Thursday, April 7, 2011

Ulimi huponza kichwa

Ulimi kitu kidogo, ila huleta balaa,
Huibua sana zogo, kwao ndugu na jamaa,
Hata kupewa kisago, kuonekana mnaa,
Ulimi huponza kichwa, wahenga walishasema.

Chunga, chunga sana chunga, maneno unoongea,
Sipende sana kuchonga, kila unachokijua,
Vema maneno kutenga, mengine kuyamezea,
Ulimi huponza kichwa, wahenga walishasema.

Katu siwe chakuchaku, domo kama cherehani,
Kubwaja huku na huku, maneno tele sokoni,
Maneno siyo kiduku, yakupe umajinuni,
Ulimi huponza kichwa, wahenga walishasema.

Busara haiji bure, kwa kupenda kuropoka,
Kujipa kiherehere, kila pahala kushika,
Kujitia ubwerere, kinywa chako kufunguka,
Ulimi huponza kichwa, wahenga walishasema.

Ulimi una madhara, bora kujiangalia,
Huziamsha hasira, hata chuki kuingia,
Ulimi ndio kinara, maneno ya kuzushia,
Ulimi huponza kichwa, wahenga walishasema.

Ulimi husababisha, vita watu kupigana,
Maneno kuchonganisha, hata watu kuuana,
Kwa maneno ya kuzusha, jamaa huchukiana,
Ulimi huponza kichwa, wahenga walishasema.

Ulimi u mdomoni, siutoe kila mara,
Vema uuache ndani, kuyaepuka madhara,
Utakuwa na amani, na msimamo imara,
Ulimi huponza kichwa, wahenga walishasema.

1 comment: