Saturday, July 16, 2011

Kalamu inaandika

Dada kamwambie kaka, awe na amani,
Wote walohuzunika, kuwa s'onekani,
Kalamu ilotoweka, ipo kibindoni,
Sasa mchakamchaka.

Kalamu inaandika, winowe pomoni,
Usome pasi kuchoka, 'furahi moyoni,
Upate kuelimika, ma'rifa kichwani,
Sote tukijumuika.

Kiswahili chasifika, hata uzunguni,
Na tena kimeshafika, Sudani Kusini,
Lugha 'staarabika, ya watu makini,
Wan'oheshimika.

Karibuni watukuka, sana karibuni,
Sote tukaburudika, tungo kinyumbani,
Karibuni pasi 'choka, hapa jamvini,
Pamoja tukatunguka.

Kalamu haitochoka, 'subuhi jioni,
Labda 'tapotoweka, humu duniani,
Nisiweze kuandika, nimelala chini,
Ila mtahuzunika.

5 comments:

 1. Afadhali meipata, likuwa kitahanani
  Mana kamata kamata, watu hatuelewani
  Na mguu ukakata, 'peni' haiyonekani
  Sasa mchaka mchaka, sijeshindiwa njiani!

  Kalamu sasa charaza, wino ndo upo pomoni
  Ustawishe baraza, ipate jaa wageni
  Vijiweni lojibanza, wote waje maskani
  Raha ya ngoma kucheza, tujimwae uwanjani.

  Lugha ya letu Taifa, kiswahili namba 'wani'
  Duniani ina sifa, sambaa ulimwenguni
  'Baraatu' kuja kufa, ndio kwanza kileleni
  Kiwekwa kimataifa, wabongo mbona mewini!

  'Hewallah' mekaribia, twajisikia nyumbani
  Kutunga tojisikia, wanopenda wataghani
  Za maoni tachangia, na pole zenye huzuni
  Kwa huba wanoumia, ndo hapa maliwazoni.

  'Insha Allah' omba 'Rabuka', mmoja wetu 'Manani'
  Kalamuyo kuandika, sijegomea njiani
  Sikhofu ukitoweka, na siye tupo njiani
  Salama 'Mola' tuweka, sijeingia huzuni.

  Wasalamu nimefika, nasimama kituoni
  Machache nloandika, lipokosa samahani
  Mja sijakamilika, ni mmoja 'Rahmani'
  Kurasa kichangamka, sitojikhini pembeni.

  ReplyDelete
 2. Hallyie....
  Yote umeshayasema,
  Maneno yenye hekima,
  Nami nimekusikia.

  Sitorudia waama,
  Ushairi kuuzima,
  Kimya kujikalia.

  Wale wanopenda soma,
  Ni hapa ndipo kisima,
  Tungo kuzifurahia.

  ReplyDelete
 3. Zimwage za malumbano
  Malenga wamwage wino
  Baraza takuwa nono
  Ndipo tazidi vutia.

  Sisahau za mafumbo
  Za mambo na vijimambo
  Hapo hutokwenda kombo
  Wengi waweza hamia.

  Kadhalika maliwazo
  Na pia za muongozo
  Zilizojaa mavunzo
  Ndizo khasa tarajia.

  ReplyDelete
 4. Hallyie.....

  Kwa hakika wanikosha,
  Hapa leo nitakesha,
  Tungo tele kuzishusha,
  Maana zinavutia.

  Hakika wewe mjuzi,
  Tena wewe mkufunzi,
  Kwako mimi mwanafunzi,
  Ujuzi najichotea.

  Kiswahili ni kitamu,
  Wala hainihishi hamu,
  Tungo zanipa wazimu,
  Ka' maradhi naugua.

  Nayaugua maradhi,
  Ila moyoni ni radhi,
  Kuzikosa sitaradhi,
  Heri kulala na njaa.

  Utunzi maisha yangu,
  Namshukuru sana Mungu,
  Nawashukuru na wenzangu,
  Ambao hufurahia.

  Kiswahili tukikuze,
  Kote tukakieneze,
  Kwa tungo tuwaeleze,
  Lugha ya kujivunia.

  Nawe karibu 'sichoke,
  Tungo bora tuandike,
  Vizazi zikatunzike,
  Wapate zisimulia.

  ReplyDelete
 5. Fadhy....

  Kadhalika sitochoka
  Kalamu yangu kushika
  'Kidau' wino meweka
  Tungozo zisubiria.

  Nilipo ni 'mwanagenzi'
  Vamia hili jahazi
  Sijuwi kupiga mbizi
  'Andanenga' mfikia.

  Kiswahili yetu lugha
  Khasa kwa wanokijuwa
  Lahaja kizichambuwa
  Hamuye katu kwishia!

  Weza uguwa maradhi
  Kunogewa na lafudhi
  Kina ya peke mahadhi
  Kwa tungo kikitumia.

  'Kipaji' utunzi kwangu
  Nitunuku MOLA wangu
  Hushughulika na yangu
  Tunga nikijisikia.

  Umenipa changamoto
  U-mwepesi si mzito
  Ziponda kama kokoto
  Betizo watushushia.

  Asante nikaribisha
  Nawe morali zidisha
  Tungo nyingi zichapisha
  Jamii kuwafikia.

  ReplyDelete