Saturday, July 30, 2011

Muwe kwangu marafiki

Nahitaji marafiki,
Ambao watanijali, bila unafiki,
Si kwa ajili ya mali, nami nina dhiki,
Bali kwa pendo la kweli, lisilo na taki,
Muwe kwangu marafiki.

Nahitaji marafiki,
Mie ninatawasali, wawe hata laki,
Sitofanya tasihili, kutaka lahiki,
Niombe ardhilhali, kukosa sitaki,
Muwe kwangu marafiki.

Nahitaji marafiki,
Ninamuomba Jalali, nipate lukuki,
Watoke kote mahali, iwe halaiki,
Nitawafanya halili, watatamalaki,
Muwe kwangu marafiki.

Nahitaji marafiki,
Ninawahitaji kweli, muwe marafiki,
Najua mtajamali, ‘sininyweshe hiyo siki,
Siyo maneno makali, nikiishindwa mikiki,
Muwe kwangu marafiki.

Nahitaji marafiki,
Tupendane kila hali, wenye tamaa sitaki,
Naahidi kuwajali, kwazo raha nazo dhiki,
Pamoja tustahimili, yayo maisha mikiki,
Muwe kwangu marafiki.

Nahitaji marafiki,
Nitawafanya aghali, fakhari kuwamiliki,
Duwa zangu mbili mbili, mpate kile na hiki,
Mola wangu tafadhali, wawe wengi halaiki,
Muwe kwangu marafiki.

Thursday, July 28, 2011

Mimi kwako nimetuwa

Ndege daima hutua, kwenye mti apendao,
Ndege hatojisumbua, mti auchukiao,
Ndege yeye huchagua, mmea autakao,
Mimi kwako nimetuwa.

Nimeruka miti yote, nimetuwa kwako wewe,
Nipe moyo wako wote, ili kwangu uchanuwe,
Raha kamili nipate, nisiende kwinginewe,
Mimi kwako nimetuwa.

Kwako wewe nimetuwa, mi’ sijamwona mwingine,
Wewe nimekuchaguwa, nahitaji tupendane,
Moyo wangu nautowa, siupeleki kwingine,
Mimi kwako nimetuwa.

Kutuwa nimeridhika, nimeamua mwenyewe,
Ninasema kwa hakika, napenda unielewe,
Mimi kwako nimefika, sifikiri kwinginewe,
Mimi kwako nimetuwa.

Kwako wewe sina shaka, moyo umenituwama,
Namwomba wetu Rabuka, atujalie salama,
Tufurahi na kucheka, pote panapo uzima,
Mimi kwako nimetuwa.

Nawe pia usihofu, kwani u chaguo langu,
Nikupende maradufu, wewe u sehemu yangu,
Naahidi hutokifu, kwenye huu ulimwengu,
Mimi kwako nimetuwa.

Wazia kuhusu mimi, ukihitaji furaha,
Lilo langu sikunyimi, nitakupa lilo weha,
Makumi kwayo makumi, daima uwe na raha,
Mimi kwako nimetuwa.

Mimi nd’o unieleze, yale yanaokusibu,
Kwa upendo nisikize, nitowe yalo majibu,
Njia nikuelekeze, we’ ulo wangu muhibu,
Mimi kwako nimetuwa.

Mimi ndiye ndege wako, kwako nimekwisha tuwa,
Kokote kule twendako, tupendane tavyokuwa,
Tuzishinde chokochoko, zao wanojisumbuwa,
Mimi kwako nimetuwa.

Tuesday, July 26, 2011

Hadi lini?

Ahadi mtazitowa, msizo zitekeleza?
Mambo mtayazodowa, na kisha kuyachagiza?
Tazidi pata madowa, kisha kujibaraguza?
Hadi lini, mtwambie!

Takumbata mafisadi, maovu mkayakuza?
Mtafanya makusudi, wananchi kuwapuza?
Mtaacha ukaidi, ukweli kutueleza?
Hadi lini, mtwambie!

Taleta maendeleo, siyo kujilimbikiza?
Takemea nyendo zao, wale wanotuumiza?
Taviondoa vilio, wagonjwa wan'oj'uguza?
Hadi lini, mtwambie!

Tuwangoje hadi lini, maana mwatuchokeza,
Semeni haya semeni, twataka wasikiliza,
Mwatutesa mioyoni, vidonda vazidi oza,
Hadi lini, mtwambie!

Hadi lini mtwambie, sana 'metunyong'onyeza,
Msitwache tuumie, siku tawatokomeza,
Yafaa mtusikie, nasi mkaja tuguza,
Hadi lini, mtwambie!

Mbona hamna huruma, tamaa tawamaliza,
Mwachota bila kupima, hamjui kubakiza,
Lini mtakuwa wema, taifa kutongamiza,
Hadi lini, mtwambie!

