
 12. @ Fadhy....

  Upunguze mumkari, juwa hasira hasara
  Silifanyie kikiri, ivute kwanza subira
  Sije jifanya mahiri, ikakufika idhara
  Mazingira weka shwari, ndipo mwaga zako sera!

  "Siwataki siwataki", linena 'thalatha' marra!
  "Wamejaa uzandiki", wazidi kuwacharura
  Sichukulie hamaki, muungwana ni busara
  Siwachukie 'samaki', kwa kushindwa kuwapara!

  ReplyDelete
 13. Hallyie....

  Wala sifanyi papara, ila ukweli sifichi,
  Kweli hasira hasara, ila nia siiachi,
  Wao hawana busara, pekechi tele pekechi,
  Ila tukikaa kimya, wao wanajisahau.

  Ni vema kuwakumbusha, 'nginevyo watazowea,
  Uduni wasababisha, u'sikini twatopea,
  Ssasa wameshatuchosha, wamezidi kutwonea,
  Tuseme sasa tuseme, pengine watasikia.

  Pengine watasikia, tukizipaza sauti,
  aibu tawaingia, tukiwashika mashati,
  Hivyo wataweka nia, nazo dhamira za dhati,
  Tuwaeleze ukweli, hali imekuwa mbaya.

  ReplyDelete