Friday, March 25, 2011

Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani

Asifiwe! Asifiwe! sauti zetu sikia,
Asifiwe! Asifiwe! kweli unatusikia?
Asifiwe! Asifiwe! mbona hujaitikia?

Asifiwe umekwenda, dunia 'meikimbia,
Wajua tulikupenda, ila Mungu kazidia,
Mauti yamekutenda, wewe umetangulia,
Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.

Umetwachia majonzi, hakika twakulilia,
Tumejawa na simanzi, hatuwezi elezea,
Mdogo wetu mpenzi, uchungu 'metuachia,
Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.

Ulijawa na adabu, nao ukarimu pia,
Kwa wako utaratibu, ni nuru imepotea,
Umekwenda kama bubu, kwa heri hukutwambia,
Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.

Wewe mtu mwuungwana, kwa njema yako tabia,
Tulikupenda kwa sana, nd'o maana twaumia,
Mfano wako hakuna, kwa pengo kulizibia,
Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.

Kuondoka kwatuliza, kila tukifikiria,
Twatamani tungeweza, kifo tungekizuia,
Mwaka huu kumaliza, nayo inayof'atia,
Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.

Lakini sisi ni nani, Mungu tukamwamulia?
Tukamwuliza kwa nini, wewe amekuchukua?
Mwamuzi ndiye Manani, aloiumba dunia,
Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.

Pengo halitozibika, wewe ulotuachia,
Daima 'takukumbuka, wema'wo kusimulia,
Tukimwomba Rabuka, mwanga kukuangazia,
Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.

Upumzike salama, kwa Mola twakuombea,
Akupe pahala pema, nuru kukuangazia,
Asifiwe mtu mwema, buriani twakwambia,
Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.

Shairi hili nimeliandika maalumu kwa marehemu Asifiwe Ngonyani, mdogo wa kike wa dada yetu, rafiki yetu na mwanablog mwenzetu Yasinta Ngonyani. Asifiwe alipatwa na mauti Jumatano 23.03.2011.
Asifiwe umetuacha kimwili tu, kiroho tungali pamoja nawe. Tunakuombea pumziko salama la milele.
Amina.

6 comments:

 1. Zawadi nzuri hii ya faraja
  Liwazo,tumaini,nguvu na umoja
  Mtanga umenena hujabwajaja
  Kwa Asifiwe aliyefika kwa mja

  ReplyDelete
 2. Nachukua nafasi hii na kusema AHSANTE SANA MTANI WANGU. Nahisi Asifiwe amekusikia kilio chako. Na pia ahsanteni sana kwa wote mloshirikiana nasi bega kwa bega katika kipindi hiki KIGUMU.

  ReplyDelete