Monday, May 16, 2011

Uwa moyoni mwangu

Unachanua moyoni, wachanua wavutia,
Zaidi ya jasimini, wachanua kuzidia,
Ni fahari yazo mboni, zenye kukuangalia,
U uwa moyoni mwangu.

Wachanua kama waridi, ila wewe wazidia,
Watu hawaishi hodi, uwa walitamania,
Wa radhi walipe kodi, jinsi unavyovutia,
U uwa moyoni mwangu.

Wang'ara wewe wang'ara, wang'ara na kuzidia,
Wang'ara watia fora, wang'ara na kuvutia,
Wang'ara wewe wang'ara, siachi kukuwazia,
U uwa moyoni mwangu.

Hakika una mvuto, yeyote kumzuzua,
Kwa mapenzi motomoto, kukukosa naugua,
Naugua homa nzito, mganga hatoagua,
U uwa moyoni mwangu.

Moyoni wewe ni pambo, pambo linalovutia,
Lililozidi urembo, hata moyo kutulia,
U uwa lenye ulimbo, hata nami kunasia,
U uwa moyoni mwangu.

Moyoni mwangu u uwa, kupata najivunia,
Uwa linonizuzuwa, uwa naloliwazia,
Uwa nililochaguwa, uwa la kufurahia,
U uwa moyoni mwangu.

8 comments:

 1. Mtani wangu hakika ulikuwa umepotea na wenye udhaifu wa mashairi tulikuwa hio kabisa...Naona umerudi na shairi moto moto kweli...Nina imani hilo Ua la moyoni mwako lipo. Na nina hisia ni kweli linastahili hayo yote uliosema. Bonge la sifa uwa limepata. Hongera zake....Kazi nzuri Mtani. Na ni furaha umerudi na kuwa nasi.

  ReplyDelete
 2. Ee malenga karibu, nilidhani u bubu
  Inanibidi nitubu, na kuzinyoa sharubu
  Kukudhania ububu, na kukifunga kitabu
  Nitajinywea ulabu, Diwani kuikaribu

  ReplyDelete
 3. Limezidi asumini, sifaze la hilo uwa
  Ndani pia halioni, waridi mnolijuwa
  Linang'ara kulikoni, almasi noambiwa
  Uwa memeya moyoni, hadhari sije chumiwa!

  Wa peke mvuto wake, huyu yule mzuzuwa
  Sisemi uturi wake, haliudi singiziwa
  Kulikosa homa yake, mahututi weza kuwa
  Uwa memea moyoni, hadhari sije chumiwa!

  Sijechumiwa hadhari, roho kuja kujitowa
  Msije kuliathiri, matawi anza chomowa
  'RABI' uwa lisitiri, na mbegu lije kutowa
  Uwa memea moyoni, hadhari sije chumiwa!

  ReplyDelete
 4. mtani ama kwa hakika nimerejea...sitokuwa tena kigulu na njia hata nikaadimika....tumwombe yeye mwenye kutujaalia haya yote atujalie afya njema tuzidi kuwa pamoja tukiufurahia ushairi huu katika lugha adhimu ya Kiswahilimtani ama kwa hakika nimerejea...sitokuwa tena kigulu na njia hata nikaadimika....tumwombe yeye mwenye kutujaalia haya yote atujalie afya njema tuzidi kuwa pamoja tukiufurahia ushairi huu katika lugha adhimu ya Kiswahili

  ReplyDelete
 5. Eeh Mwanasosholojia,
  Hakika mekaribia,
  Tungo kuwaandikia,
  Na zenu kufurahia.

  ReplyDelete
 6. @Mtakatifu Simon mmmmh!

  @Hallyie
  Ahsante sana kwazo tungo,
  Zilopepetwa kwa ungo,
  Sitousema uwongo,
  Tungozo nafurahia.


  ante sana kwazo tungo,
  Zilopepetwa kwa ungo,
  Sitousema uwongo,
  Tungozo nafurahia.

  ReplyDelete
 7. Asante mefarijika
  Loandika mesomeka
  Tungozo ndizo hakika
  Hapa kuja hafikia.

  ReplyDelete