Hatukufundishwa hivyo, Mwalimu 'livyo'lekeza,
Hivyo sasa mfanyavyo, somo mshalipuuza,
Hivi ndivyo mpendavyo, maadili yalooza,
Hadi lini, mtwambie!

Kila siku twawambia, mngali mwajendekeza,
Mmeharibu tabia, watot'wenu mwawafunza,
Nao weharibikia, kila kitu wakombeza,
Hadi lini, mtwambie!

Nani huyo kawaroga, tuje tukamcheteza,
Maana mwamwaga mboga, ugali mwahanikiza,
Mtamaliza maboga, mkabaki mwamwagaza,
Hadi lini, mtwambie!

Hadi lini mtwambie, tumechoka kungojeza,
Hadi lini twandikie, msopenda kusikiza,
Aibu iwaingie, ili muje kutweleza,
Hadi lini, twambieni!

Monday, July 25, 2011

Duuh!

Sitaraji jambo jema,
Kama hujawa makini,
Singoje yao huruma,
Jiulize ni ya nini?

Wala usijidanganye,
Ukadhani umefika,
Tena usijichanganye,
Pamoja nao vibaka.

Wao siyo watu wema,
Ni vema kujihadhari,
Kwao wala si salama,
Kumejaa nayo shari.

Sitaraji ihsani,
Kwani hawana fadhila,
Wamejaa nuksani,
Ha’mwogopi hata Mola.

Tuliwapa madaraka,
Kwa hizo ahadi zao,
Wameguka vibaka,
Kujali matumbo yao.

Wameuleta ugumu,
Katika maisha yetu,
Lazima tuwalaumu,
Tuliwapa kura zetu.

Leo wala hawajali,
Watwona hatuna ma’na,
Lazima tuseme kweli,
Kwa marefu na mapana.

Tunataka nani aseme,
Ndipo wao wasikie?
Ama hadi twandamane,
Ndipo wakatufyatue?

Ukweli huwa ukweli,
Hata ungefichwa vipi,
Uwekwe marashi ghali,
Ungali haukwepeki.

Kweli wametuangusha,
Tena kwa anguko kuu,
Bora kujirekebisha,
Majuto ni mjukuu!

Wednesday, July 20, 2011

Usingizi siupati

Usiku mie silali, sina hali,
Mwenziyo sinayo khali, hata sili,
Chakula mwenziyo sili, ni ukweli,
Nakuwaza wewe!

Usingizi siupati, wa manati,
Zito langu blanketi, bati bati,
Nawaza kila wakati, varangati,
Wewe upo mbali!

Bora 'ngekuwa karibu, eeh muhibu,
Yatoke yan'onisibu, masahibu,
Penzi lisiniadhibu, kwa irabu,
Kwako nimefika!

Mwingine mie simwoni, hakya nani,
Watawala mawazoni, na moyoni,
Nikutunze kama mboni, ya thamani,
Uwe furahani!

Saturday, July 16, 2011

Kalamu inaandika

Dada kamwambie kaka, awe na amani,
Wote walohuzunika, kuwa s'onekani,
Kalamu ilotoweka, ipo kibindoni,
Sasa mchakamchaka.

Kalamu inaandika, winowe pomoni,
Usome pasi kuchoka, 'furahi moyoni,
Upate kuelimika, ma'rifa kichwani,
Sote tukijumuika.

Kiswahili chasifika, hata uzunguni,
Na tena kimeshafika, Sudani Kusini,
Lugha 'staarabika, ya watu makini,
Wan'oheshimika.

Karibuni watukuka, sana karibuni,
Sote tukaburudika, tungo kinyumbani,
Karibuni pasi 'choka, hapa jamvini,
Pamoja tukatunguka.

Kalamu haitochoka, 'subuhi jioni,
Labda 'tapotoweka, humu duniani,
Nisiweze kuandika, nimelala chini,
Ila mtahuzunika.

Sunday, July 10, 2011

Yangu kalamu

Nimeshikwa na wazimu, jambo gumu,
Nahitaji kufahamu, mumu humu,
Ni nani nimtuhumu, ana sumu,
I wapi yangu kalamu?

Kitambo sijaandika, kwa hakika,
Kalamu wapi 'meweka, 'taka saka,
Ama ilikwishachoka, takataka,
I wapi yangu kalamu?

Njoo wewe nikwulize, nieleze,
Ilipo nielekeze, 'sin'cheze,
Jambo nataka juze, wasi'kize,
I wapi yangu kalamu?

Isake kwa'yo busara, si hasira,
Visiwani ama Bara, wastara,
Nataka ile imara, ilo bora,
I wapi yangu kalamu?

Iletwe kalamu hima, n'weze sema,
Ifike hapa mapema, 'sije goma,
Sitaki kupata homa, hujasoma,
I wapi yangu kalamu?